Mende huchukiwa sana na watu na huhusishwa na uchafu na maradhi. Lakini wajua kwamba wadudu hawa wana manufaa makubwa sana kwa binadamu?
Mjini Havana, nchini Cuba kuna aina ya mende ambao hufugwa kama wanyama vipenzi na hata visa vyao husimuliwa kwenye hadithi, anasimulia Mary Colwell. Kwenye kisa kimoja, mende kwa jina Martina huwafanyisha mtihani wanaotaka kumchumbia kwa kuwaudhi kila wanapomtembelea.
"Mwaga kahawa kwenye viatu vyao uone watalichukulia vipi hilo,” anapendekeza nyanyake Martina. "Ni muhimu sana kujua mumeo mtarajiwa hufanya nini anapokasirika – mtihani wa kahawa hufanikiwa.” Kuna
aina 4,500 ya mende, na ni aina nne pekee ambao huwa waharibifu. Wengi
hawaishi karibu na nyumba za watu na hutekeleza jukumu muhimu katika ikolojia
kwa kula vitu vilivyokufa na vinavyooza. Baadhi wana sifa
nzuri na huishi pamoja na kusaidiana katika kutafuta chakula na makazi. Wana uwezo
wa kuishi katika mazingira magumu. Aina moja kwa jina Eublaberus posticus
wanaweza kuishi mwaka mmoja kwa kunywa maji pekee.
Wale
wazito zaidi, huwa na uzani wa gramu 35, na urefu wa sentimeta 8 na huishi
Australia. Wale wadogo zaidi huishi Ulaya na Amerika Kaskazini na wana urefu wa
sentimeta moja pekee. Badala
ya kuwachukia, wanasayansi huwafurahia sana na kuwatumia kwa manufaa ya
binadamu. Mwaka 1999, mende walitumiwa na Prof Robert Full katika Chuo Kikuu
cha California, Berkley, kumpa wazo la kuunda roboti ya miguu sita iliyosonga
upesi na kwa urahisi.
Mende
huwa thabiti sana, na wakianguka huwa wanainuka upesi na kwa urahisi kwa
kutumia mabawa. Miguu
ya mende pia imekuwa ikitumiwa na wavumbuzi wanaotengeneza miguu bandia ya
kutumiwa na binadamu. Kuna
pia mende ambao wamekuwa wakiunganishwa na kompyuta ndogo inayowekwa mgongoni
na kuongozwa kufika maeneo ambayo mwanadamu hawezi kufika.
"Nilipoona hili
mara ya kwanza, nilishangaa sana,” mtafiti mkuu katika mradi huo unaoendeshwa
katika Chuo Kikuu cha A&M cha Texas, Hong Liang anasema.
Mende
wanatumiwa pia katika matibabu. Wanasayansi kwa miaka mingi wamekuwa
wakishangazwa na uwezo wa mende kukaa muda mrefu maeneo yenye sumu na uchafu
bila kudhurika. Wamegundua kwamba huwa wanatoa kemikali za kupigana na sumu.
Wanaweza
kusaidia katika kutengeneza dawa za kusaidia binadamu kukabiliana na bakteria
zinazohangaisha sana watu kwa mfano E. Coli na MRSA ambazo zimekuwa hazisikii
dawa.
Hii
si mara ya kwanza mende kutumiwa kwa sababu za kimatibabu. Mwanahabari Lafcadio
Hearn karne ya 19 alipitia maeneo ya kusini mwa Marekani na kuripoti jinsi watu
wenye pepopunda walivyokuwa wakipewa chai iliyotengenezwa kwa kutumia mende.
“Sijui
ni mende wangapi hutumiwa hadi upate kikombe cha chai, lakini wakazi wa New
Orleans wana imani sana na tiba hii,” aliandika.
Leo
katika hospitali Uchina, krimu inayotengenezwa kwa kutumia ungaunga wa mende
waliosiagwa hutumiwa kutibu vidonda vya moto na pia humezwa kutibu vidonda vya
tumbo.
Mende
wanahitajika sana hivi kwamba Wang Fuming aliamua kufungua biashara ya ufugaji
mende eneo la Shandong, mashariki mwa Uchina. Huwa anafuga mende 22 milioni kwa
wakati mmoja. Anasema tangu 2010, bei ya mende waliokaushwa imepanda mara kumi.
CHANZO: BBC SWAHILI
CHANZO: BBC SWAHILI
1 comment:
Asante kwa hii "Entomology 101". Jee? kuna soko la bidhaa hii ya mende katika nchi nyingine duniani beside China. Nadhani inaweza kuwa good investment, kwani hapa Marekani kwenye majiji ya New York na Chicago nimewaona Mende wakubwa sana.
Post a Comment