Advertisements

Tuesday, December 20, 2011

Mwakyembe aunguruma



  Ni kuhusu matokeo ya ugonjwa wake
  Ripoti nzito ya madaktari yatua serikalini
  Asema amerudi salama, hatalipiza kisasi
Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harisson Mwakyembe, ambaye alirejea nchini wiki iliyopita kutoka kwenye matibabu chini India, amezungumzia kuhusu ugonjwa wake na kusema serikali imeletewa ripoti nzima kuhusiana na kilichokuwa kinamsumbua.
Dk. Mwakyembe, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kyela, mkoani Mbeya, alisema Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Apollo nchini India alikokuwa anatibiwa, wametuma ripoti nzito yenye uzito wa kilo 10 kwa serikali ya Tanzania, kuelezea walichobaini baada ya kumfanyia uchunguzi.
Dk. Harrison Mwakyembe alikuwa nchini India kuanzia Oktoba 9, mwaka huu akipatiWa matibabu ya ugonjwa wa mparaganyiko wa ngozi.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo vya IPP nyumbani kwake, Kunduchi, jijini Dar es Salaam jana, Dk. Mwakyembe, alisema kuwa, licha ya ripoti hiyo kutumwa serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi, pia madaktari walimueleza kila kitu, lakini kwa sasa hawezi kuzungumzia chochote kwa kuwa ni mapema kufanya hivyo.
MUNGU AMENISAIDIA, NIMERUDI SALAMA
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama ugonjwa wake unahusishwa na kunyweshwa sumu, Dk. Mwakyembe, alikataa kuweka bayana badala yake alisema hakwenda India kutafuta mchawi bali kupata matibabu.


“Mimi sikwenda India kutafuta mchawi bali nilienda kutafuta matibabu na bahati nzuri Mwenyezi Mungu amenisaidia nimerudi salama,” alisema. 
Dk. Mwakyembe ambaye wakati wote wa mazungumzo, alionekana mwenye furaha, amani na kujiamini na wakati wote alimshukuru Mungu kwa kupata nafuu baada ya kupata matibabu.
SITALIPIZA KISASI
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari wa IPP, aliweka mbele nguvu za Mungu, ambapo alisema kama kuna watu walitaka kumuangamiza anawasamehe na hana sababu ya kulipiza kisasi.
“Sitalipiza kisasi hiyo sio kazi yangu bali Mungu anajua cha kufanya na watu wenye kulipiza visasi maisha yao sio marefu,” alisema.
Dk. Mwakyembe huku akiwa amezungukwa na ujumbe wa viongozi wa Wilaya ya Kyela, waliofika nyumbani kwake kumjulia hali ya afya yake, alisema maombi ya Watanzania katika kipindi chote alichokuwa India yamesaidia kumponya.
KUENDELEA KUPIGA VITA UFISADI
Mwanasiasa huyo anayejulikana kwa kupambana na vitendo vya ufisadi, aliahidi kuendeleza jitihada zake bila uwoga na kwa kasi kubwa na kwamba hatarudi nyuma.
Alipoulizwa kama ugonjwa wake unahusisha chuki za kisiasa, alisema hilo anamuachia Mwenyezi Mungu na kwamba yeye hana cha kufanya.
“Huu ugonjwa matibabu yake yalikuwa magumu kidogo, lakini madaktari walionitibu walijitahidi pamoja na maombi ya Watanzania nayo yamesaidia kunifikisha hapa nilipo leo,” alisema. 
NIKO TAYARI KUENDELEA NA KAZI
Kuhusu kurejea kazini, Dk. Mwakyembe, alisema yupo tayari kuendelea na kazi kama kawaida baada ya madaktari waliomtibu kuridhika kwamba anaweza kufanya hivyo.
MWENYEKITI KYELA: MAFISADI WAMEHUSIKA
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya, Gabriel Kapiji, akizungumza na waandishi wa habari, alidai mafisadi wamehusika katika ugonjwa unaomkabili mbunge wao.
Kapiji na ujumbe wake walifika nyumbani kwa Dk. Mwakyembe kwa ajili kumjulia hali, baada ya kurejea nchini kutoka India alikokuwa amelazwa.

Bila kumung'unya maneno, Kapiji, alisema watu wote wanaopingana na ufisadi ndiyo wanaotaka kuangamizwa na mafisadi na kwamba Dk. Mwakyembe ni mmoja wa watu wanaowindwa.
“Endelea na kazi yako na sisi tupo nyuma yako kwa kuwa mafisadi hawataki kuona juhudi zenu zinafanikiwa hata siku moja,” alisema.
KAULIYA KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA
NIPASHE ilimtafuta Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, kwa ajili ya kutoa ufafanuzi kama serikali imepata ripoti ya madaktari waliokuwa wanamtibu Dk. Mwakyembe, alijibu kwa kifupi kuwa ni mapema kuisemea na kisha akasema yupo kwenye kikao na kukata simu.
KAULI YA WAZIRI WA AFYA
Naye Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, alipoulizwa kuhusiana na taarifa hiyo iliyotumwa serikalini, alisema haijafika ofisini kwake.
Waziri Mponda, alisema serikali inapokea taarifa nyingi kutoka Hospitali ya Apollo ambazo zinalenga kutoa ushauri, lakini ya Dk. Mwakyembe haijapokelewa na kusema kuwa labda bado ipo njiani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: