Friday, June 14, 2024

WADAU WAKUTANA KUJADILI MIKAKATI YA KUKABILIANA NA DHARURA ZA MAAFA YA KIAFYA


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Islam Seif Salim akifungua mkutano wa kitaalamu uliojadili mikakati ya kuweka utayari wa kukabiliana na dharura za Maafa ya kiafya katika miji huko Verde Mtoni Zanzibar.

Na Fauzia Mussa, Maelezo
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Dkt. Islam Seif Salum amesema Serikali itaendelea kuchukua jitihada za kukabiliana na dharura za kiafya ili kuwanusuru Wananchi kutokana na Maafa.
Akifungua mkutano wa kitaalam wa kujadili mikakati ya kuweka utayari wa kukabiliana na dharura za Maafa ya kiafya huko katika Hoteli ya Verde Mtoni Zanzibar amesema upangaji holela wa Mipango miji unasababisha kutokea kwa majanga ya kiafya nchini.
Aidha amesema Serikali kwa kushirikiana na Wadau imeamua kuweka mipango miji yenye Miundombinu rafiki ili kuiweka nchi salama wakati maafa yanapotokezea.

Aidha amesema Serikali inatoa elimu mara kwa mara kwa wananchi ili kuweza kujikinga na dharura za kiafya ikiwemo COVID 19 na Kipindupindu.

" Uratibu na ufuatiliaji uliobora na umeweza kuongeza uwezo wetu wa kukabiliana na Maafa ya kiafya wa haraka endapo yatatokezea, hii ni kutokana na Ushirikiano wetu na washirika wengine wa maendeleo ikiwemo wenzetu WHO.” Alifahamisha Katibu huyo.

Amesema kasi ya ukuaji wa Miji barani Afrika, ikiwemo Zanzibar, imeongezeka na kuleta changamoto kubwa za kiafya hasa maeneo ya mjini kutokana na kuwa na ongezeko kubwa la idadi ya Watu na kukuwa kiuchumi.

Hata hivyo amewataka Wananchi kuendelea kufuata miongozo inayotolewa na Serikali kupitia Wataalamu wa Afya ili kujikinga na Maafa.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi Shirika la Afya ulimwengu (WHO) Dkt. Andamicheal Ghirmay amesema katika kipindi cha miaka 15 ijayo zaidi ya nusu ya Wakazi wa Afrika wanatarajiwa kuishi maeneo ya Mijini hivyo kukosena kwa utayari wa kukabiliana na dharura za kiafya kutapelekea Mamilioni ya Watu kuwa hatarini kutokana na athari za Maafa ya kiafya siku zijazo.

Amefahamisha kuwa kujitokeza kwa Janga la COVID 19 katika miaka ya karibuni imeonyesha udhaifu na umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya afya yenye uwezo wa kukabiliana na dharura hizo hasa katika maeneo ya Mjini.

Amesema WHO itaendelea kutoa msaada wa rasilimali na utaalamu ili kuhakikisha mazingira ya mijini nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla yanakuwa na uwezo wa kukabiliana na dharura za kiafya mara zinapotokezea.

Nao baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo wamesema wamepata utaalamu na maarifa ya kuandaa mikakati madhubuti ya kujiandaa kwa dharura za kiafya sambamba kuwa na uwezo wa kulinda afya kwa ajili ya ustawi wa jamii.

Mkutano huo wa siku mbili,umewashirikisha Wataalam, Watunga sera na Wadau kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Nigeria Thailand, Botswana na China ambapo Jumla ya Washiriki 60 walijadiliana jinsi ya kuandaa mikakati ya kuimarisha dharura za afya katika Mazingira ya Miji.

No comments: