Advertisements

Sunday, March 29, 2020

Mwanamke mwenye maambukizi ya corona, anaweza kunyonyesha kwa kuzingatia haya

Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dk. John Jingu akizungumza na maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka katika Kata za mkoa wa Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo kwa wataalam hao juu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis 

By Aurea Simtowe,Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Pamoja na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya corona kuendelea kusambaa duniani, kuna njia ya kumuepusha mtoto anayenyonya asiambukizwe, ofisa programu wa elimu ya afya kwa umma, Dk Tumaini Haonga amesema.

Dk Haonga alisema hayo wakati akitoa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo kwa watendaji wa Idara ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ndani ya jiji la Dar es Salaam.

Hadi jana jioni, idadi ya walioambukizwa virusi vya corona kote duniani ilikuwa ni zaidi ya watu 620,000 huku vifo vikifika zaidi ya watu 28,600 katika nchi 199.

Tanzania imetangaza kugundua watu 14 wenye maambukizi.

Dk Haonga alisema wanawake ambao watabainika kuwa na maambukizi, hawapaswi kuogopa kunyonyesha watoto kwa kudhani ni njia ya kuwakinga.

Alisema badala yake wazingatie wanavyoelekezwa na wataalamu kama kunawa mikono kwa sabuni na kwa kutumia maji yanayotiririka.

“Mama anaruhusiwa kuendela kumnyonyesha mtoto ikiwa ni moja kwa moja au kwa kukamua na mtoto kupewa maziwa na mtu mwingine,” alisema.

“(Hiyo ni) kwa sababu njia pekee ambayo mtoto huweza kupata maambukizi ni sawa na watu wengine, yaani kupitia majimaji baada ya mtu kukohoa au kupiga chafya.”

Alisema sababu nyingine ya m oto kuendelea kuwa salama ni kwamba virusi vya corona haviishi katika maziwa ya mama wala majimaji ya jasho ambalo mtu anatokwa, bali vinaishi katika hewa ya oksijeni ndiyo maana vikimpata mtu hukimbilia moja kwa moja katika mapafu.

Alisema kitu anachopaswa kuzingatia mama mzazi aliyeambukizwa ni kuosha mikono kwa usahihi kwa kutumia sabuni na maji yaliyotiririka na kuziba pua na mdomo kwa kutumia barakoa ili kuhakikisha kuwa hata akikohoa au kupiga chafya virusi havifiki kwa mtoto kupitia majimaji yatakayoruka

“Kwa wale ambao bado hawajapata maambukizi, ni lazima wazingatie usafi kwa kunawa mikono kwa ufasaha kila wanapotaka kunyonyesha ili mtoto asiambukizwe,” alisema Dk Haonga.

Kuhusu wanawake wajawazito alisema ugonjwa huo huweza kuathiri watoto waliomo tumboni kwa sababu wamekuwa wakiwategemea mama zao katika kila kitu, kama hewa na chakula.

“Hii inaonyesha kuwa mtu akiwa na maambukizi yanaweza yakaenda kwa mtoto, lakini ushahidi wa kutosha kuweza kuona ni kwa asilimia ngapi kina mama wajawazito wanaweza wakawaambukiza watoto, hilo bado halijajengwa kwa sababu ugonjwa huo bado ni mpya,” alisema Dk Haonga.

Maelekezo hayo yanaweza kuondoa hofu kwa watu ambao walikuwa wakiamini kuwa kunyonyesha kunaambukiza moja kwa moja ugonjwa huo, kama Ruth Jairo, mkazi wa eneo la Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

“Nilikuwa napata ugumu sana,” alisema Jairo.

“Kila nikitaka kumnyonyesha mtoto, nawaza nina uhakika gani kama atakuwa salama. Nililazimika kukamua kila mara anapotaka kunyonya kwa sababu kazi zangu muda wote niko njiani na kukutana na watu wengi.

“Lakini sasa ninao ujasiri wa kumnyonyesha moja kwa moja bila hofu yoyote.”

No comments: