ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 4, 2015

Wanne wafungua pazia la fomu za urais CCM

Dodoma. Pazia la Chama cha Mapinduzi (CCM) kupata mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba limefunguliwa rasmi jana mjini Dodoma.
Makada wanne walichukua fomu za kuwania nafasi hiyo, huku wakisindikizwa na wapambe wao na kukutana na Katibu wa Oganaizesheni, Dk Mohamed Seif Khatib aliyewakabidhi fomu hizo, katika ofisi za makao makuu ya chama hicho.
Shughuli hiyo ilitawaliwa na kila aina ya mbwembwe, shangwe na shamrashamra, hasa wakati wagombea hao walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari na kueleza mikakati yao ya kwenda Ikulu.
Waliochukua fomu jana ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Balozi wa Kudumu wa Umoja wa Afrika (AU), katika Umoja wa Mataifa (UN), Amina Salum na Mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere.
Wakati makada hao wakitangulia, leo ni zamu ya wengine wakiwamo Makamu wa Rais Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, ambao tofauti na makada wengine, hawakuitisha mikutano ya kutangaza nia.
Kwa mujibu wa ratiba ya jana, mmoja kati ya waliotarajiwa kuchukua fomu alikuwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa lakini alishindwa ikielezwa kuwa alikuwa katika msiba wa Mbunge wa Ukonga, Eugen Mwaiposa.
Mbwembwe
Wagombea waliokuwa kivutio tangu katika uchukuaji wa fomu hadi kujibu maswali ya wanahabari ni Makongoro na Wasira, huku Profesa Mwandosya akiwaponda wagombea urais wanaojikita kuwaponda wenzao, badala ya kueleza watalifanyia nini Taifa. Mgombea wa kwanza kufika katika ofisi hizo akiwa na msafara wa magari manne na wapambe takriban 100 alikuwa Profesa Mwan dosya. Aliambatana na wabunge, Profesa David Mwakyusa (Rungwe Magharibi), Abdul Marombwa (Kibiti), Aliko Kibona (Ileje), Hilda Ngoye (Viti maalumu) na Mchungaji Lackson Mwanjali (Mbeya Vijijini).
Baadaye alifuatia Wasira, kisha Amina ambaye aliambatana na Mbunge wa Viti maalumu, Anna Abdallah huku Makongoro akifunga pazia la uchukuaji huo wa fomu jana.
Wasira na Profesa Mwandosya waliambatana na wake zao, huku Makongoro na Amina wakiwa na wapambe tu.
Dk Bilal na Dk Magufuli

Uchukuaji wa fomu unaendelea tena leo kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 12 jioni na miongoni wanaotarajiwa ni Dk Bilal, Dk Magufuli, Amos Siyatenzi, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, Balozi Ali Karume na Lowassa.
WanaCCM ambao wametangaza nia ya kugombea urais ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, Profesa Sospeter Muhongo, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mbunge wa Nzega Dk Hamis Kigwangalla.
Profesa Mwandosya
Alitumia dakika 53 katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, kueleza masuala mbalimbali atakayoyafanya iwapo atakuwa rais. Mbali ya kukerwa na wanaowaponda wenzao akiwataka kueleza watalifanyia nini Taifa, alisema: “Kuchukua fomu leo (jana) ni hatua ya kuelekea katika jumba jeupe (Ikulu). Uamuzi huu ni mzito lakini nimejiandaa kiakili, kiafya na kimaono.”
Mwandosya ambaye alijitosa kuwania urais mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu, nyuma ya Dk Salim Ahmed Salim na Rais Jakaya Kikwete alisema, “Wagombea wamejitokeza wengi sana. Mimi hii ni mara yangu ya pili na wingi huu unaonyesha ukomavu wa demokrasia.”
Aliposhika nafasi ya tatu 2005, alivishwa taji la shaba, kwamba safari hii atavikwa taji la dhahabu kwa sababu hafikirii kushindwa na kwamba CCM kitampima kwa rekodi yake.
“Sababu kubwa si urais wala mambo yanayofuatana na urais kama kupigiwa ving’ora, misururu ya magari na kupigiwa saluti. Kubwa zaidi ni kukijenga chama. Rais bora atatoka CCM na nitaendelea pale alipoishia Rais Kikwete, nitaondoa umaskini na kuifanya Tanzania kuwa nchi iliyoendelea kwa kujenga misingi imara,” alisema.
Akijibu swali juu ya uzoefu wake na alivyoshindwa kupenya mwaka 2005 alisema: “Imepita miaka 10 tangu niwanie urais, sasa nina uzoefu wa kutosha serikalini ni tofauti na mtu anayetokea nje ya mfumo wa Serikali.”
Akizungumzia ukosefu wa ajira kwa vijana alisema jambo hilo litamalizwa kwa kuwawezesha vijana kujiajiri ili nao waweze kuwaajiri vijana wenzao.
Wasira
Wasira alisema katika kipindi alichotumikia Serikali katika ngazi tofauti ameandaliwa vizuri: “Uchumi wa kisasa ambao haujali maisha ya watu hauna maana.”
Wasira alipoulizwa atawezaje kutekeleza sera ya chama chake ya ujamaa na kujitegemea katika kuifanya nchi kukua kiuchumi alisema, China ni wanachama wa ukomunisti lakini ni miongoni mwa nchi ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa... “Ubepari ni mfumo wa mashindano ambao wananchi maskini hawawezi kuondoka katika umaskini lakini ujamaa unajali maisha ya watu wote.”
Alisema kila wakati nchi inakuwa na vipaumbele vyake na kwamba katika kipindi alichokuwapo serikalini wameweza kuanzisha benki ya kilimo.
“Siyo kwamba tupo kama tulivyokuwa. Umaskini uliokuwapo mwaka 1961 siyo kama uliopo sasa, tumeendelea kupambana nao,” alisema Wasira.
Hata hivyo, alisema bado hawajawekeza vizuri katika kilimo kwa kutilia mkazo kwenye utafiti, umwagiliaji, ugani na mkopo. Kuhusu kukaa muda mrefu serikalini, alisema hiyo hoja, bali mtu amefanya nini?.. “Rais anatakiwa awe na upeo, anayejua historia na kujua mahitaji ya sasa na siku zijazo, hoja si kukaa muda mrefu.”
Alipoulizwa haoni kama historia yake ya kutoka ndani ya chama na kurejea inaweza kumkwamisha, Wassira alisema chama kina misingi, kanuni na taratibu zake: “Hakuna mahali panapoeleza kuwa ukitoka ndani ya chama na kurudi unapewa hukumu ya kifo.”
Kuhusu kauli aliyowahi kuitoa ya kuwa yeye si mvua nchi ilipokumbwa na tatizo la njaa, Wasira aliwataka Watanzania kumwamini kuwa atahimili nafasi ya urais endapo atafanikiwa kuipata.
Amina
Amina ambaye amewahi kuwa waziri alisema ataipeleka Tanzania katika uchumi wa kati na mpango huo utakwenda sambamba na kumaliza kabisa rushwa na ufisadi na kuinua sekta ya viwanda.
Alijikita katika ajenda tatu; uchumi, kupunguza umaskini na kuboresha zaidi huduma za jamii. Alisema ili nchi iweze kupiga hatua, ni lazima kuwepo na viwanda vitakavyowezesha kukua kwa sekta ya kilimo.
“Lazima tubadili aina ya ufanyaji kazi ili tuweze kupata maendeleo. Lazima tuboreshe miundombinu ya reli, barabara na anga. Nchi yetu imekuwa na pengo la wenye nacho na wasionacho na katika kumaliza hili ni lazima tuunganishe elimu na ajira,” alisema.
Kuhusu rushwa alisema lazima iwepo Mahakama maalumu ya kushughulikia kesi za rushwa huku akizungumzia kubana matumizi kwa kuwa na vyanzo vya ndani vya mapato, kuacha kutegemea wafanyabiashara na nchi wahisani.
Makongoro
Makongoro alisema baadhi ya wanachama wa CCM wanapohusika na rushwa na kisha kuhojiwa na vyombo vya dola vilivyowekwa kisheria, wamekuwa wakitoa majibu yasiyoridhisha.
“Kama watu wamekula rushwa na wanatumia nafasi hiyo kama dhamana waliyopewa katika chama kinachosema cheo ni dhamana. Halafu idadi ya watu kama hao inaongezeka kama uyoga hiyo inafanya imani ya watu katika chama iwe ndogo,” alisema.
Alisema ni bahati mbaya kwamba ndani ya CCM kuna makundi ambayo si ya itikadi bali ya uhasama... “Kimsingi makundi haya yanatokana na kuwapo kwa mmoja wao aliyemzidi mwenzie katika kuchota fedha zetu hazina,” alisema.
Alisema hata Rais Jakaya Kikwete anapowaambia wanaCCM waachane na makundi ya uhasama, wasitoe rushwa wala kukiuka utaratibu wamekuwa hawafuati kwa sababu ya usugu. Alisema kuwa atarudisha fomu zake mjini Dodoma Juni 20.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

inasikitisha kuona mgombea urais bwana wasira bado hana uyakinifu wa kutosha, anazidi kupotosha watu. china uchumi wake umekuwa sana mara dufu baada ya kuachana kivitendo na sera za ukomunisti. kwa sasa aangalie vizuri kimaneno china inaitwa nchi ya kikomunisti lakini realistically uchumi wao ni wa mfumo wa ki capitalistic. siasa za ujamaa duniani zimeshafeli na ukiangalia nchi zenye nguvu za kiuchumi na maendeleo zaidi ni nchi za kibepari. sijui kwa nini bado watanzania tunataja ubepari kama stigma wakati ujamaa huo haujatufikisha popote kimaendeleo. upepari umejikita kujitegemea zaidi kimaarifa na kiutendaji wakati ujamaa watu wanaitegemea zaidi serikali iwasaidie na kuwafanyia mambo yao. wakati umefika if we are serious enough to move into another economic level we have to change our economic policies. tumechoka na siasa za umaskini. na swali labda tunasema sisi ni maskini tutawezaje siasa za kitajiri? wealth is created it is not endowed. basically all countries in the world had been poor before they started to be smart to create wealth through different resources. hamuoni nchi kama Hong Kong singapore south korea zimeendelea juzi juzi tu kwa sababu they are too smart na sisi tunaendelea kusota licha ya kuwa na rasilimali nyingi za asili kuliko nchi hizo. shame on us !!!!!!!