Advertisements

Sunday, December 10, 2017

JWTZ yazungumzia kurejeshwa miili ya askari waliokufa DRC

Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa(Picha na Maktaba yetu)

Serikali inashirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) kuhakikisha miili ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa na waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inarejeshwa nchini.
Akizungumzia na waandishi wa habari leo Jumapili Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa amesema miili ya askari hao itarejeshwa nchini kati ya Jumanne Desemba 12, au Jumatano Desemba 13,2017.
Mwakibolwa amesema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano yalidumu kwa saa 13.
Amesema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 wamejeruhiwa na wengine wawili hawajulikani walipo.
Mwakibolwa amesema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu.

Amesema shambulio hilo ni kubwa zaidi kutokea tangu JWTZ ianze kushiriki ulinzi wa amani nchini DRC mwaka 2011.
"Taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha nchini inafanyika chini ya uratibu wa Serikali na Umoja wa Mataifa. JWTZ na Serikali tunaendelea kuchukua hatua stahiki kufuatilia tukio hili ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika," amesema Mwakibolwa.
Amesema tukio hilo halitawavunja moyo JWTZ wala kutetereka kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya nchi bali linawaongezea ari, nguvu, ushupavu na uhodari zaidi katika kutekeleza majukumu yao.
"Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini DRC. Kwa umoja wetu Watanzania tuwaombee dua roho zao zipumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao," amesema.

Chanzo: Mwananchi

No comments: