ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 12, 2022

WAZIRI MBARAWA AWATAKA MAKANDARASI KUCHANGAMKIA FURSA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa, akizungumza na Makandarasi (hawapo pichani), katika mkutano wa mwaka wa mashauriano uliofanyika jijini Dodoma
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Eng. Consolatha Ngimbwa, akitoa taarifa ya utekelezaji wa Bodi hiyo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa (hayupo pichani), katika mkutano wa mwaka wa mashauriano wa makandarasi uliofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya wadau wa Sekta ya Ujenzi walioshiriki mkutano wa mwaka wa mashauriano wa Bodi ya Usajili ya Makanadarasi (CRB), wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (hayupo pichani) alipofungua mkutano huo jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akipata maelezo katika Banda la Brela wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa mashauriano uliofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Eng. Aisha Amour, akisalimiana na Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Rhoben Nkori, katika mkutano wa mwaka wa mashauriano wa Bodi hiyo uliowakutanisha makandarasi na wadau wa Sekta ya Ujenzi, jijini Dodoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa (wa tatu kulia kwa waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi katika mkutano wa mwaka wa mashauriano, jijini Dodoma.


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameitaka Bodi ya Usajili ya Makandarasi (CRB), kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa wakandarasi wazawa kujenga miradi kwa viwango bora na kuikamilisha kwa wakati.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa mwaka wa mashauriano wenye kauli mbiu “Umuhimu wa Mchango wa Makandarasi Katika Uchumi wa Tanzania” Prof. Mbarawa amesema Serikali inapenda kufanya kazi na Makandarasi wazawa na itahakikisha mapendekezo yote yanayotolewa na CRB yanafanyiwa kazi kwa wakati.

“Jipangeni muwe na uwezo wa kusimamia miradi ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa nasi tutawapa kazi”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Waziri Mbarawa amewataka CRB kufanya tafiti ili kujiridhisha kama utendaji kazi wa ‘force account’ na ule wa wakandarasi wadogo upi unaleta matokeo chanya kwa Serikali.

Waziri Prof. Mbarawa ameahidi kufuatilia utaratibu wa dhamana kwa wakandarasi ili kuweka mazingira nafuu ya dhamana za Benki na Bima ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali nchini.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Eng. Consolatha Ngimbwa, ameiomba Serikali kutoa fursa nyingi za ujenzi kwa makandarasi wanaohusika na ujenzi wapatao 4,500 sawa na asilimia 36 ya makandarasi wote ili kuhuisha Sekta ya Ujenzi ambao imeathririka kutoka na uwepo wa ujenzi unaotumia ‘force account’.

Eng. Ngimbwa amewataka Makandarasi kushirikiana ili kujengana uwezo na kuiomba Serikali kutoa baadhi ya kazi katika miradi mikubwa inayojengwa na makandarasi wa nje ili kuwajengea uwezo na uzoefu.

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi hiyo, Rhoben Nkori, amesema zaidi ya makandarasi 12,993 wamesajiliwa na Bodi hiyo ambapo katika mkutano huo pamoja na mambo mengine watalaamu hao watapata fursa ya kujadili, kubadilsha na uzoefu na kupatia ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili makandarasi nchini.


No comments: