Advertisements

Thursday, June 15, 2017

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA SPORTPESA

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ubashiri wa michezo ya SportPesa Bw. Pavel Slavkov (kushoto), katikati ni Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji Bw. Abbas Tarimba.Viongozi hao wa SportPesa walimtembelea Makamu wa Rais Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi wa SportPesa waliofika ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo kwa lengo la kujitambulisha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa SportPesa Tanzania. 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amekubali ombi la kuwa mgeni rasmi katika mchezo kirafiki kati ya Timu ya Everton ya nchini Uingereza na timu ya Gor Mahia ya Kenya ambayo ilitwaa kombe la michuano ya Sportpesa iliyofayika hapa nchini hivi karibuni.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amekubali ombi hilo baada ya Kukutana na kufanya mazungumzo na Watendaji wa Kampuni inayojishughulisha na ubashiri wa michezo ya Sports Betting nchini ambao waliongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji Tarimba Abbas Ikulu- Dar es Salaam.
Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amepongeza mipango na mikakati mizuri ya kampuni hiyo ya kutaka kukuza vipaji vya wanamichezo hasa kwa mpira wa miguu kwa Tanzania Bara na Zanzibar na kusema kama malengo hayo yatafikiwa Tanzania itakuwa bora katika mchezo wa mpira wa katika bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.
Makamu wa Rais pia amewahakikishia watendaji wa kampuni hiyo kuwa milango ya ofisi yake ipo wazi na pindi wakiwama katika jambo lolote wawasiliane na ofisi yake ili tatizo linalowakabili liweze kutafutiwa ufumbuzi ili lisikwamishe shughuli za kampuni hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya Sports Betting nchini Tarimba Abbas amemweleza Makamu wa Rais kuwa kampuni hiyo ina malengo makubwa ya kufanya biashara hapa nchini kwa kuzingatia sheria na kanuni za nchini.
Mkurugenzi huyo Tarimba Abbas amesema katika mipango yao wanataka katika kipindi cha miaka Mitatu ijayo kampuni yao iwe ni moja ya kampuni bora nchini katika ulipaji wa kodi kwa Serikali kama wanavyofanya kwa sasa katika Serikali ya Kenya.
Amesema mipango na mikakati waliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha wanainua vipaji vya wanamichezo nchini kwa sababu Tanzania Bara na Zanzibar kuna vipaji vingi vya wachezaji wa mpira wa miguu ambavyo haviendelezwi ipasavyo.
Watendaji wa Kampuni hiyo pia wamemshukuru Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kukubali ombi lao na kuwa Mgeni rasmi katika mchezo wa kirafiki kati ya Timu ya Everton ya nchini Uingereza na timu ya Gor Mahia ya Kenya mchezo ambao unatarajiwa kufanyika tarehe 13 Julai mwaka huu katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Utawala na Utekelezaji wa Kampuni ya Sports Betting nchini Tarimba Abbas amesema moja ya lengo la kuileta Timu ya Everton nchini ni pamoja na mambo mengine ni kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii nchini kupitia mchezo huo ambao unatarajiwa kuangaliwa na maelfu ya watazamaji Duniani kote.
Mkurugenzi huyo pia amemweleza Makamu wa Rais kuwa tayari wameshawasiliana na mamlaka inayohusika na masuala ya utalii nchini ili iweze kutumia fursa hiyo kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini kama hatua ya kuongeza idadi ya watalii watakaokuja kutembelea vivutio nchini na kuongeza mapato ya Serikali kupitia sekta hiyo.

No comments: