Advertisements

Wednesday, June 17, 2015

Risala ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kutoka kwa Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein akitoa Risala ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa Wananchi na Waislamu wote nchini katika Risala hiyo amewataka Wananchi kuwa amani na Utulivu na kuwaombea kwa Mola wetu kuwajaalia Rehma baraka za Mwezi Mtukufu wa Ramadhan pia amewataka kufanya ibada kwa wingi katika kipindi chote cha mwezi huu,(Picha na Ikulu.)

RISALA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN YA RAIS WA
ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI,
MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN,
MWAKA 1426 HIJRIYA, 2015 MILADIYA

BISMILLAHI RAHMANI RAHIM


Ndugu Wananchi,
Assalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatu

Kwa wingi wa heshima na unyenyekevu naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu; Subhana Wataala kwa kutupa rehema na fadhila za kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mara nyengine tena, tukiwa na amani, utulivu na salama nchini. RAMADHAN KARIM.

Mwenyezi Mungu ametujaaliya mwezi wa Ramadhani kuwa ni mwezi bora kuliko miezi mengine. Huu ni mwezi ambao Yeye Mola wetu ameujaza sifa na sharia Zake kwa aya tano za Surat Al – Baqara, kuanzia Aya ya 183 hadi Aya ya 187. Katika Aya 185 ya Sura hii, Mwenyezi Mungu ameusifu mwezi wa Ramadhani kwa kusema:

“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa katika mwezi huo hii Kurani ili iwe uongozi kwa watu, na hoja zilizo wazi na uongozi wa upambanuzi (wa baina ya haki na batili).”

Huo ni moja ya Utukufu wa Mwezi wa Ramadhani ambapo Ibada za waja huwa na fadhila kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, tuna wajibu wa kujiandaa na kuweka azma ya kuzidisha Ibada kwa wingi ikiwa ni pamoja na kufanya mambo yote ya kheri, kusali sala za faradhi na sunna na kujifunza na kusoma sana Kurani. Tukumbuke kuwa huu ni mwezi iliyoteremshwa Kurani. Kwa hivyo, kusoma Kurani na kuzingatia mafunzo yake kuna fadhila kubwa. Kadhalika, Aya tulioitaja inatubainishia kuwa Kurani ni uongozi ulio wazi, wa kubaini mambo mabaya tukayaacha na mambo mema tukayaendeleza, ili tuweze kufanikiwa hapa Duniani na kesho Akhera.

Ndugu Wananchi,
Ramadhani ni mwezi wa rehema na tunahitajiwa tuzidishe vitendo vya kufanya wema kwa wenzetu, katika biashara na mambo mengine. Aidha, Kurani inatufundisha maadili mema ikiwemo kuwa na moyo wa huruma na kuwasamehe wengine, hasa katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. Pamoja na mambo hayo tunahimizwa kutoa sadaka na kufunga. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa waumini wa kweli na wenye kutekeleza mafundisho ya Kurani kama ilivyoelezwa katika Aya ya 92 ya Surat Al – Imran.

“Hamtaweza kuufikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda (nguo, vyakula, pesa) na chochote mnachokitoa, basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua”. Tukumbuke kila tunapotoa, Mola wetu atalipa kheri na hayo yameelezwa sana katika Qurani na Hadithi za Bwana Mtume (S.A.W).

Kadhalika, Mola wetu (SW) ametuambia katika Surat Sab’a, Aya 39 (Juzuu ya 22), yenye tafsiri isemayo:
“Na chochote mtakachotoa basi Yeye Atakilipa; naye ni Mbora wa wanaoruzuku”.

Kwa hivyo, huu ni wakati wa kuwafikiria wengine, hasa wale wenye mahitaji katika kutekeleza saumu zao ili nao waone rehema za Ramadhani. Hili si jambo linalowahusu matajiri au wenye vyeo peke yao. Hazrat Abu Zarri amesema:
“Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W) amesema, usifikirie kuwa kila kitendo kidogo kabisa cha wema ni kuwa kidogo”.

Kila anayetoa basi ajue malipo yake ni makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni vyema kutoa kwa kuwapa wanaohitaji hasa kwa jamaa, majirani, marafiki na kadhalika.

Ndugu Wananchi,
Katika mazingatio ya kufanya wema (ihsani), na kufuata maadili, yanayotukuzwa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, tunapaswa tuzingatie umuhimu wa kudumisha na kukuza amani na utulivu. Ibada ya saumu inahitaji kuwepo kwa utulivu wa nafsi ili kuwapa watu wasaa wa kuitekeleza Ibada hii yenye malipo makubwa kwa Mwenyezi Mungu. Katika kuifikia hali hii, sote tuna wajibu wa kusimamia amani na utulivu ili utekelezaji wa ibada zetu usiathirike. Katika kufunga yapo mambo ya kuharibu funga (saumu) ya mfungaji. Miongoni mwa mambo hayo ni kusema uongo na kuwafitini watu. Kwa hivyo, tujiepushe na mambo ya aina hiyo. Lakini, badala yake, tuzidishe mapenzi baina yetu, tuhurumiane na tusaidiane katika mambo yote ya kheri. Tuendeleze utamaduni wetu wa kula pamoja, kufutarishana na kupelekeana vyakula vya tunu. Mambo haya yana umuhimu katika kuendeleza mila na tamaduni njema za Wazanzibari. Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kuyafanya hayo.

Wakati huo huo, nawanasihi wenye kumiliki mikahawa washirikiane na waumini wanaoutukuza Mwezi huu Mtukufu katika kuondoa kero ambazo zinaweza kuwasababishia karaha wanapoitekeleza ibada ya funga. Tudumishe utamaduni wetu wa kuheshimu dini. Jambo ambalo limechangia kudumu kwa amani ya nchi yetu tangu kale na dahari. Kila mmoja anapaswa kuhakikisha kuwa Mwezi wa Ramadhani unaheshimiwa kwa vitendo. Kadhalika, wazazi nao wanapaswa wawe waangalifu kwa watoto wao nyakati za usiku, ili wawe na nyendo njema pamoja na kuwashajihisha kufanya ibada na kuhudhuria darsa misikitini.

Vile vile, vyombo vyetu vya ulinzi havina budi viimarishe doria za ulinzi katika maeneo yetu mbali mbali, hasa kwa wakati ambao watu wengine wanakuwa katika shughuli za Ibada. Zaidi ya hao, nawakumbusha madereva wazingatie sheria za usalama wa barabarani kwa kutoendesha gari na vyombo vyengine kwa mwendo wa kasi; kwa kisingizio cha kutaka watu wawahi kufutari na kupakia abiria zaidi, jambo ambalo huhatarisha usalama wao. Askari wa usalama barabarani na taasisi nyengine zinazohusika zina wajibu wa kulisimamia suala hili ipasavyo.

Ndugu Wananchi,
Kama tunavyofahamu, kwamba mahitaji huwa ni mengi zaidi katika mwezi wa RamadhanI. Kwa baraka za Mwenyezi Mungu, tulijaaliwa kupata mvua ambazo wakulima walizitumia vyema na tumeweza kupata mazao mbali mbali ya chakula yakiwemo yale ambayo huwa yanatumika kwa wingi katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Sambamba na hilo, Serikali imeendelea kushirikiana na wafanyabiashara wetu katika utekelezaji wa sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kutoa unafuu wa kodi katika uingizaji nchini wa bidhaa muhimu za chakula ikiwemo mchele, unga wa ngano, sukari na tende. Lengo la uamuzi huu wa Serikali ni kuhakikisha kuwa chakula cha kutosha kinakuwepo katika kipindi chote cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kinapatikana kwa bei nafuu.

Ndugu Wananchi,
Kama nilivyoeleza katika miaka iliyopita, napenda nitumie fursa hii tena kwa mwaka huu niwakumbushe wafanyabiashara wote kuwa msipandishe bei za bidhaa zenu bila ya sababu za msingi. Wafanyabiashara wasivutiwe na kutaka kupata faida kubwa, bali wawafikirie zaidi wananchi wenzao. Si jambo la busara kuutumia mwezi huu kwa kuwapandishia bei wananchi, hasa wanyonge. Hatua hiyo ni kinyume na malengo ya Serikali ya kupunguza unafuu wa kodi kwa bidhaa za chakula. Kwa bahati mbaya wapo baadhi ya wakulima wenye tamaa ambao huamua kuleta sokoni mazao ambayo hayajapea. Wakulima hawa si waadilifu kwa hivyo, taasisi zinazohusika zina wajibu wa kusimamia taratibu na utekelezaji wa Sheria ya kumlinda mtumiaji, ikiwa ni pamoja na kuwaepusha kuuziwa bidhaa ambazo muda wake wa matumizi umemalizika.

Ni dhahiri kuwa katika Mwezi wa Ramadhani shughuli za biashara huimarika zaidi. Nawanasihi wafanyabiashara kuendelea kuzingatia sheria. Biashara zote zifanywe katika maeneo yaliyoruhusiwa ili kuepusha usumbufu na msongamano usio wa lazima. Kadhalika, wafanyabiashara pamoja na wafanyakazi wa Baraza la Manispaa kwa mji wa Unguja na Mabaraza ya Miji ya Pemba, waongeze juhudi zao katika kuimarisha usafi wa miji yetu. Uzoefu unaonesha kuwa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani taka huwa zinaongezeka. Kwa hivyo, jitihada zaidi zinahitajika katika kuimarisha usafi wa miji yetu. Tukumbuke kwamba Uislamu unahimiza sana unadhifu.

Kama nilivyoiagiza Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA) katika Ramadhani za miaka iliyopita na mwaka huu naiagiza tena ZAWA na Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati kufanya kila jitihada ili iwapatie maji wananchi kwa kutumia magari katika sehemu zote ambazo huduma za maji safi na salama zina upungufu. Natoa wito kwa wananchi washirikiane na Mamlaka hiyo, ili kuifanikisha shughuli hiyo ipasavyo.

Ndugu Wananchi,
Wakati tunapokuwa katika Mwezi Mtukufu, ni vyema tukawa tunazingatia matayarisho ya ibada ya Hija kwa wale wanaokusudia kwenda Hija mwaka huu. Muda uliobaki ni mfupi na kutokana na sheria za sasa za Hija, matayarisho yanalazimika kukamilishwa mapema zaidi mwaka huu. Namuomba Mwenyezi Mungu awape baraka wale wote wanaojiandaa na watakaojaaliwa kwenda kuhiji mwaka huu na awajaalie kheri na safari ya salama.

Ndugu Wananchi,
Napenda nimalizie risala yangu kwa kukutakieni nyote kheri, rehema na Baraka za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Namuomba Mola wetu atupe nguvu na uwezo wa kuendeleza ibada za saumu, na ibada nyengine katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na kudumisha na kuendeleza amani, umoja na mshikamano. Tumuombe Mwenyezi Mungu atujalie Ramadhani njema.

Ahsanteni,
RAMADHAN KARIM

Wassalamu Aleikum Warahmatullahi Wabarakatu

1 comment:

Anonymous said...

Hotuba nzuri. Kheri na baraka Mashallah. Lkn subiri Octoba ifike tushuhudie dhulma na kipigo cha kupasuana vichwa. Ramadhan Kareem.