Advertisements

Friday, October 5, 2012

NILISAJILIWA YANGA KWA SHILINGI LAKI MOJA TU, ASEMA SAID SUED 'SCUD' ALIYEBOMOA MSIMBAZI MARA MBILI 1991

Said Sued Scud (kushoto) akihojiwa na Mhariri Mtendaji wa Mwanaspoti Frank Sanga nyumbani kwake Kigoma

NA FRANK SANGA, aliyekuwa Kigoma
WAKATI Said Bahanuzi alikuwa mwiba kwa Simba ilipomenyana na Yanga juzi, miaka 21 iliyopita akiwa na umri wa miaka mitatu tu, Yanga ilikuwa na mshambuliaji aliyeongoza mashambulizi dhidi ya Simba. Mpachika mabao huyo kamwe hatasahaulika!

Bahanuzi, ambaye amesajiliwa na Yanga msimu huu akitokea Mtibwa Sugar na moja kwa moja kuwa mfungaji bora katika michuano ya Kombe la Kagame Julai mwaka huu, ndiye aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa penalti katika sare ya 1-1 juzi.


Wakati Bahanuzi akiwa na umri wa miaka mitatu mwaka 1991, kuna kijana alitoka Mkoa wa Kigoma na kusajiliwa Yanga ambako alifanya maajabu na kuweka historia ya aina yake.

Mwaka 1991, Said Sued Scud akiwa na umri wa miaka 24 wakati huo aliweka historia ya aina yake ambayo imeendelea kunasa katika ubongo wa mashabiki wa timu zote mbili, Simba na Yanga.

Scud aliweka rekodi na historia kwa kuifunga Simba bao katika mechi zote mbili za mzunguko wa kwanza na wa pili, na kuifanya Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika kila mechi.

Hakuna raha kama mchezaji wa Yanga kuifunga Simba na hakuna raha kwa mchezaji wa Simba kama kuifunga Yanga. Scud ambaye sasa ana umri wa miaka 45, aliipata raha hiyo mara mbili na bado anapata raha hiyo mpaka sasa.

Uzuri wa kufunga katika mechi za watani ni mchezaji kujijengea jina miongoni mwa wapenzi wa soka nchini na unapofunga mara ya pili hujijengea mashabiki wengi na kuendelea kukumbukwa siku zote.

Scud alifunga bao katika ushindi wa Yanga dhidi ya Simba dakika ya saba katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu Bara), Mei 18, mwaka 1991 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akiwa hana uzoefu wowote wa mechi kubwa, Scud aliyekuwa amesajiliwa kutoka Kurugenzi ya Kigoma iliyokuwa inashiriki Ligi Daraja la Tatu, alifunga tena bao la ushindi katika mechi ambayo Yanga waliifunga Simba bao 1-0 katika mechi ya mzunguko wa pili Agosti 31, 1991 katika Uwanja wa Taifa na kuanzia hapo jina lake limeendelea kutawala mpaka sasa na litaendelea kutawala siku zote.

Said Sued alipewa jina la Scud kutokana na mashuti yake makali yaliyokuwa yakifananishwa na makombora ya Kirusi, ambayo Iraq iliyafanyia marekebisho na kuyatumia katika Vita ya Ghuba mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya kuvamiwa na Marekani.

Kuna maswali mengi ambayo yamekuwa yakiulizwa na mashabiki wa soka. Kwanini Scud aliichezea Yanga msimu mmoja tu, kwanini anasema mabao aliyowafunga Simba hayakuwa bora kwake, yupo wapi sasa, anafanya nini, maisha yake yakoje, anaonaje soka la sasa.

Fuatilia makala haya yaliyofanywa na Mwanaspoti nyumbani kwa Scud mjini Kigoma.

Unayaonaje maisha baada ya soka?
Ni kawaida, nimeyazoea. Sasa najishughulisha na ujasiriamali na nina ng'ombe sita wa maziwa, nina mashamba ya mihogo, mahindi na michikichi. Ninashukuru Mungu maisha yanakwenda vizuri.

Unazungumziaje soka la sasa na enzi zenu? 
Enzi zetu wachezaji wa nje au mapro walikuwa wachache sana, sasa kuna wachezaji wengi wanatoka nje na wanaleta hamasa katika soka letu.

Enzi zetu wachezaji wa nje walikuwa na uwezo mkubwa mathalan William Fahnbullar wa Simba, alikuwa ni mchezaji mwenye kiwango cha juu, hiyo iliifanya hata timu yake kuwa juu, lakini tatizo lilikuwa inapofika kwenye mechi ya Simba na Yanga, alikuwa hapewi pasi na wenzake.

Wachezaji walikuwa wanaoneana wivu kwa sababu walikuwa wanaamini kuwa amesajiliwa kwa pesa nyingi. Hata Yanga ilikuwa hivyo hivyo, alikuwapo Elisha John aliyesajiliwa kutoka Coastal Union kwa pesa nyingi ingawa alikuwa Mtanzania.

Alipokuja Yanga kila mchezaji akawa anampa pasi yeye hata kama amebanwa na mabeki wengi. Lakini jambo kubwa ni kwamba zamani tulikuwa tunafanya mazoezi kwa juhudi kubwa na ndiyo maana wachezaji wengi walikuwa wazuri.

Ungekuwa unacheza mpira sasa ungefanya jambo gani ambalo hukufanya wakati wa enzi zako?

Lazima ningekwenda nje ya nchi kucheza soka. Hata wakati ule nikiwa Yanga nilitakiwa kwenda Kenya kufanya majaribio, lakini kuna baadhi ya viongozi wa Yanga walinizuia.

Katika imani yangu tumekatazwa kuwasema vibaya marehemu, viongozi wengi walionizuia ni marehemu kwa hiyo nisingependa kuwasema kwa ubaya.

Unadhani ulipata masilahi makubwa enzi zako? 
Huwezi kulinganisha na sasa, wenzetu wa sasa wana pesa nyingi na wanapata vitu mbalimbali, mpira wa sasa unalipa vizuri.

Ulinufaika nini kimaisha kuchezea Yanga msimu mmoja tu? 
Nilinufaika sana, namshukuru Mungu kwa yote niliyofanya wakati huo. Mungu anatutaka tushukuru kwa kila jambo.Nilitengeneza marafiki wengi ambao sasa ni kama ndugu zangu.

Nina marafiki wengi Dar es Salaam na mikoa mingine ya nchi. Hilo tu kwangu ni faraja ingawa maisha yangu ni ya kawaida tu.

Ulipoifunga Simba katika mechi zote mbili za mwaka 1991 ulipewa zawadi gani? 

Tulikuwa tunapewa zawadi timu nzima. Hata hivyo, lazima niseme ukweli kuwa nilikuwa napata vizawadi vingi kutoka kwa watu binafsi ambao walikuwa wamefurahia mabao hayo, lakini hakukuwa na zawadi kubwa.

Ulijisikiaje kuifunga Simba mara mbili katika msimu moja? Nilisikia furaha, kwa sababu mechi ya Simba na Yanga ndio humkuza mchezaji. Mpaka leo bado nasikia raha sana kwa kuifunga Simba mechi zote mbili. Unajua kwangu ufungaji upo katika damu, nilikuwa nafunga katika mashindano mbalimbali tangu nikiwa shule ya msingi.

Nilikuwa Mfungaji Bora katika mashindano ya Taifa ya Shule za Msingi ya Umishumta yaliyofanyika mwaka 1986 mjini Arusha na mwaka 1988 mjini Songea.

Baada ya kumalizika mashindano ya Umishumta mjini Songea mwaka 1988 na kuibuka Mfungaji Bora, nilifuatwa na viongozi wa timu ya Majimaji wakitaka kunisajili, lakini kaka alinizuia kwa sababu nilikuwa bado mdogo.

Wakati huo shule za msingi zilikuwa na wachezaji wazuri sana. Nakumbuka Morogoro walikuja katika mashindano hayo na David Mihambo ambaye baadaye alisajiliwa na Simba.

Ni nani alikusajili Yanga na kwa Shilingi ngapi? 
Aliyenisajili Yanga alikuwa ni Alif Azizi wa Kasulu. Azizi alikuwa mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia na alikuwa mpenzi mkubwa wa Yanga. Nilisajiliwa kwa pesa kidogo tu. Nilipewa Shilingi 100,000 (laki moja tu).

Kwanini ulicheza Yanga msimu mmoja tu wa 1990/91? Ni kama vilivyosema awali kwamba imani yangu haitaki niwaseme marehemu vibaya, viongozi wengi wa wakati huo ni marehemu, lakini kwa kifupi ni kwamba walitaka wanisajili halafu waniache dakika za mwisho ili msimu unaofuata nisiwe na timu ya kuchezea.

Lakini kwa bahati nzuri kuna watu walinitonya mapema na ndiyo maana nikagoma kusaini na nikaamua kujiunga na Milambo ya Tabora, huko nikakutana na kina Dadi Phares, Wastara Baribari, Quresh Ufunguo, Job Ayoub Kwasakwasa, Ferouz Teru, Said John na wengineo.

Yanga walivutiwa na nini mpaka kukusajili na walikuona wapi? Ni kama nilivyosema kuwa aliyenipeleka Yanga ni Alif Aziz.

Wakati huo nilikuwa nachezea Kurugenzi ya Kigoma iliyokuwa daraja la tatu, huo ulikuwa msimu wa 1989/90. Lakini nilifahamika vizuri zaidi katika mashindano ya Taifa ya Vijana ya Mwenge yaliyofanyika mjini Tabora ambako mikoa yote ilishiriki.

Nilicheza vizuri sana katika mashindano hayo na katika fainali tuliingia sisi Kigoma na Tabora. Dakika ya kwanza tu niliifunga bao la kuongoza ambalo lilitufanya tushinde mchezo kwa bao 1-0 na kutwaa ubingwa.

Nakumbuka kipa wa Tabora alikuwa Abdul Abbas Wambopa. Nilikuwa Mfungaji Bora katika mashindano hayo. Huko ndiko ambako nilionekana na hata kusajiliwa Yanga.

Ni lipi bao bora ambalo umewahi kufunga katika maisha yako? 
Bao langu bora ni lile ambalo nilifunga katika mchezo ambao Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na Pamba ya Mwanza. Bao la Yanga nilifunga mimi (Scud) na Pamba wakasawazisha dakika za mwisho kupitia kwa Hamza Mponda.

Nilidhani ungeyataja mabao uliyowafunga Simba? 
Hapana! Pamba ilikuwa nzuri sana, ilikuwa imekamilika nafasi zote uwanjani, ilikuwa na wachezaji kama Paul Rwechungura, George Masatu, David Mwakalebela, Deo Mkuki, Mao Mkami, James Washokera, Andrew Godwin, Hussein Marsha, Fumo Felician, Ali Bushir, Hamza Mponda na wengineo.

Nasema hilo ni bao bora kwa sababu tulicheza na timu imara na nilikuwa nimezungukwa na msitu wa mabeki imara wa Pamba, lakini nilifumua shuti kali ambalo lilitinga moja kwa moja wavuni.

Kumbuka kuwa hiyo ilikuwa ni mechi ya tatu tu kwangu ya Ligi Kuu, nilikuwa bado kijana na mgeni, nilifunga bao ambalo naamini ndio bora kwangu.

Kwa hiyo mabao ya Simba yalikuwa ni ya kawaida tu? 
Yale yalikuwa mabao ya kawaida, lakini yana historia kubwa.

Ninachojivunia mabao niliyowafunga Simba ni kuandika historia na kutengeneza rekodi ya mechi ya watani wa jadi, lakini bao bora ni lile ambalo niliwafunga Pamba.

Baada ya kuwafunga Simba mechi ya kwanza, ulifikiria ungefunga tena mechi ya pili? 
Nilitamani sana kuifunga tena Simba, lakini kazi kubwa ilikuwa kwa kocha wetu Syllersaid Mziray ambaye mpaka saa tisa alasiri siku ya mechi ya mzunguko wa pili alikuwa hajui nani acheze kama mshambuliaji. Wakati wa mchana alitangaza kikosi cha wachezaji 10, akasema bado anatafakari mchezaji wa kucheza namba tisa kwa sababu tulikuwa wengi tena wazuri.

Wakati huo Yanga ilikuwa na washambuliaji nikiwamo mimi (Scud), John Mngazija, Ramadhani Kilambo, Joseph Machela na wengineo.
Tuliweka kambi mjini Zanzibar ambako tulicheza mechi mbili za kirafiki tukijiandaa na mechi ya mzunguko wa pili dhidi ya Simba.

Katika mechi hizo mbili nakumbuka nilifunga bao zuri sana katika mechi mojawapo, nimesahau timu ambayo tulicheza nayo nadhani ni Mlandege, lakini Kalambo na Mngazija nao walikuwa wamefunga mabao mazuri, hilo likampa wakati mgumu Mziray kujua nani aanze katika mechi hiyo.

Ilipofika saa kumi jioni tukiwa uwanjani, Mziray akatangaza kuwa mimi nitaanza kama namba tisa katika mechi hiyo. Nashukuru Mungu sikumwangusha kocha wangu, kwani nilifunga bao kama nilivyokuwa nimefanya katika mechi ya mzunguko wa kwanza.

Unaweza kulielezea bao hilo? 
Yanga tulipata kona, wachezaji wengi wakajazana kwenye lango, mimi nikajitoa nikasogea nyuma ya eneo la boksi, baada ya kona kupigwa mpira ukatua kwenye msitu wa wachezaji, baadaye katika kuokoa mpira ukatoka nje ya boksi ambako nilikutana nao na kuachia fataki kali sana ambalo lilijaa wavuni na bao hilo likadumu mpaka mwisho wa mchezo.

Unadhani matarajio yako kisoka yalitimia wakati huo? 
Kila jambo tumepangiwa na Mungu, kwa imani yangu tunaamini kuwa tuna mkataba na Mungu. Kwa hiyo utaratibu wa maisha yangu ulipangwa na Mungu. Namshukuru Mungu kwa yote aliyonifanyia. Naamini malengo yalitimia.

Wachezaji wengi maarufu wanatoka Kigoma, kwanini mkoa huu hauna timu katika Ligi Kuu Bara? 

Kigoma hakuna utawala mzuri wa soka. Hata nchi kama haina utawala mzuri wa soka hatuwezi kufika popote.

Wenzetu Mkoa wa Dodoma walikuwa na utamaduni mzuri. Walikuwa na timu tatu lakini walikuwa na utaratibu wa kuiandaa timu moja kila msimu ili ipande Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na ndiyo maana unaona timu zao zote tatu; CDA, Waziri Mkuu na Kurugenzi zilicheza Ligi Kuu.

Sisi hapa Kigoma tuna uongozi ambao ni wa kisiasa zaidi, watu wenye uwezo wa kuongoza hawapewi nafasi na ndiyo maana tupo tupo tu.

Je hauna mpango wa kusomea ukocha? 
Nilisoma kozi ya awali ya ukocha hapa Kigoma wakati alipokuja Mkufunzi Charles Boniface Mkwasa, nasubiri nisome kozi ya kati ya ukocha na baadaye kozi ya juu.

Una ushauri gani ili kuendeleza soka nchini? 
Ushauri wangu ni kuwataka viongozi wa soka kuanzia ngazi ya kitaifa mpaka mikoani wawathamini wachezaji wa zamani.

Wanatakiwa kuwaendeleza na kuwapa uongozi katika idara mbalimbali kama kamati za ufundi, sioni hilo likifanyika sasa, viongozi wengi ni wabinafsi.

Kuna uhusiano gani kati yako na Hussein Sued?
Yule ni mdogo wangu wa 13, sisi tupo 14 kwa baba na mama. Sasa nasikia anachezea Ruvu Shooting, amepita timu nyingi kuanzia Toto Africa, Yanga, Kagera Sugar na sasa yupo Coastal Union.

Upande wa familia, una watoto wangapi? 
Nina mke mmoja anaitwa Mama Sange, nina watoto saba na mtoto wa kwanza anaitwa Sange, sasa anasoma sekondari. Nataka watoto wangu wote wasome. Kazi za ufugaji na kilimo ninafanya ili niwe na uwezo wa kuwasomesha watoto wangu wote mpaka kiwango watakachofika.

Asante sana, ninafurahia kukutana na wewe. Karibu tena Kigoma

Bin Zubery Blog

No comments: