ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 12, 2011

Sitta, Mengi, Zitto Kabwe wang`arishwa

Majina ya Samuel Sitta, Reginald Mengi na Zitto Kabwe, yalikuwa kinywani mwa viongozi wa Baraza la Maadili la Kiislamu Tanzania (Bamakita), kuwa ni miongoni mwa watu waliofanikisha vita dhidi ya ufisadi nchini.
Kadhalika, viongozi hao wamejitosa katika vita ya kujivua gamba ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuitaka Sekretarieti mpya ya CCM chini ya Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama, kutorudi nyuma katika vita dhidi ya ufisadi na mafisadi nchini.

Msimamo wa Bamakita ulitolewa juzi jioni na Mwenyekiti wake, Sheikh Athumani Mkambaku, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam na kusema kuwa viongozi wapya wa Sekretariati ya CCM wana wajibu wa kuwatetea Watanzania wengi wanyonge bila kuwaogopa mafisadi na vibaraka wao, ambao ni wachache.
Alisema Baraza hilo linaipongeza CCM kwa hatua ya kukisafisha chama kwa falsafa ya ‘kujivua gamba’ kwa kuwaondoa katika nafasi za uongozi watuhumiwa wa ufisadi waliokuwa wakitishia uhai wake katika jamii ya Watanzania.
“Pamoja na kukipongeza chama pia tunawaomba viongozi wapya wa chama hicho wasirudi nyuma bali wazidishe mapambano dhidi ya ufisadi na mafisadi waelewe kuwa wanapaswa kuwatetea Watanzania wanyonge, ambao ni wengi na wapigakura na kwamba wasiwaogope mafisadi na vibaraka wao, ambao ni wachache sana,” alisema Sheikh Mkambaku.
Aliongeza: “Sisi kama Waislamu tuko nyuma ya wale wote wanaopambana dhidi ya ufisadi.”
Katika tamko hilo Baraza liliwapongeza wote waliojitoa mhanga kupambana na mafisadi bila kujali madhara yatakayowakuta wakiongozwa na Spika wa Bunge wa zamani katika kipindi cha mwaka 2005-2010, Sitta na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi. Sitta kwa sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
“Baraza letu linawaona watu hawa kama ni watu waliotusaidia sana Watanzania,” alisema Sheikh Mkambaku.
Alisema pia wanampongeza Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, kwa namna anavyojitahidi kufichua ufisadi unaofanywa na baadhi ya watumishi wa serikali wasiokuwa waadilifu.
“Kwa kweli kijana huyu (Zitto) anaonyesha kuwa analipenda taifa letu na anatusaidia Watanzania,” alisema Sheikh Mkambaku.
Aliongeza: “Na ndio maana hata pale serikali inapofanya vizuri pia huisifu kama alivyompongeza Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni kwa kuung’arisha Mkoa wa Kigoma kwa barabara zenye kiwango cha lami, wakati akichangia hotuba ya Waziri Mkuu bungeni.” Hata hivyo, Sheikh Mkambaku alisema wameshtushwa na mwenendo wa baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo vimekuwa mstari wa mbele kuwapamba wanaCCM wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi.
“Gazeti moja lilikuwa likichapisha nyaraka mbalimbali za siri zenye saini za wanaCCM hao kuonyesha jinsi walivyo mafisadi, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida, limekuwa likiwapamba. Hapa tunajiuliza kwanini? Je, vigogo hawa wanakuwa mafisadi wakiwa katika uongozi wa CCM tu, wakiondolewa hawawi mafisadi?” alihoji Sheikh Mkambaku.
Aliongeza: “Au kuna ajenda gani ya siri inayoendelea kati ya mafisadi na gazeti hilo? Na zile nyaraka za siri walizokuwa wanazitoa katika gazeti hilo zilikuwa za uongo? Imekuwaje waandishi wa gazeti hilo wameamua kulamba matapishi yao?”
Kutokana na hilo, Baraza hilo limewataka waandishi wa habari kufanya kazi kwa kufuata maadili ya uandishi. Pia limewataka waandishi wa habari kuelewa kuwa wanajukumu kubwa la kufanya kazi zao kwa maslahi ya Watanzania walio wengi, ambao wanaumizwa na mafisadi hadi leo, ambapo Watanzania wanasherehekea miaka 50 ya uhuru wakiwa gizani kutokana na matatizo ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond na Dowans.
“Hivyo, hatuwezi kulalamikia giza huku tukiwasafisha wale waliotusababishia giza hilo,” alisema Sheikh Mkambaku.
Tamko hilo limetolewa na Bamakita miezi mitatu baada ya Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Taifa ya CCM na Sekretarieti ya chama hicho kujiuzulu.
Hatua hiyo ilifikiwa Aprili 11, mwaka huu wakati wa kikao cha CC kilichofanyika mjini Dodoma, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. Hatua hiyo ilikuwa ni mwanzo wa mageuzi makubwa ndani ya chama hicho lengo likiwa ni kukirejesha katika maadili na kurejesha imani kwa wanachama wake na umma kwa ujumla.
Kufuatia hatua hiyo, Rais Kikwete aliwachagua wajumbe wapya wa Sekretarieti na CC ya CCM baada ya kuwaondoa wanne; wawili kutoka kwenye sekretarieti na CC, na wawili kutoka kwenye CC.
Waliovuliwa ujumbe kwenye sekretarieti na CC, ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba; Katibu wa Fedha, Amos Makalla; Katibu wa Mipango, Kidawa Hamid Saleh; Katibu wa Mambo ya Nje, Bernard Membe; Naibu Katibu Mkuu Bara, George Mkuchika na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Ramadhan Ferouz.
Wajumbe walioondolewa katika CC ni Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Wajumbe wapya waliochaguliwa kwenye sekretarieti ni Wilson Mukama (Katibu Mkuu); Nape Nnauye (Katibu wa Halmashauri Kuu-NEC, Itikadi na Uenezi); Vuai Ali Vuai (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar); January Makamba (Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa); Mwigulu Mchemba (Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha) na Aisha Abdallah Juma (Katibu wa NEC, Organaizesheni).
Mkutano huo wa NEC uliazimia mambo 26, likiwemo la kuwataka vingozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi na utovu wa maadili kupima na kujiwajibisha kabla ya kufanyika kwa kikao kingine.
Kwa mujibu wa chama hicho, watuhumiwa hao wasipoachia nafasi zao chama kitawaondoa kwa nguvu. Miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu ambao wanatuhumiwa kwa kashfa mbalimbali ni Rostam Aziz ambaye anatuhumiwa kwa kashfa ya Kagoda na Dowans.
Rostam ni mjumbe wa NEC Mkoa wa Tabora. Mwingine ni Lowassa ambaye anatuhumiwa kwa kashfa ya Richmond ambaye alijiuzulu uwaziri Mkuu Februari, 2008.
Naye Nazir Karamagi, ambaye ni Mjumbe wa NEC Mkoa wa Kagera anatuhumiwa kwa kashfa ya Richmond. Karamagi alijiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini sambamba na Lowassa mwaka 2008.
Mwingine anayetakiwa kujivua gamba kwa kujiuzulu ujumbe wa NEC ni Chenge ambaye anatuhumiwa kwa kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi mwaka 2002 kwa bei kubwa kuliko bei halisi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: