Advertisements

Wednesday, June 21, 2017

CWT Kilimanjaro chawakingia kifua waathirika wa vyeti feki

Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Kilimanjaro, kimeiomba Serikali kuwalipa mafao walimu waliobainika kuwa na vyeti feki wakidai kuwa walimu hao wamelitumikia taifa kwa muda mrefu.
Chama hicho kimesema, walimu wengi walioondolewa kazini wanadaiwa katika taasisi mbalimbali za fedha walizokopa na walitegemea kulipa madeni yao kwa kutegemea kukatwa katika mishahara yao.
Katibu wa Chama cha Walimu, Kilimanjaro, Digna Nyaki, amesema hayo leo (Jumatano) wakati akiongea na walimu wa Wilaya ya Moshi.
“Naipongeza Serikali kwa zoezi la uhakiki wa vyeti feki hapa nchini lakini bado Serikali inayo jukumu la kuangalia maslahi ya watumishi hao, hususan walimu,” amesema.
Nyaki amesema walimu waliobainika kuondolewa kazini wameacha pengo kubwa huku wengine wakishindwa kurejesha fedha kwa wakati katika taasisi za fedha walizokopa.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Moshi, Godlisten Kombe amesema walimu waliokopeshwa na Saccos ya walimu na kuondolewa kazini wameacha madeni makubwa ambayo hadi sasa hayajalipwa.
Kombe amesema kwa mkoa wa Kilimanjro, watumishi 496 wameondolewa kazini na wengi wao ni walimu.