Advertisements

Monday, July 31, 2017

RC Rukwa aagiza operesheni ya usafi wa vyoo wilaya nzima

 Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemuagiza afisa afya wa wilaya ya Kalambo kuhakikisha anakagua usafi wa vyoo na maeneo yanayo zunguka nyumba kwa wilaya nzima ili kujiepusha na ugonjwa wa Kipindupindu katika Wilaya hiyo.
 Ametoa agizo hilo katika mkutano na wananchi siku ya usafi wa mwisho wa mwezi maarufu kama “Magufuli Day” baada ya Mkuu huyo kukagua nyumba 12, maduka ya wafanyabiashara pamoja na soko katika makao makuu ya wilaya hiyo huku nia ikiwa ni kutaka kujua hali ilivyo wanakojisaidia, wanakohifadhi taka pamoja na hali ya upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
 Katika ukaguzi huo amebaini kuwa wananchi wengi husafisha nje ya nyumba tu huku nyuma ya majumba yao hali ikiwa mbaya jambo ambalo hupelekea kuibuka kwa kipindupindu na kuisababishia serikali kuwa katika wakati mgumu kwa magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika endapo usafi utazingatiwa.
 “Leo nilipenda nione usafi wa matai, nimeuona na nimetoa “marks” 60, Nimepita karibu maeneo mbali mbali, usafi mnaoufanya ni wakuficha uchadu kidogo, huku mbele kusafi lakini nyuma kuchafu sana, nawaomba hilo mlirekebishe” Alisema.
Pia aliishauri halmashauri hiyo ya kalambo kuweza kusimamia sharia za usafi zilizopo bila ya huruma ili kuleta mabadiliko na kuitaka halmashauri hiyo kutenga fedha za makusanyo ya ushuru ili kuweza kuboresha hali ya usafi katika mji huo.
Mwezi mmoja uliopita Wilaya hiyo ilikumbwa na ugonjwa wa kipindupindu na kuua mtu mmoja na kuwaacha wengine ishirini katika hali mbaya jambo ambalo serikali haitaki ijirudie.

“Juzi hapa kulitokea kipindupindu kule Kijiji cha Samazi, hapana hatutaki watu wafe kwa kipindupindu, sasa nimeona choo kinamwaga maji machafu kinyesi kinatoka nje bata wanapokea wanakula, hatupo salama,” Alimalizia.

Pamoja na hayo Mh. Zelote alisisita kuwa usafi ni wa kila siku si lazima kusubiri jumamosi ya mwisho wa mwezi na kueleza kuwa siku hiyo imewekwa maalum ili kuwakumbusha wananchi kuwa wanahitajika kufanya usafi maeneo wanayofanyia biashara pia na kuwa usafi ni muhimu. 

No comments: