Advertisements

Tuesday, April 11, 2017

DPP aomba Shikuba apelekwe Marekani



Ali Hatibu Haji maarufu Shikuba
By Tausi Ally, Mwananchi tally@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki amewasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kuwasafirisha Ali Hatibu Haji maarufu Shikuba na wenzake wawili kwenda nchini Marekani kukabiliana na mashtaka ya kujihusisha na dawa za kulevya.

Aliwasilisha maombi hayo kwa nyakati tofauti jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha. Wakili mwingine wa Serikali katika shauri hilo ni Veronika Matikila.

Wakili Kakolaki alidai maombi hayo yameanzishwa na Waziri wa Katiba na Sheria na kwamba, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) alipatiwa nakala kwa ajili ya kufuatilia. Yamewasilishwa chini ya sheria ya kusafirisha wahalifu na kuomba yasikilizwe kwa njia ya mdomo.

Alidai maombi hayo ni kwa ajili ya kuwakamata na kuwasafirisha kwenda Marekani wajibu maombi hao watatu kujibu mashtaka ya kujihusisha na dawa za kulevya. Washtakiwa wengine ni Iddi Salehe Mfuru na Tiko Emmanuel Adam.

Pia, Wakili Kakolaki aliomba Mahakama itoe amri ya kuwahifadhi washtakiwa wakati wanasubiri kibali cha kuwasafirisha nje ya nchi kwenda kukabiliana na mashtaka yanayowakabili.

Wakili Majura Magafu anayemwakilisha Shikuba aliieleza Mahakama kuwa, wamesikia maombi ya upande wa mashtaka na akaomba wapewe muda. Wakili mwingine wa utetezi ni Hudson Ndusyepo.

Alidai suala la kumtoa raia nje ya nchi siyo rahisi na kwamba, kwa sababu washtakiwa walishafikishwa mbele ya Mahakama aliomba maombi hayo yaahirishwe ili waweze kupata nafasi ya kupitia nyaraka walizopewa.

Wakili Magafu alidai kuwa nyaraka hizo ni hati ya ushahidi ambao unatarajiwa kutolewa nje ya nchi. Pia, Wakili Adinani Chitale anayemwakilisha Adam, aliomba muda wa kupitia nyaraka hizo.

No comments: