ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 9, 2026

KONGAMANO LA TANZANIA NA MISRI LAFUNGUA FURSA MPYA ZA BIASHARA, UWEKEZAJI NA UTALII



Na Mwandishi Wetu, Misri


Mahusiano ya muda mrefu kati ya Tanzania na Misri yameendelea kupata nguvu mpya kufuatia kufanyika kwa Kongamano la Biashara, Uwekezaji na Utalii la Tanzania na Misri, ambalo limewakutanisha viongozi wa serikali, wafanyabiashara, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka mataifa hayo mawili.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara Ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi wakati wa kuhitimisha Kongamano hilo ambalo limetoa fursa za ushirikiano wa kiuchumi na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Misri. 

Amesema Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali yaliyolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Mageuzi hayo yameongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa moja ya vituo vinavyoongoza kwa kuvutia uwekezaji barani Afrika.

Ametumia  wasaa huo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Misri kutumia fursa zilizopo kwa kuwekeza katika hoteli, vituo vya burudani, miundombinu ya utalii wa baharini, taasisi za mafunzo ya ukarimu na huduma za kidijitali zinazohusiana na utalii.

“Ninawakaribisha kuja kutalii Tanzania kwakuwa kwa sasa kuna safari za moja kwa moja za ndege kati ya Cairo na Dar es Salaam, amesema Dkt. Abbasi”.

Naye Naibu Waziri wa Utalii na Mambokale Misri, Mhe. Yomna El Bahar amesema Kuwa Misri ipo tayari kuendeleza mashirikiano baina ya nchi hizo mbili ikiwemo kubadilishana uzoefu kwani Misri imeweza kufikisha watalii milioni 16 hivyo kama Tanzania tuna mengi ya kujifunza ikiwemo namna ya kuendeleza utalii wa utamaduni na kujifunza jinsi wanavyoyatumia kimkakati historia yao kujitangaza.

Kongamano hilo lililoanza Juni 8, 2026 limehitimishwa leo Juni 9, 2026 katika Hoteli ya Sofitel jijini Cairo, Misri.














No comments: