Advertisements

Monday, July 31, 2017

TANESCO YAGOMA KUKATA UMEME KUPISHA BOMOABOMOA KIMARA

Shirika la Umeme nchini (Tanesco) limedaiwa kugomea zoezi la ukataji umeme kwenye nyumba zinazotakiwa kuvunjwa eneo la Kimara na Kiluvya ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro leo Jumatatu, Julai 31 kwa kile kinachoelezwa na shirika hilo kuwa Tanroads hawajajipanga.

Mratibu wa bomoabomoa, Ephrahim Kinyafu amesema Tanroads wameweka kambi eneo hilo tangu saa nne asubuhi wakiwasubiri Tanesco kuendelea na zoezi la kukata umeme lakini hawajafika, walipompigia simu Meneja wa Tanesco Kimara, Christopher Nguma akadai hawawezi kuwakatia umeme wateja wao.

“Kwanza asubuhi ya saa mbili nilikuwa ofisini kwa Meneja wa Tanesco nikamweleza kuhusu ukataji wa umeme meneja alichonieleza ni kwamba Tanroads hawajajipanga hawawezi kuja kukata umeme leo alafu waje kuvunja nyumba baada ya miezi, “alimnukuu alivyo mweleza meneja huyo Kinyafu.

Kinyafu amesema sababu nyingine waliyoieleza Tanesco ni kuwa utaratibu wa kuwakatia umeme unaambatana na kutoa notsi ya saa 48, lakini hawajatoa na badala yake Tanroads wanawataka wakakate umeme kitu ambacho hakiwezekani.

“Tanesco pia wamegoma baada ya kutoa taarifa yetu jana kwamba suala letu la bomoabomoa liko mahakamani kwahiyo wanasema kama tunakesi mahakamani basi hawatakata umeme, “amesema Kinyafu.

Meneja wa Tanesco Kimara, Christopher Ndono alipotafutwa kuzungumzia suala la kugomea kukata umeme amesema taarifa zote wanazo Tanroads.

“Sina cha kuzungumzia juu ya hilo, taarifa zote wanazo Tanroads maana wao ndiyo wenye eneo,” amesema Ndono.

Hata hivyo, alipotafutwa injinia wa Barabara ya Tanroads eneo la Kimara na Kiluvya, Jonhson Rutechura ambaye pia ndiye msimamizi wa bomoabomoa amesema atafutwe baadaye.

No comments: