Advertisements

Thursday, June 15, 2017

Viongozi wa Dini Watangaza Siku Saba za Kumwombea Rais Magufuli

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Viongozi wa dini wametangaza maombi ya siku saba nchi nzima kumwombea Rais John Pombe Magufuli ili aendelee na juhudi zake za kulinda raslimali za watanzania kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote, Askofu William Mwamalanga kwa niaba ya viongozi wa dini.

“Tumeamua kufanya maombi ya siku saba kwa kumtaka kila mtanzania popote alipo kutembea hatua saba kila siku akimwombea Mhe. Rais Magufuli ili Mungu amlinde pamoja na anaofanyanao kazi kwa usahihi (uaminifu)”, alisema Askofu Mwamalanga.

Ndani ya siku hizo saba kila mtanzania atakuwa ametembea jumla ya hatua 49 akimwombea Rais Magufuli na wazalendo wenzake.

Kwa mujibu wa Kiongozi huyo wa Dini, maombi hayo yataanza leo Alhamisi Juni 15 nchi nzima na yatajumuisha watu wa dini zote nchini, yaani madhehebu ya Kiislam, Kikristo, Kihindu, Budha na madhehebu mengine.


Maombi haya yanafanyika baada ya kuona kuwa Mhe. Rais Magufuli anachukua hatua madhubuti za kutaka waliohusika kwa namna yoyote kuiba raslimali za Taifa hususani madini, wanachukuliwa hatua na kuitaka kampuni ya ACCASIA kulipa kile ambacho walichukua kinyume cha sheria.

Askofu Mwamalanga alisema kuwa Kamati yake inamwomba Rais Magufuli achukue hatua za haraka kudhibiti raslimali za nchi kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambako mali nyingi zinatoroshwa na wajanja wachache.

Kamati hiyo ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini zote imemwomba Mhe. Rais aziunganishe Wizara za Nishati na Madini na Maliasili na Utalii na kuunda wizara moja ambayo itasimamia kwa karibu raslimali za watanzania.

“Tunamwomba Rais Magufuli amchague mtu makini na mzalendo mwenye uchungu na nchi hii ili asimamie wizara hiyo, na nina hakika wizara hiyo ikisimamiwa vizuri, ndoto ya Rais ya kuifanya Tanzania kuwa nchi mhisani itatimia kwa kuwa hapa Mungu ametujalia kila kitu”,alisema Askofu Mwamalanga.

Viongozi hao wamempongeza Rais Magufuli kwa Uzalendo na Ujasri alionao katika kulinda raslimali za Taifa na kupambana na maovu. Wamesema ni kiongozi wa kuigwa na Marais au viongozi Duniani kote.

Kuhusu suala la walioachishwa kazi kutokana na kuwa na vyeti feki, Askofu Mwamalanga alisema kuwa Kamati inamwomba Mhe Rais kuwasamehe wale ambao wameitumikia nchi hii kati ya miaka mitano na 30 ili walau wapatiwe kifuta jasho licha ya kwamba walitumika bila kuwa na vyeti halali vya Kidato cha nne.

“Msamaha tunaoomba si wa kuwarudisha kazini bali tunaomba kwa ajili ya kupata kiinua mgongo kwani wengine walitumika kwa uaminifu na hata kupewa tuzo za ufanyakazi hodari (bora) hasa katika sekta za Afya,wauguzi, Elimu na maeneo mengine”, alisema Askofu Mwamalanga.

Mapema wiki hii, Rais Magufuli alipokea ripoti ya pili ya uchunguzi wa makinikia ambayo iliwajumuisha wanasheria na wachumi. Katika ripoti hiyo ilibainika kuwa kiasi kikubwa cha madini kilichukuliwa bila watanzania kupata chochote. Takriban madini yenye thamani ya shilingi trilioni 108 yalisafirishwa nje ya nchi bila Tanzania kupata faida kutokana na madini hayo.

No comments: