Advertisements

Thursday, April 20, 2017

MSICHANA ALIYEDAIWA KUFA AKUTWA MAKABURINI

JESHI la Polisi limefafanua utata wa msichana aliyekufa Mbezi Tangi Bovu jijini Dar es Salaam kuwa ni tofauti na msichana aliyekutwa makaburini siku moja baadaye akiwa amekaa na kitambaa chekundu mdomoni.

Kwa mujibu wa ndugu, marehemu na msichana aliyekutwa makaburini ni marafiki wanaoishi katika mtaa mmoja Mbezi Juu wilayani Kinondoni.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Suzan Kaganda amesema, ndugu walishindwa kuchunguza mwili vizuri wakiamini aliyekufa ni ndugu yao ambaye ni Anna Mathew (23), kumbe aliyekufa ni Juliana Tawete (32).

“Baada ya ajali kutokea walijitokeza ndugu kwenda kutambua mwili wa marehemu katika Hospitali ya Mwananyamala baada ya ajali ya Aprili 16 kuamkia 17 mwaka huu, wakatambua huyo ni binti yao kumbe hakuwa yeye,” alisema Kamanda Kaganda.

Anasema kwa mshangao juzi usiku wakati mwili wa mtu aliyeaminika kuwa ni Anna ukiwa Hospitali ya Mwananyamala, ndugu zake walienda kutoa taarifa Kituo cha Polisi Kawe wakidai kuwa ndugu yao aliyekuwa amekufa wamemuona makaburini huko Mbezi Juu.

“Ni watu wawili tofauti kabisa, kwa hiyo ni ndugu tu walikosea, unajua kuingia chumba kile cha kuhifadhia maiti kuangalia ndugu yako unaweza kupata mawenge, hata hivyo tunaendelea kuchunguza tukio hili,” alisema Kamanda Kaganda.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, wakati akivuka barabara eneo la Mbezi Tangi Bovu, Juliana aligongwa na gari ambalo halikusimama na kwamba alikuwa ameshuka kwenye gari, baada ya ajali hiyo askari walikuja na kupima ajali huku mwili huo ukipelekwa Hospitali ya Mwananyamala.

Gazeti hili lilifika katika Hospitali ya Mwananyamala ambapo alikuwepo Anna pamoja na ndugu zake pamoja na familia ya Juliana wakiwa na askari kwa ajili ya kuutambua mwili tena na pia Anna kufanya vipimo.

Hawakutaka pia kueleza majibu ya vipimo. Familia ya Anna hawakutaka kuzungumza na vyombo vya habari huku mtu aliyejitambulisha kama babu yake alidai kuwa familia inaendelea kufanya uchunguzi kwa sababu hawaelewi kilichotokea ingawa ndugu yao yuko hai.

“Kama kuna kitu wanaenda kuchunguza ni kumchunguza binti alikuwa wapi mpaka aonekane kesho yake makaburini akiwa na kitambaa chekundu mdomoni, tena akiwa analia, binti huyo ni mdogo miaka 23,” alisema mtu ambaye hakutaka kutaja jina lake ambaye alisema Anna na Juliana ni marafiki na wanaishi mtaa mmoja wa Gold Star, Mbezi Juu.

Dada wa marehemu Juliana, Gladis Charles alisema aliyekufa kweli ni mdogo wake Julieth kwani ameshuhudia mwili wake na kuutambua. Mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa leo jijini Dar es Salaam.

HABARI LEO

No comments: