Advertisements

Tuesday, June 13, 2017

Nani alifanya nini mikataba ya madini

Wakazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye bar iliyopo katika eneo la Plaza wakitazama matangazo ya moja kwa moja kwenye luninga kuhusu tukio la Rais John Magufuli kupokea ripoti ya kamati ya pili ya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Picha na Dionis Nyato

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ripoti ya kamati ya pili ya makinikia iliyowasilishwa jana imeibuka na majina ya vigogo ikieleza jinsi walivyohusika kuingia mikataba mikubwa ya migodi ya madini na kulitia hasara Taifa.

Kamati hiyo iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya nchi yakiwamo makontena 277 imependekeza vigogo hao wachukuliwe hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro akiwasilisha ripoti kwa Rais Magufuli mbele ya viongozi wengine wakuu wa Serikali, Ikulu jijini Dar es Salaam jana, aliwataja Dk Abdallah Kigoda (marehemu), Daniel Yona, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo kuhusika

Hao wote wamewahi kushika nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti.

Wengine ni wanasheria wakuu wa zamani na manaibu; Andrew Chenge, Johnson Mwanyika, FelixMrema na Sazi Salula.

Mbali na hao pia wamo makamishina wa madini na wakuu wa idara ya mikataba wa zamani; Paulo Masanja, Ally Samaje Dk Dalaly Kafumu, Maria Ndossi na Julius Malaba.

Kamati ya Profesa Osoro imeitaka Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria wakuu wa Serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba, makamishna wa madini na wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini.

Pia imetaka hatua zichukuliwe kwa watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.

Ndani ya ripoti

Katika ripoti hiyo, Profesa Osoro ameeleza jinsi Dk Kigoda alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini alivyoingia mkataba na mgodi wa Bulyanhulu Gold Mines Ltd (Kahama Mine Corporation Limited) ambapo kwa jitihada kubwa alifanikiwa kujadiliana na kampuni hiyo na kuiwezesha Serikali kupata asilimia 15 ya hisa katika kampuni za uchimbaji.

“Hata hivyo, mkataba huo ulifanyiwa marekebisho Juni, 1999 na kusainiwa na Waziri wa Nishati na Madini aliyefuata, Dk Abdallah Kigoda. Marekebisho hayo yaliondoa asilimia 10 ya hisa ambazo Serikali ilikuwa inamiliki na kubakiza asilimia tano tu,” alisema.

Alisema marekebisho mengine katika mkataba huohuo yalifanyika Oktoba, 1999 ikiwa ni miezi minne tangu yale ya awali yafanyike.

“Marekebisho haya ya pili pia yalitiwa saini na Dk Abdallah Kigoda, ambayo yaliondoa asilimia tano ya hisa za Serikali zilizokuwa zimebakia na hivyo Serikali kubaki bila hisa yoyote.”

Profesa Osoro alisema katika marekebisho hayo, Serikali ilikubali kulipwa Dola 5 milioni za Marekani ikiwa ni malipo ya mauzo ya hisa zake.

Vilvile, Serikali ilikubali kuendelea kulipwa kiasi cha Dola 200,000 za Marekani kila mwaka.

Hata hivyo, alisema kamati yake haikuweza kupata uthibitisho wa kufanyika kwa malipo ya jumla ya Dola 6,800,000 za Marekani.

“Kamati imeona kwamba marekebisho hayo ya mkataba yaliyofanywa na Mheshimiwa Dk Abdallah Kigoda hayakuwa na masilahi kwa Taifa kwani Serikali ilipoteza haki ya umiliki wa hisa na kuinyima mapato kutokana na gawio,” alisema Profesa Osoro.

Mlolongo wa hatua haukuishia kwa waziri huyo ambaye Rais Magufuli alisema marehemu tu ndio hawatachukuliwa hatua, pia ulienda kwa mawaziri wengine Yona na Karamagi katika kampuni ya Pangea Gold Mine.

Profesa Osoro alisema kampuni hyo ina mikataba miwili ya uchimbaji madini na wa kwanza ulisainiwa Desemba 2003 na Yona akiwa Waziri wa Nishati na Madini na wa pili ulisainiwa na Karamagi akiwa waziri wa wizara hiyo.

“Katika mikataba hii yote Serikali haina hisa yoyote katika kampuni na pia mkataba huu unatoa nafuu kubwa sana za kodi kwa kampuni, jambo ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato,” alisema Profesa Osoro.

Yona aliingia tena kwenye mkataba wa kampuni ya North Mara Gold Mine ambao aliusaini Juni 1999 akiwa waziri wa wizara hiyo na baadaye marekebisho ya mkataba huo yalifanywa mwaka 2007 na Karamagi.

“Katika mkataba huo Serikali haina hisa yoyote katika kampuni. Aidha katika mkataba wa awali uliotiwa saini na Yona, Serikali ilitoa nafuu ya asilimia 15 ya nyongeza ya mtaji wa kampuni na kuifanya kampuni hiyo iwe inajilipa kwanza ili kurudisha mtaji wake na asilimia 15 iliyopewa na Serikali na hivyo kusababisha kampuni kutangaza hasara katika biashara kila mwaka. Jambo hilo limekuwa linaikosesha Serikali kodi ya mapato,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa kamati aliongeza kuwa, wamebaini kwamba marekebisho yaliyofanyika mwaka 2007 kuondoa nafuu ya asilimia 15, bado malimbikizo ya hasara kutokana na nafuu ya kodi iliyokuwa imetolewa na Serikali iliendelea kudaiwa na kampuni hiyo. Haikuishia hapo katika mkataba wa kampuni ya Geita Gold Mine (AngloGold Ashanti) uliosainiwa na Dk Kigoda akiwa waziri, Serikali haikupata hisa yoyote na pia mkataba huo unatoa nafuu mbalimbali za kodi kwa kampuni, jambo ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato. “Mikataba ya uchimbaji madini inaeleza kuwa inaongeza na kurekebisha masharti yaliyomo katika leseni za uchimbaji madini,” alisema.

Alisema kuwa kamati inaona kuwa masharti ya aina hiyo ni batili kisheria kwa kuwa waziri hawezi kurekebisha masharti ya leseni yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni kupitia vifungu vya mkataba wa uchimbaji wa madini.

Profesa Osoro alisema kamati imebaini kuwa kumekuwapo na uongezaji wa muda wa leseni wa maeneo ya uchimbaji madini kinyume cha sheria na bila kuzingatia masilahi ya Taifa.

“Kwa mfano, kuongeza muda wa leseni na maeneo ya uchimbaji uliofanywa na Ngeleja na Profesa Muhongo, kwa kampuni za North Mara Gold Mines Limited na Pangea Minerals Limited. Pia leseni mbalimbali zilizotolewa na Kamishna Paulo Masanja, Kamishna Dalaly P. Kafumu na Kaimu Kamishna Ally B. Samaje,” alisema mwenyekiti huyo.

Alisema katika kipindi hicho washauri wakuu wa Serikali kwa masuala ya kisheria walikuwa ni pamoja na Chenge, Mwanyika na manaibu wanasheria wakuu ambao ni Mrema na Salula na wakuu wa idara ya mikataba, Maria Ndossi na Julius Malaba.

Dk Kafumu Ngeleja wazungumza

Dk Kafumu ambaye ni mbunge wa Igunga akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema yuko tayari kuhojiwa na vyombo vitakavyomhitaji. “Nisingependa kuzungumza lolote kuhusu mapendekezo hayo, nitakuwa ninazungumza kabla ya kuhojiwa na Serikali, kwani ni mmoja kati ya waliotajwa, nitakuwa tayari kuhojiwa kwa sababu ni maagizo ya Rais,” alisema Dk Kafumu.

Kwa upande wake, Ngeleja alisema hawezi kuzungumzia agizo la Rais Magufuli la kuhojiwa na vyombo vya usalama kutokana na kuhusika kwake katika mikataba ya madini. Hata hivyo alitaja uzembe wa usimamizi wa sheria kuwa ndiyo uliolifikisha Taifa hapo kwa kuwa sheria zilizopo ni nzuri, lakini hazisimamiwi ipasavayo.

“Kuhusu kuhojiwa au kuwajibika sina neno la kusema lakini nampongeza sana kwa moyo wa dhati Mheshimiwa Rais maana amezungumza kwa hisia na uzalendo kabisa kuhusu tunachostahili kupata badala ya tunachopata,” alisema Ngeleja ambaye pia mbunge wa Sengerema.

Hata hivyo, alikiri kuwa mikataba mingi iliyopitishwa siyo mizuri kwa kuwa inawanyonya Watanzania ambao wameshindwa kupitia sheria mpya (ya madini ya mwaka 2010) kuifanyia kazi.

“Kifungu cha 11 pia kinachosema mikataba yote ipelekwe bungeni baada ya miaka mitano na kifungu cha 10 kinasema Serikali ishiriki kimkakati kwenye migodi, lakini usimamizi wake ndiyo shida,” alisema Ngeleja.

Kuhusu mchanga kusafirishwa nje ya nchi, alisema walishaliona jambo hilo mapema lakini wakabainisha kuwa mashine za kufanya kazi hiyo zina gharama kubwa zaidi hivyo kuhitaji ubia katika ujenzi baina ya Serikali na sekta binafsi.

Wakati Ngeleja akisema hayo, Chenge hakutaka kuzungumza na waandishi habari waliomfuata mara baada ya kuahirishwa kikao cha Bunge jana. “Siongei na watu,” ndiyo maneno pekee aliyoyasema mbunge huyo mkongwe wa Bariadi Magharibi.

No comments: