Advertisements

Friday, June 10, 2011

Mambo 10 yanayokera faragha!


SAFU ni ile ile, mwandishi ni yule yule, ukurasa ni ule ule lakini mada ni nyingine. Sijajua lugha tamu ya kutumia hapa ili uupokee mwaliko wangu wa kujiunga nami. Rafiki zangu, nafarijika sana ninapokutana nanyi hapa kila Ijumaa. Karibuni.

Nashukuru kwa kuchagua kusoma gazeti hili, hususan katika ukurasa huu ambao unakuongezea elimu juu ya mambo mbalimbali ya uhusiano, mapenzi na maisha. Ni imani yangu umekuwa ukivuna mengi.


Twende moja kwa moja kwenye mada; nazungumzia juu ya mambo ambayo yanawakera wengi faragha. Rafiki zangu, kwa bahati mbaya sana, wengi huwa hawasemi wanapokosewa faragha. Wanaamua kubaki na maumivu makali wakati ukweli ndani ya nafsi zao wanakereka.

Hakuna ubishi kwamba, katika uhusiano wa mapenzi (hasa ndoa), faragha ni sehemu muhimu, inayotakiwa kuhakikishwa inalindwa heshima yake kwa gharama yoyote ile. Eneo hilo ndilo chanzo cha usaliti; chanzo cha nyumba ndogo, watoto wa mitaani n.k.
Kama mwanandoa atakosea eneo hili, ndoa yake inaweza kuwa hatarini kutingishika kama si kusambaratika kabisa. Mpendwa msomaji wangu, kwa nini upoteze heshima yako kwa sababu ya jambo dogo ambalo unaweza kulisimamia?

Hapa ipo dawa, kwanza nitakupa mambo kumi ambayo yanakera zaidi faragha ili uweze kuwa ‘smart’ unapokutana na mwenzi wako. Ukumbuke kwamba, baadhi ya mambo hayo, wengi wanakuwa hawapo tayari kuwaeleza wenzi wao ukweli kuwa yanawakera.

KWA NINI YANAKERA?
Kabla ya kuingia kwenye vipengele vyenyewe, kwanza tuone kwa nini nazungumzia mambo yanayokera. Kaka na dada zangu, faragha si uwanja wa mapambano, si eneo la kujadiliana tofauti zenu, ni sehemu ya kustarehe!

Ukiwa katika eneo hilo, unatakiwa kuwaza mambo mawili tu; kumfurahisha mpenzi wako na kuhakikisha nawe unafurahia penzi unalolipata. Ikiwa ndivyo, ikitokea kukawa na mambo yanayokera, tafsiri ya wazi iliyopo ni kwamba, utamuudhi mpenzi wako, utapoteza maana ya eneo lenyewe na mwisho utamfanya mwenzi wako afikirie kutafuta mtu mwingine ambaye ataweza kumfurahisha.
Mpo ndugu zangu? Sasa twende darasani tukajifunze.

(10) KUWA KINARA
Hili ni moja kati ya mambo yanayokera faragha. Kuna baadhi ya watu, wakiingia uwanjani wanataka wao kuwa vinara wa mchezo. Wajuaji na viongozi wa pambano zima. Hawataki ushauri, kila wanachotaka wanataka kiende vile vile.

Hapa lazima niwe wazi kuwa, wanaume hasa ndiyo wenye tabia hii. Hataki kujadiliana na mwenzake kuhusu namna ya kucheza mchezo; haraka nyingi, akifikiria juu ya hatma yake mwenyewe na kumsahau mwenzake.

Hapa mara nyingi mmoja hubaki njiani na mwingine akifika salama alipokuwa akienda. Sababu hii inatosha kabisa kumfanya mwenzi wako afikirie kutafuta sehemu nyingine ambayo atafurahia kuliko kero unazompatia.

(9) USAFI WA MWILI
Unaweza kuona kama ni kitu kidogo sana, lakini hili ni kubwa sana katika uhusiano na hasa faragha. Rafiki zangu, hakuna mtu anayependa kuwa na mwenzi mchafu! Achilia mbali faragha hata nje ya hapo.

Lakini hapa, naomba nizungumzie zaidi kwa upande huo, usafi ni kitu muhimu sana kwa faragha. Mwili ukiwa mchafu, unakaribisha harufu mbaya. Mathalani ukiwa hujafanya usafi katika maeneo yako nyeti ni hatari maana mkiwa na mwenzi wako unaweza kutoa harufu mbaya ambayo itamkera.

Ni vyema ukahakikisha unakuwa msafi muda wote, unasafisha mwili wako ili kumuepushia kero mwenzi wako. Inapendeza zaidi kama mtakutana katika uwanja huo ukiwa tayari umeshaoga.

Kutoka kwenye mihangaiko yako ya kutwa nzima, halafu kukimbilia faragha si sahihi, bado utakuwa unanuka jasho na si ajabu hata kikwapa kikawa kinatoa harufu, kuoga ni dawa! Kuna wengine wana tatizo la kutoa harufu mdomoni, hapa sitazungumza sana juu ni nini cha kufanya katika kupambana na tatizo hili lakini labda niseme tu, ni vizuri kuhakikisha kinywa chako kinakuwa safi, ama kwa kupiga mswaki au kutafuta bazoka zenye harufu ya kuvutia ili kupambana na tatizo hilo.

Inawezekana unachukulia kama ni tatizo dogo lakini lina athari kubwa sana katika uhusiano. Rafiki zangu, kama mnavyoona, nafasi yangu ni ndogo, tuvumiliane hadi wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii, SI YA KUKOSA!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love, vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake;www.shaluwanew.blogspot.com au jiunge naye kwenye facebook.

1 comment:

Anonymous said...

Irene amekuruhusu kutumia picha yake? Is she the author of this piece?