Advertisements

Wednesday, August 29, 2012

MFADHILI MKUU WA CHADEMA SENGEREMA AHAMIA CCM

MLEZI na Mfadhili Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Sengerema, mkoani Mwanza, Bw. Alex Manji, ametangaza rasmi kukihama chama hicho na kujiunga Chama Cha Mapinduzi (CCM).

 
Bw. Manji ambaye hivi karibuni alitangaza kuwania ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA, katika Uchaguzi Mkuu ujao, alifikia uamuzi huo kwenye Mkutano Mkuu wa Uchaguzi Jumuiya ya Wazazi wa CCM, wilayani hapa, uliofanyia jana.

Alisema hajashawishiwa na mtu kukihama chama hicho bali amebaini kuwa kuendelea kukaa huko ni sawa na kupoteza muda wake kwani CCM ndio chama kilichomlea tangu utoto wake.

“Nimeamua kurudi nyumbani CCM kwa hiari yangu, nitakuwa bega kwa bega na wanachama wote kuhakikisha tunaisambaratisha CHADEMA hapa Sengerema.

“Ninaijua vizuri CHADEMA kwa sababu nimekuwa mdhamini wao mkuu katika jimbo hili,’’ alisema Bw. Manji ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama hicho Kata ya Nyampulukano.
 
Katika mkutano huo, Bw. Manji alipewa kadi yenye namba 0136371 iliyotolewa Novemba 5,2010, na mgeni rasmi Kamanda wa Vijana wa CCM wilayani hapa, Bw. William Ngeleja, ambaye alisema uamuzi aliochukua ni wa busara na unastahili kupongezwa.
 
Akizungumzia uchaguzi huo, Mbunge wa jimbo hilo, Bw. William Ngeleja, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuchagua viongozi ambao watasaidia kuimarisha chama katika Uchaguzi Mkuu ujao.
 
“Ndugu wajumbe, naomba tuwe makini tunapochagua viongozi ambao watakuwa msingi imara wa chama chetu huko tunakokwenda ili tuendelee kuwatumikia wananchi,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Bw. Jaji Tasinga, aliwataka wajumbe wa mkutano huo wajitokeze kwa wingi kutoa maoni yao kwenye tume ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya.

No comments: