Saturday, January 9, 2016

Umeya wa Ilala, Kinondoni moto

Umeya wa Ilala, Kinondoni moto
UCHAGUZI wa mameya katika Manispaa za Ilala na Kinondoni jijini Dar es Salaam ni wa vuta nikuvute na sasa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ameingilia kati.

Waziri huyo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik kuhakikisha kabla ya Januari 16, mwaka huu uchaguzi wa mameya katika manispaa hizo, uwe umefanyika. Simbachawene alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema hadi leo uchaguzi wa mameya katika manispaa hizo, umeshindwa kufanyika kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuwepo kwa mvutano wa vyama vya siasa juu ya uhalali wa wajumbe, wanaotakiwa kushiriki katika kupiga kura; na mapingamizi kadhaa ya kisheria mahakamani.

Aidha alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibari ya mwaka 2010, muundo wa serikali za mitaa Zanzibar na Tanzania Bara, si jambo la Muungano.

Simbachawene alisema sheria za serikali za mitaa, zimebainisha kuwa wabunge wa viti maalumu kuwa wajumbe wa baraza la madiwani la halmashauri za wilaya; na sheria hizo zinaruhusu wabunge wa viti maalumu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuingia na kuwa wajumbe wa baraza la madiwani kwenye mamlaka za serikali za mitaa katika ngazi ya wilaya.

“Kwa kuzingatia vifungu hivi vya sheria za serikali za mitaa, wabunge wa viti maalumu wanakuwa wajumbe wa baraza la madiwani kwa misingi ya mapendekezo ya vyama husika, lakini lazima mchakato wa kupatikana kwao, uwe ulianzia kwenye mamlaka hiyo ya serikali za mitaa kwa mfano wilaya, mji, manispaa au jiji husika,” alisema.

Alisema kutokana na maelezo aliyoyatoa, kwa namna yoyote ile, haiwezekani kwa mbunge au mbunge wa viti maalumu kupiga kura nje ya halmashauri ya wilaya aliyokuwepo, wakati anapendekezwa na chama chake ili kupata nafasi ya uongozi.

“Napenda kuviasa vyama vya siasa kuheshimu sheria zilizopo ili kujenga, kukuza na kudumisha demokrasia, lakini pia kuondoa na kuepusha migogoro na mivutano isiyo ya lazima baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2015,” alisema Simbachawene.

Uchaguzi waahirishwa tena Agizo hilo la Waziri, limekuja baada ya uchaguzi wa mameya, uliotakiwa kufanyika jana, kuahirishwa kutokana na pingamizi, lililowekwa mahakamani kuhusu kuzuiwa kwa uchaguzi huo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu juzi ilitoa zuio kwa wakurugenzi wa Manispaa za Ilala na Kinondoni, kuacha kuendesha uchaguzi wa mameya na naibu mameya kutokana na pingamizi hadi mashauri ya msingi yatakaposikilizwa.

Jana madiwani wa vyama vyote walifika kwenye manispaa hizo ili kuchagua mameya na pia kuapishwa, lakini walielezwa kuwa uchaguzi umeahirishwa tena. Zuio la diwani wa Chadema Katika hatua nyingine, juzi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitupilia mbali ombi la zuio la uchaguzi wa meya katika Manispaa ya Ilala na Kinondoni.

Jopo la majaji watatu, Jaji Amaisario Munisi, Lugano Mwandambo na Ignas Kitusi, lilitoa uamuzi huo katika ombi la zuio la uchaguzi huo, lililowasilishwa na Diwani wa Kata ya Vijibweni, Kigamboni, Isaya Charles wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kusema kuwa hana haki kisheria ya kuwasilisha ombi hilo.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Mwandambo alisema mleta maombi, hana haki kisheria kuwasilisha ombi hilo, kwa kuwa ni diwani katika Kata ya Vijibweni Manispaa ya Temeke, lakini uchaguzi unafanyika katika manispaa nyingine, za Ilala na Kinondoni, ambako yeye siyo mjumbe.

Charles aliwasilisha ombi hilo kupitia kwa mawakili wake, Omary Msemo na Fredrick Kihwelo, akiomba zuio la kufanyika kwa uchaguzi huo, wa Ilala na Kinondoni, wakati wa usikilizwaji wa shauri lake la kuomba tafsiri ya jedwali la kwanza la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shauri hilo, Charles aliiomba mahakama itamke kama masuala yanayohusu uchaguzi wa umeya ni mambo ya muungano. Aliiomba mahakama itamke kama wabunge wa viti maalumu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, wanaruhusiwa kushiriki kupiga kura kumchagua meya wa upande wa Tanzania Bara.

Alidai kuwa, Desemba 10, mwaka jana uchaguzi wa umeya ulivunjika kwa sababu ya madai ya kuwepo kwa wajumbe, ambao ni wabunge wa viti maalumu kutoka Zanzibar, hivyo anahofu hali hiyo ingejitokeza katika uchaguzi ambao uliokuwa ufanyike jana .

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata alipinga ombi hilo, akisema kuwa mleta maombi, hana haki kisheria ya kuwasilisha ombi hilo, kwa sababu siyo mjumbe katika manispaa hizo, za Ilala na Kinondoni, na kufafanua kuwa waliotakiwa kuwasilisha ombi hilo ni wajumbe katika manispaa husika, Ilala na Kinondoni.

Aidha, alihoji orodha ya majina ya wajumbe waliokuwepo kwenye uchaguzi huo, yakiwemo majina ya wanaodaiwa kuwa wabunge wa viti maalumu, aliitoa wapi wakati yeye siyo mjumbe? Pia, mleta maombi, alitakiwa kuthibitisha kama wajumbe hao, walikuwepo kwenye kikao hicho au la ?

Mwenyekiti wa jopo la majaji hao, Jaji Munisi pia alihoji kuhusu majina hayo, jambo lililosababisha mahakama kuahirisha kwa muda ili mleta maombi athibitishe, kama wajumbe hao walikuwepo kwenye mkutano.

Wakili Msemo alithibitisha kuwa orodha ya majina ya wajumbe, yaliyotajwa kwenye hati ya kiapo, inayounga mkono maombi hayo, walikuwepo kwenye uchaguzi huo uliovunjika.

Jaji Munisi aliutaka upande wa serikali, kuwasilisha mahakamani hati ya kiapo kinzani baada ya siku 14 ; na waleta maombi wajibu siku saba baada ya kiapo hicho kuwasilishwa mahakamani. Kesi itatajwa tena Januari 29 mwaka huu.

HABARI LEO

No comments: