Ugaidi uliofanywa na watu wanaojitambulisha kuwa ni wafuasi wa kikundi cha Al Shabbab katika Jumba la Biashara la Westgate, jijini Nairobi, nchini Kenya, Jumamosi iliyopita, ni la kutisha na kusikitisha sana kwani mbali ya kusababisha vifo vya watu zaidi ya 60 na majeruhi zaidi ya 170, ni tukio baya ambalo linatishia amani katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Hii si mara ya kwanza kwa Al Shabbab kutangaza kuhusika na unyama kama huo, kwani mwaka 2010 wakati wa fainali za kombe la dunia walifanya ushenzi mwingine mbaya kama huo kwenye uwanja wa mpira mjini Kampala, Uganda wakati wapenzi wa soka wakitazama fainali za mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yalifanyika katika ardhi ya Afrika, Afika Kusini. Katika shambulizi la Kampala watu 79 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Al Shabbab ni kikundi cha Wasomali wanaotaka kuendesha nchi hiyo kwa sharia na wamekuwa wakiendesha vitendo vya kigaidi ndani ya Somalia kwenyewe na nchi za jirani kama Uganda na Kenya. Kikundi hiki ambacho kimekuwa kikifanya mambo ya kishenzi kabisa, kama vile kuua watu wasiokuwa na hatia, na kusababisha hali ya wasiwasi kwa nchi jirani, kinadai kufanya ushenzi huo kupinga kuwako kwa majeshi ya Uganda na Kenya katika kupambana nao ndani ya Somalia.
Tunasikitika kwamba Kenya imekuwa ikipatwa na madhara haya ya Al Shabbab siyo kwa sababu nyingine yoyote, ila kwa sababu tu ya kupakana na nchi hiyo. Kenya imekuwa mwathirika wa vitendo vya ugaidi vya Al Shabbab kwa sababu tu ya kukataa kuona ushenzi huo ukifanywa nchini mwake.
Tunachukua fursa hii kuwapa pole Wakenya wote kwa janga hili la kundi la kigaidi; tunawatakia moyo wa subira wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika kadhia hii, pia tunawaombea majeruhi uponyaji wa haraka ili warejee kwenye hali zao za kawaida na hatimaye kuendelea na maisha yao kama kawaida.
Ni dhahiri matukio kama haya, na hasa yanapotokea jirani kabisa na taifa letu, ni dhahiri kwamba hali ya usalama katika eneo letu lote la Afrika Mashariki siyo salama. Wakati nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zikijipanga kuzidisha ushirikiano kwa maana ya kujenga mtandao mpana zaidi wa kiuchumi katika sekta zote, tunasikitika kwamba juhudi hizo zinakwazwa na watu ambao kwao amani ni kero.
Al Shabbab ni kikundi cha kigaidi ambacho hata Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikwishapitisha maazimio mengi tangu mwaka 1992 dhidi ya Somalia na wao katika juhudi za kurejesha usalama nchini mwao. Katika maazimio haya Al Shabbab wametajwa kwa uwazi jinsi walivyo hatari kwa usalama wa eneo lote la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika kwa ujumla. Kenya imepata madhara ya mashambulizi ya kigaidi ya Al Shabbab mara nyingi.
Mabasi yamelipuliwa, baa zimelipuliwa na hata majengo mengine pia yamelipuliwa tangu mwaka 2011 hadi sasa. Uchokozi na ushenzi huu wa Al Shabbab ndio uliifanya Kenya kuamrisha majeshi yake kwanza kuwafurusha magaidi hao ambao walikuwa wameweka ngome mpakani na nchi hizo, lakini baadaye kujiunga na majeshi ya UN kuhakikisha amani inarejea Somalia.
Pamoja na kutambua machungu ambayo majirani zetu Kenya wanapitia, na kwa kweli kuomba jumuiya ya kimataifa kufikiria kwa kina zaidi hatua dhabiti zaidi zinazostahili kuchukuliwa dhidi ya Al Shabbab, tunafikiri ni wakati mwafaka pia kwa vyombo vya usalama hapa nchini kujitazama na kujitafakari kama vimekaa kimkakati katika kukabiliana na majanga ya kigaidi kama haya.
Itakumbukwa kwamba wakati kikundi cha Al Qaeda kilipofanya mashambulizi yake Afrika Mashariki mwaka 1998, kililenga balozi za Marekani jijini Nairobi na Dar es Salaam.
Hadi leo ni vigumu kusema ni kwa nini walichagua Kenya na Tanzania, lakini jambo moja lililo dhahiri ni kwamba kama mashambulizi yanafanywa dhidi ya Kenya na Uganda, basi hata hapa kwetu yanaweza kufanywa.
Ni kwa kutambua ukweli huo ndiyo maana tunavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwa macho zaidi, kuimarisha mbinu za kutambua matukio haya kabla ya kutokea, kuongeza utambuzi huu kwa kufanya kazi kwa bidii zaidi. Pia tunawachagiza wananchi wawe walinzi wazuri wa nchi yao kwa kutoa taarifa mapema kwa vitu wanavyovishuku kutokuwa na mwenendo salama ndani ya nchi yetu hasa kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Tunasema haya kwa dhati kabisa kwa sababu katika siku za hivi karibuni vitendo vya kihalifu vyenye sura za kigaidi vimetokea nchini mara kadhaa.
Kuna matukio ya mabomu mawili kule Arusha, kuna mashambulizi ya tindikali dhidi ya viongozi wa dini na hata watumishi wa umma, na kuna hata matukio ya mauaji ya kutumia risasi yenye sura ya kigaidi.
Matukio yote haya yemeichafua sana sura ya taifa letu ndani na nje, lakini kwa bahati mbaya kasi na uwezo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kuchunguza kwa kweli haitii moyo kabisa.
Ni kwa kutafakari haya na yaliyowakuta majirani zetu tunaamini kwamba kuna kila sababu ya vyombo vya ulinzi na usalama kujitazama upya na kujipanga vizuri zaidi ili kuimarisha ulinzi na usalama nchini.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment