Advertisements

Sunday, April 9, 2017

Kocha Muingereza avutia na vipaji vya kuogelea

Collins Saiboko akichuana katika mashindano ya taifa ya kuogelea mita 50 ana kwenye bwawa la shule ya Heaven of Peace Kundichi jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).
KOCHA wa mchezo wa kuogelea wa Uingereza, Sue Purchase amevutiwa na vipaji vilivyooneshwa na waogeleaji wengi chipukizi huku akitoa wito kwa wadau kushirikiana Chama cha Kuogelea (TSA) kuondoa changamoto mbalimbali.

Purchase alisema hayo wakati wa mashindano ya klabu bingwa ya Tanzania yanayoendelea kwenye bwawa la shule ya Heaven of Peace (Hopac) na kudhaminiwa na Davis & Shirtliff, CRDB Bank, Mediterraneo Hotel & Restaurant, Coca Cola, Aggrey & Clifford na The Terrace.

Alisema kuwa kuna waogeleaji wengi wa Tanzania ambao wanaweza kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa, lakini tatizo kubwa ni vifaa hasa bwawa la kuogelea la viwango vya kimataifa, ambalo hakuna nchini.

“Kwa kweli nimefarijika sana, nimeona waogeleaji wengi wenye vipaji ambao kama wataendelezwa, nchi inaweza kufanya vyema katika mashindano ya kimataifa hasa Jumuiya ya Madola, Dunia na Olimpiki ya 2020 mjini Tokyo, Japan,” “Kinachotakiwa sasa ni kubadili mfumo wa mazoezi kwa kutumia vifaa vilivyopo, waogeleaji wengi wanaonekana kuchoka kwa muda mfupi kutokana na kukosa muda wa kutosha wa mazoezi, ili kufikia viwango, wanahitaji kuongeza muda wa kufanya mazoezi,” alisema Purchase.

Alifafanua kuwa ni vigumu kufanya vyema kimataifa kwa kufanya mazoezi kwa masaa mawili au matatu na jioni tu wakati waogeleaji wa nchi nyingine wanafanya mazoezi asubuhi na jioni kwa masaa mengi zaidi.

Mweyekiti wa Kamati ya Ufundi ya TSA, Amina Mfaume amekiri kuwa tatizo kubwa ni muda wa mazoezi na kusema hiyo inatokana na kubanwa kwa waogeleaji na shughuli za masomo.

“Ni kweli kuwa waogeleaji wetu hawapati muda muafaka wa mazoezi, kuna tatizo la shule na vifaa, timu nyingi zinafanya mazoezi kwenye mabwawa ya shule na lazima wafanye hivyo jioni baada ya muda wa masomo.”

Katibu Mkuu wa TSA, Ramadhani Namkoveka alisema kuwa wanajitahidi kutafuta wadau ili kusaidia ujenzi wa mabwawa ya kisasa ya kuogelea ili kuwawezesha waogeleaji wengi kupata muda zaidi wa mazoezi kwa gharama nafuu.

Jumla ya waogeleaji 172 kutoka klabu 15 nchini wanashiriki katika mashindano hayo ambayo yanamalizika leo jioni, ambapo washindi watatangazwa.

BAHARI LEO

No comments: