Advertisements

Monday, November 10, 2014

simba SC dume, ukawa kimyaa


Mshambuliaji waSimba,raia wa Uganda Emmanuel Okwi.

Na Ibrahim Mussa
BAADA ya matokeo ya sare sita mfululizo, hatimaye Simba imepata ushindi wake wa kwanza katika mechi ya saba kwa kuifunga Ruvu Shooting bao 1-0 katika Ligi Kuu Bara, jana, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ushindi huo uliwazima kabisa mashabiki wa kundi maarufu la wanachama waliosimamishwa uanachama la Simba Ukawa ambao wamekuwa wakidai Simba itatoa sare saba mfululizo na mambo yatakuwa mabaya zaidi kama wasiporudishwa, wengi wakiamini wana nguvu ya ushirikina.

Alikuwa ni mshambuliaji raia wa Uganda, Emmanuel Okwi, aliyefuta mzimu wa sare kwa kufunga bao zuri katika dakika ya 76 baada ya kufanya kazi nzuri yeye mwenyewe pamoja na Elius Maguli.Okwi aliumiliki mpira mbele ya mabeki wa Ruvu na kutoa pasi kwa Maguli ambaye alipiga shuti kali lililopanguliwa na kipa wa Ruvu, Abdallah Rashid kisha Okwi akamalizia kazi kwa kuutupia mpira wavuni.

Ushindi huo umeifanya Simba kufikisha pointi tisa na kuwa ushindi wake wa kwanza katika ligi kuu ya msimu huu.Simba ilionyesha kuwa na nia ya kupata ushindi katika mechi hiyo lakini upinzani ulikuwa mkali. Ruvu walionekana kuwa wagumu kufungika licha ya Simba kupata kona tisa huku wao wakiwa hawana hata moja kwenye mchezo huo.

Staika wa Simba, Amissi Tambwe alishindwa kuitumia nafasi ya kufunga katika dakika ya 37 baada ya kuwapita vizuri mabeki wa Ruvu kisha kupiga shuti lililotua mikononi mwa Abdallah.Kocha wa Simba, Patrick Phiri ambaye alionekana kuwa na furaha kubwa mara baada ya mchezo huo, alisema kikosi chake kinaimarika siku baada ya siku.

Kocha wa Ruvu, Tom Olaba alisema: “Timu yangu imecheza vizuri lakini kutotumia nafasi vizuri tulizopata ndiyo kumesababisha tufungwe.” Lakini msemaji wa Ruvu, Masau Bwire, ambaye amekuwa na maneno mengi, alipata kashkashi kutoka kwa mashabiki waliokuwa wakimzonga baada ya mchezo na baadaye akasema walifurahi kumuona na walitaka kupiga naye picha tu.

Wakati huohuo, Okwi amefichua siri kuwa alimlazimisha kocha wake, Patrick Phiri ampange licha ya kujua kuwa alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya mguu.“Nilikuwa nasumbuliwa na mguu muda mrefu tu, kocha anajua na hata daktari wa timu anajua hilo, walitaka nipumzishwe lakini sikukubali kwa kuwa niliona wachezaji wengi ni chipukizi, bila sisi wazoefu kukomaa hali ingezidi kuwa mbaya.

“Naipenda sana Simba ndiyo maana nililazimika kumwambia kocha anipange hivyohivyo tu,” alisema Okwi mara baada ya mechi ya jana.

Simba Ukawa wawekewa ulinzi mkali Taifa
Mashabiki wa kundi la Simba Ukawa walilazimika kuingia wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari.
Mashabiki hao ambao huwa na kawaida ya kushangilia mwanzo mwisho kila Simba inapocheza, waliingilia upande unaoaminika kuwa ni wa Simba kisha wakati wa kutoka wakatokea upande unaoaminika kuwa ni wa Yanga wakiwa chini ya ulinzi mkali.

Mara baada ya kufika eneo la kuegesha magari, mashabiki hao walikaa kwa muda wakisubiri gari lao wakiwa chini ya askari 11 na walinzi wengine nane wa uwanjani hapo, muda mfupi baadaye gari aina ya Coaster lenye namba T746 DBW lilifika na kuwachukua kuondoka uwanjani hapo huku likilindwa na magari matatu yaliyokuwa na sakari.

Wakati kikundi hicho kikiondoka uwanjani hapo, kulikuwa na majibizano ya chini kwa chini kati yao na mashabiki wengine wa Simba ambao baadhi walikuwa kwenye maeneo tofauti ndani hadi nje ya uwanja wakiwasubiri watoke, lakini walitoka salama. GPL

No comments: