Advertisements

Saturday, April 15, 2017

AHUKUMIA JELA MIAKA 30 NA VIBOKO 5 KWA KOSA LA UBAKAJI

Mahakama ya Wilaya ya Hai imemhukumu Daudi Maulid (22) mkazi wa Kijiji cha Longoi, Kata ya Masama Rundugai, kutumikia kifungo cha miaka 30 jela na viboko vitano baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi na kumsababishia ujauzito.
 
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Arnold Kirekiano baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi watano uliotolewa mahakamani.
 
Miongoni mwa mashahidi hao ni mwanafunzi huyo, Dawati la Jinsia na Watoto na daktari.
 
Hakimu alisema anatoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo katika jamii.

Alisema kwa kosa la kubaka atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na viboko vitano na kosa la kumpa mimba mwanafunzi atatumikia kifungo cha miaka mitatu na kulipa fidia ya Sh500,000.
 
Awali, mwendesha Mashtaka wa Polisi, Valeria Banda alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Oktoba 7, 2015 katika kijiji hicho huku akijua anafanya kosa.
 
Mshtakiwa alidaiwa kumbaka mwanafunzi huyo aliyekuwa na miaka 16 ambaye alikuwa anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Patmos iliyopo wilayani hapa na kumpatia ujauzito.
 
Kabla ya hukumu kutolewa, upande wa mashtaka uliiomba Mahakama kutoa adhabu kali dhidi ya mshitakiwa.

No comments: