Advertisements

Sunday, October 26, 2014

SIMULIZI: Sir Andy Chande: Mwalimu Nyerere aliniomba msamaha

Baada ya wiki iliyopita, mwandishi wa simulizi hizi, Sir Andy Chande kusimulia namna Serikali ilivyotaifisha kampuni kutoka kwa watu wenye asili ya Asia. Sasa endelea…
Lakini Jayli alinizuia akitaka nisipoteze tumaini na kujiingiza kwenye huzuni. Aliongea na mimi kwa upole, umakini na usahihi mkubwa. Giza lilipokuwa likiingia nikaona ninaanza kuelewa. Wakati fulani kwenye mazunguzo yetu aliniambia kama ulikuwa ni mpango wa Mungu vitu vichukuliwe vitarudi siku moja.
Nikaanza kufikiria kuwa inawezekana kulikuwapo na sababu ya Kimungu ya kupitia matatizo, hiyo ndiyo ikawa sababu ya kukaa kimya na kuacha kuchukua maamuzi magumu ambayo baadaye ningekuja kujuta.
Pia Jayli alinisaidia kupata elimu kwa watoto wangu, na kulikuwapo  mfuko wa kusomesha kutoka kwa baba mkwe.
Kwa hiyo kila kitu kikaanza kurudi kwa njia hiyo. Siku iliyofuata nilikwenda kazini kama kawaida. Nikafika pale saa tatu asubuhi, kama ilivyokuwa siku iliyotangulia nikakuta polisi wamelizunguka jengo. Ndani ya jengo kulikuwa na mtu nisiyemfahamu amesimama karibu na meza yangu akichunguza karatasi nilizozitupa kwenye ndoo ya takataka.
Nilipoingia tu aligeuka haraka na kuanza kujitambulisha mwenyewe. Alisema jina lake ni Hironimus Msefya na kwamba ameteuliwa kuwa rais wa kampuni yangu. Nilimuuliza kama alikuwa anataka kuonana na wafanyakazi, lakini alisema hapana.
“Nilitaka kukutana na wewe kwanza” alisema
Nilitumia muda mrefu kuzungumza za Msefya. Baadaye nilibaini kuwa alikuwa ameteuliwa kisiasa kushika nafasi ile, akiwa ni mbunge wa zamani asiyejua lolote kuhusu mambo ya viwanda.
 Baada ya kuondoka ofisini asubuhi ile, bila kujitambulisha kwa wafanyakazi wengine, nilikuwa nikimwona mara chache sana kwenye lile jengo. Baada ya kuondoka niliendelea kupanga karatasi zangu kama kawaida.
Wakati huo huo, huko katika ukumbi wa Karimjee, ikapitishwa rasimu kuhusu utaifishaji mali, aliyeiwasilishwa rasimu hiyo ni waziri wa biashara, Babu.
Rasimu hiyo ilisema kuwa walionyang’anywa viwanda vyao walilipwa fidia na kwamba wafanyakazi hawatalipwa mshahara chini ya uliokuwapo mwanzo. Ili kuhakikisha kuwa utaifishaji una kuwa sawa. Wazo hilo lilipitishwa kuwa sheria siku ile ile wala hakuna mtu aliyepinga.
Niliposikia jambo lile jioni ile, sikuweza kuzuia tabasamu. Kama ningekubali ofa niliyokuwa nimepewa na Mwalimu Nyerere ya kuwa kiongozi wa TANU kule Tabora.
Siku iliyofuata, nilikuwa tayari kuendelea na biashara yangu. Niliwaita wafanyakazi wangu nikawaambia kuhusu mipango yangu ya baadaye. Pia nilitaka kusikia maoni yao. Niliwakuta baadhi ya wafanyakazi Wahindi walikuwapo bado wakihofia muskabari wa maisha yao.
Baadhi ya wafanyakazi Waafrika walipata hofu waliposikia habari kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Serikali. Siku ile jioni niliitwa Ikulu kwenda kuonana na rais. Tofauti na mara ya mwisho alivyoniita, safari hii Mwalimu alikuwa amekaa kwenye ofisini kwake, huku mtu mwingine amekaa kwenye kona.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Rais wa Tanzania, Mwalimu Nyerere hakusimama nilipokuwa naingia kwenye chumba, badala yake alinionyesha kiti cha kukaa karibu yake. Kisha akaanza kikao chetu cha kuomba msamaha. Akaniambia namna gani alivyofikia uamuzi wa kutaifisha kampuni yangu.
Baadaye niligundua kuwa kwa namna Azimio la Arusha lilivyokuwa linafanya kazi ilikuwa ni lazima viwanda vya usagaji vitaifishwe na kuwa mali ya umma. Mwalimu aliniuliza kuhusu mipango yangu ya baadaye kama nilikuwa nayo na ni ipi?
Nilimwambia kuwa kwa mawazo yangu alikuwa amefanya kosa kubwa sana. Utaifishaji haukuwa jibu la matatizo ya uchumi wa Tanzania na kwamba historia itasema ni nani kati yetu alikuwa anasema ukweli.
Mwalimu alikasirika kidogo. “Usijali historia” alisema. “Unataka kufanya nini? Labda kama unataka nafasi serikalini kwenye wizara ya mambo ya nje, nina uhakika hilo linaweza kufanyika haraka,” alisema.
Ulikuwa ni wakati wangu wa kumpa jibu la haraka. Sikuwa nataka kazi wizara ya mambo ya nje ( Hata hivyo, siku chache zilizopita nilikuwa nimekataa kazi UNIDO).
“Nataka kuendelea kumiliki kampuni yangu, kitu cha msingi niruhusiwe tu” nilisema.
Mwalimu alitabasamu akasema “Endelea”. Pia akaongeza kuwa angehakikisha kuwa angesaidia kupatika kwa fidia haraka. Niliondoka na kurudi ofisini kwangu nikawakuta wafanyakazi bado wanasherehekea kutaifishwa kwa kiwanda badala ya kufanya kazi.
Haraka niliitisha kikao na kuwaambia “Ni kweli kampuni sasa inamilikiwa na umma, lakini inamaanisha kuwa inamilikiwa na nyinyi na mimi pia.” Kama wafanyakazi wasingeweza kuendele kufanya kazi maana yake ningekuwa katika hali mbaya.
Niliwataka wafanyakazi waendelee na kazi na tangu siku hiyo, hatukuwa kumbusha tena kufanya kazi. Siku iliyofuata nilijisikia kuchoka kama vile sikuwa nimerudi kwenye biashara kama kawaida.
Siku iliyofuata nilikutana na jambo jingine la kushtua, wakati huu kutoka kwa Waziri wa Fedha, Amir Jamal, Mtanzania mwenye asili ya Asia. Amir alikuwa rafiki wa karibu wa Mwalimu Nyerere. Amir alitaka tuonane kwa ajili ya kupata chakula cha mchana pamoja saa 8:45 mchana nyumbani kwake Seaview.
Nilimwambia kuwa nimekwisha kula, lakini nitakwenda. Mpango wa Amir wa kutaka tukutane kirafiki zaidi ulishindwa. Aliniambia kuwa siku iliyofuata nilitakiwa kuonana na rais, pia alisema kuwa ameteuliwa kusimamia ufuatiliaji wa fidia wa mali za familia ya Chande.
Iliundwa kamati maalumu kwa ajili hiyo,  na kwamba Katibu wa Wizara ya Fedha, Amon Nsekela atakutana na mimi kunipa taarifa zaidi.  Nilimshukuru Amir kwa jambo hilo, nikasubiri simu ya Nsekela.
Hata hivyo, jambo ambalo Amir hakulisema ni kuwa alikuwa amemwambia mhasibu mkuu wa Chande Industries Ltd kutokunipa fedha yoyote mimi au kaka yangu hadi maelezo mengine yatakapotolewa. Maelezo kama hayo pia yalitolewa kwa viwanda vingine vilivyokuwa vimetaifishwa.
Sikushangaa kuwa kamati ya kufuatilia malipo  haraka iliishia kuteuliwa haraka tu. Baada ya wiki kadhaa naibu katibu aliteuliwa kama mwenyekiti wa kamati akiwawakilisha waziri wa fedha na viwanda.
Mwanachama wa mwisho kuteuliwa alikuwa ni Steen Hansen, mhasibu kutoka Denmark aliyekuwa ameletwa na Serikali ya Tanzania kama mshauri, ambaye baadaye alikuja kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ukaguzi Tanzania. Kweli hii ilikuwa habari nzuri kwangu.
Mwananchi

No comments: