Advertisements

Wednesday, December 13, 2017

MBUNGE CHADEMA APINGANA VIKALI NA MBOWE

Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu ametoa msimamo unaotofautiana na ule uliotolewa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuhusu ushiriki katika uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani.

Ukawa wamesema kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) haitaahirisha uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani ili kuruhusu majadiliano, hawatashiriki uchaguzi huo. Lakini Komu amesema kufanya hivyo ni kosa kubwa linaloweza kuwaathiri katika chaguzi zijazo.

Viongozi wa Ukawa unaoundwa na Chadema, Chauma, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF waliitaka Nec kuahirisha uchaguzi huo katika majimbo ya Singida Kaskazini, Longido, Songea Mjini na ule wa kata sita ili wadau wapate nafasi ya kujadili kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo kwenye kata 43 vinginevyo hawatashiriki.

Viongozi wa Ukawa; Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; Mwenyekiti wa Baraza Kuu la CUF, Julius Mtatiro; Kaimu Katibu wa Chauma, Eugene Kabendera na Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Danda Juju walitoa msimamo huo juzi lakini jana Komu akizungumza kuhusu uamuzi huo wa Ukawa alisema uamuzi ni halali kwa kuwa umepitia vikao halali, lakini unaweza kujadiliwa.

“Usahihi ni kitu kingine. Hatuko sahihi kususia uchaguzi haya ni mapambano, kwenye vita unapopigana unaonyesha wapi unakosea na kujisahihisha,” alisema mkurugenzi huyo wa fedha wa zamani Chadema.

“Hata hizo kata 43 hatukuonewa kote ndiyo maana tulishinda kata moja tuliyojipanga vizuri, kikubwa tunapaswa kujenga uwezo wetu na kupambana… kama tutasusia je, tumejipangaje kuhakikisha hicho tunachokipigania tutakipata?” alihoji.

Mbunge huyo alisema uamuzi huo unazua maswali mengi kwani CCM itapita katika majimbo yote bila kupingwa... 

“Watapata jukwaa la kueleza mambo yao sisi hatutapata, lakini je, kama huu hatutashiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule wa mwaka 2020 tutashiriki au la, haya ndiyo maswali yanayohitaji majibu.”

Juzi, Mbowe alisema kulikuwa na kasoro nyingi kwenye uchaguzi wa kata 43 ambazo zinahitaji kurekebishwa, lakini mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima katika taarifa yake aliyoitoa jana alisema chama cha siasa kutangaza kugomea uchaguzi hakuwezi kuifanya Tume iuahirishe.

“Ikitokea vyama vikasusa vyote kushiriki kwenye uchaguzi hapo ndipo unaweza kuahirishwa kwa kuwa hakutakuwa na mgombea,” alisema Kailima.

No comments: