Advertisements

Saturday, February 27, 2021

MLONGAZILA YAPOKEA WATAALAMU BINGWA KUTOKA CUBA

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila (katikati) Dkt. Julieth Magandi akizungumza mara baada ya kuwapokea wataalamu wa afya kutoka nchini Cuba, kulia ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa Muhimbili-Upanga Bw. Makwaia Makani na kushoto ni kiongozi wa msafara wa wataalamu hao Dkt. Miguel Pino O’Connor.
Wataalamu kutoka Cuba pamoja na baadhi ya viongozi wa MNH-Mloganzila wakisikiliza taarifa ya hospitali iliyotolewa na Dkt. Magandi.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Sis. Redemptha Matindi (wa kwanza kushoto) akiongoza wataalamu kutoka Cuba kutembelea maeneo mbalimbali ya kutolea huduma hospitalini hapa.
Daktari Bingwa wa Radiolojia Irene Mhalu akitoa ufafanuzi kuhusu huduma za CT-Scan zinavyofanyika katika Hospitali ya Mloganzila.

Hospitali ya Taifa ya Muhimbili –Mloganzila imewapokea wataalamu bingwa 10 kutoka nchini Cuba ikiwa ni mikakati yake ya kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya hususani huduma za kibingwa.

Kaimu Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Julieth Magandi amesema wataalamu hao ni wa uuguzi, usingizi, madaktari wa wodi za wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu na wa upasuaji wa macho (Oculoplastic Surgery).

“Hii ni hatua muhimu sana kwa hospitali yetu na taifa kwa ujumla kwani wataalamu hawa wamekuja wakati muafaka ikiwa hospitali inaendelea kufanya maboresho ya utoaji wa huduma za afya hivyo uwepo wao ni hatua nzuri ya kuendelea kuwapatia ujuzi zaidi wataalamu wetu na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi amefafanua Dkt. Magandi.

Kwa mujibu wa Dkt. Magandi uwepo wa wataalamu hao utaongeza nguvu kazi katika maeneo mbalimbali ya huduma ambapo watakuwa nchini kwa muda wa miaka miwili.

Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ina jumla ya vitanda 608, kwa siku inahudumia wagonjwa wa nje 450 hadi 500 na wagonjwa wa ndani 350 hadi 400, huku ikiwa na vyumba vya upasuaji 13.

Kwa upande wake kiongozi wa msafara wa wataalamu hao Dkt. Miguel Pino O’Connor amesema wapo tayari kufanya kazi, kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo watalamu wa Muhimbili -Mloganzila katika maeneo mbalimbali watakayokuwa wakitoa huduma.

Wataalamu hao wametembelea baadhi ya maeneo ya kutolea huduma ikiwemo Idara ya Magonjwa ya Dharura, wodini, Radiolojia na wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu( ICU).

No comments: