Advertisements

Friday, April 11, 2014

WAANDISHI WA HABARI WAASWA KUEPUKA KUANDIKA HABARI ZINAZOTOA HUKUMU KATIKA JAMII.

 Mkurugenzi Mkuu wa magazeti ya The Guardian na Nipashe Bw. Kiondo Mshana (kushoto) akizungumza na watendaji wa Idara ya Habari leo jijini Dar es salaam walipomtembelea ofisini kwake eneo la Mwenge kwa lengo la kukuza ushirikiano na kujadili changamoto mbalimbali za tasnia ya habari hapa nchini.
 Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene (katikati) akiwa ameambatana Mkurugenzi Mkuu wa magazeti ya The Guardian na Nipashe Bw. Kiondo Mshana (kulia) kuingia chumba cha habari cha magazeti ya The Guardian na Nipashe alipotembelea ofisini hizo eneo la Mwenge jijini Dar es salaam.
 Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari –Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo (kulia) akisalimiana na Muhariri Mtendaji wa gazeti la The Guardian Bw. Wallace Mauggo(kushoto) mara baada ya kuwasili kwenye chumba cha habari cha gazeti hilo leo jijini Dar es salaam. Katikati ni Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene.
 Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa magazeti ya The Guardian na Nipashe Bw. Kiondo Mshana (kushoto) alipotembelea ofisini za magazeti hayo Mwenge jijini Dar es salaam kwa lengo la kukuza ushirikiano na kujadili changamoto mbalimbali za tasnia ya habari hapa nchini.
 Mpiga Picha Mkuu wa gazeti la Guardian Bw.Seleman Mpochi (kulia) na Muhariri mtendaji wa Gazeti la Nipashe Bi. Frola Wingia wakifuatilia mazungumzo ya Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene alipozitembelea ofisi za magazeti hayo jijini Dar es salaam.
Mwandishi mwandamizi wa gazeti la Guardian Bw. Polycarp Machira (kushoto) na Naibu Muhariri wa gazeti hilo Bw. Wenceslaus Mushi wakifurahia jambo wakati wa mkutano kati ya watendaji wa magazeti ya Guardian na Nipashe na Idara ya Habari.
Picha na 8. Mkurugenzi Mkuu wa magazeti ya The Guardian na Nipashe Bw. Kiondo Mshana akitoa maelezo kwa Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene kuhusu utendaji kazi wa chumba cha habari katika ofisi hizo alipotembelea ofisini za magazeti hayo eneo la Mwenge jijini Dar es salaam.
Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mkuu wa magazeti ya The Guardian na Nipashe Bw. Kiondo Mshana (katikati) na Afisa Habari wa Idara ya Habari Bi. Jovina Bujulu (kushoto) alipotembelea ofisini za magazeti hayo Mwenge jijini Dar es salaam kwa lengo la kukuza ushirikiano na kujadili changamoto mbalimbali za tasnia ya habari hapa nchini.

Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
9/4/2014. Dar es salaam.

Serikali imetoa wito kwa waandishi wa habari kuzingatia weledi taaluma ya habari wanapotekeleza majukumu yao ili kuepuka kuandika habari zinazotoa hukumu juu ya masuala mbalimbali yanayotokea katika jamii na zinazolenga kuwashawishi wananchi  kufanya mambo yasiyokuwa na maslahi kwa taifa.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na msemaji wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Bw. Assah Mwambene alipozitembelea ofisi za magazeti ya The Guardian Ltd na Nipashe yanayochapishwa na kampuni ya IPP Media  kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na watendaji wa magazeti hayo ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa ziara yake katika vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Akizungumza na watendaji wa magazeti hiyo amesema kuwa taaluma ya habari hapa nchini ndiyo inayotoa mwelekeo wa nchi kutokana na umuhimu  ilio nao katika kuihabarisha jamii juu ya masuala mbalimbalimbali yanayotokea nchini na kuongeza kuwa kuwepo wa vyombo vya habari nchini kumechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya sekta mbalimbali nchini
.
Amesema kuwa serikali kwa upande wake inatambua mchango mkubwa unaotolewa na magazeti hayo hapa nchini na kuongeza kuwa  itaendelea kuheshimu na kulinda uhuru wa vyombo vya habari.

“Sisi tunajivunia uwepo wenu kutokana na jukumu kubwa mlilonalo kwa watanzania maana bila ninyi hatuna Idara ya Habari, napenda nitumie fursa hii kuipongeza kampuni ya IPP  hasa wahariri wa gazeti la The Guardian kwa kazi nzuri mnayoifanya kwa kutoa kipaumbele kwa ajenda zenye mustakabali mwema wa taifa letu” Amesema.

Ameeleza kuwa heshima ya vyombo vya habari hususan magazeti hapa nchini haitokani na uchapishaji wa habari zenye lengo la kuuza gazeti bali utoaji wa habari zenye kutoa  kipaumbele juu ya mambo ya msingi na yenye maslahi kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa taaluma ya habari hapa nchini inapaswa kuheshimiwa na waandishi wa habari wenyewe amabao ndio wadau muhimu wa tasnia hiyo kutokana na mchango mkubwa walio nao katika kuleta mabadiliko katika jamii.

“Taaluma ya habari hapa nchini inapaswa kuheshimiwa, kwa upande wetu kama Idara sasa tunatoa msukumo kwa waandishi wa habari kuwa na sifa  na ndio maana tunatoa vitambulisho kwa waandishi wa habari wenye sifa kuhakikisha kuwa wanaofanya kazi ya uandishi wa habari ni wale tu wenye sifa ya kuwa na taaluma ya habari”.

 Kuhusu mchakato unaoendelea nchini wa kupata katiba mpya amesema kuwa vyombo vya habari vinapaswa kuepuka uandishi wa habari zenye ushabiki na uchochezi kutokana na unyeti wa zoezi lenyewe na jinsi linavyogusa maisha ya watu na kusisitiza kuwa vyombo vya habari ndivyo vitakavyoisaidia jamii kujua hali halisi ya mambo yanayotokea katika zoezi hilo.

“Baadhi ya vyombo vimesahau majukumu yake kwa kuanza kuonyesha misimamo kwa kuwaamulia wananchi katika masuala ya msingi hasa kwenye mchakato unaoendelea wa kupata katiba mpya, jambo hili si sahihi naomba tusaidiane katika hili ili tusiwagawe wala kuwachanganya watanzania”

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari –Usajili wa Magazeti Bw. Raphael Hokororo ametoa wito kwa waandishi wa habari kuepuka kuingilia majukumu ya taasisi nyingine kwa kugeuka kuwa mahakama.
“Baadhi ya magazeti hapa nchini wakati mwingine yanageuka kuwa mahakama kwa kuwahukumu watu, huu sio uandishi bora wa habari” Amesisitiza Bw. Hokororo.

Amewataka waandishi wa habari na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini kuzingatia weledi wa taaluma ya habari kwa kuwaachia wanananchi wenyewe kuamua juu ya masuala muhimu yenye mustakabali wa taifa lao badala ya kuwaamulia.

Ametoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha kuwa wanawajengea uwezo waandishi wa habari walio katika vyombo vyao kwa kuwaendeleza kielimu na kuwapatia vifaa vya kisasa ili viweze kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa magazeti hayo Bw. Kiondo Mshana ameushukuru uongozi wa Idara ya Habari kwa kuwa na program ya kuvitembelea vyombo vya habari hapa nchini huku akibainisha kuwa ni fursa ya pekee inayojenga mahusiano mema baina ya serikali na vyombo vya habari.

“Ninashukuru sana kwa ujio wenu  na kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya hapa nchini, kwa upande wetu mmetueleza mambo makubwa, kwetu hii ni shule tosha na tumejifunza mengi kutoka kwenu naomba tuendelee kuwasiliana ili tuifikisha nchi hii mahali pazuri”
Ametoa wito kwa wahariri na waandishi wa habari kote nchini kuzingatia weledi  wa taaluma ya habari kwa kuepuka kuandika habari za hisia na chuki ili kuepusha madhara katika jamii na kusisitiza kuwa atahakikisha vyombo anavyovisimamia vinatanguliza masllahi ya taifa.
“Gazeti la Guardian ni kioo cha jamii , linasomwa na watu wengi ndani na nje ya nchi, mimi kama mkurugenzi mkuu siwezi kuruhusu habari zinazolenga kuwagawa wananchi zisizo na maslahi kwa taifa zichapishwe, taifa  hili ni letu sote machafuko yakitokea nchini hayabagui mwandishi wa habali na asiye mwandishi sote tunapata msukosuko ” Amesisitiza Bw. Mshana.

Kuhusu suala la elimu na maadili kwa wafanyakazi walio chini yake ameeleza kuwa yeye kama kiongozi anaendelea kulipa kipaumbele kwa kutoa msisitizo kwa watumishi wote wa vyombo hivyo kuzingatia maadili ili jamii iendelee kuiheshimu taaluma ya habari.
Naye muhariri Mtendaji wa gazeti hilo Bw. Wallace Mauggo ameiomba serikali kuendelea kuijengea uwezo Idara ya Habari ili iweze kutekeleza majukumu yake bila vikwazo vyovyote kutokana na umuhimu mkubwa ilio nao kwa taifa na tasnia ya habari.

No comments: