Advertisements

Tuesday, December 5, 2017

ZIARA YA JPM, MAJALIWA BANDARINI ZANG'OA KIGOGO

WIZARA ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imemwondoa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) anayesimamia operesheni, Lazaro Twange kwa kutowajibika ipasavyo.

Imechukua hatua hiyo siku chache baada ya Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara za kushitukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kugundua utendaji usioridhisha, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema wamechukua hatua hiyo kutokana na kutoridhiwa na kusikitishwa na utendaji wa Bodi na Menejimenti ya TPA wa kutofanya maamuzi kwa wakati hali inayochangia malalamiko kuhusu utoaji huduma kuongezeka bandarini hapo.

Profesa Mbarawa alisema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza bandarini Dar es Salaam juzi siku chache baada ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kutembelea bandari hiyo na kubaini madudu kadhaa.

Alisema wanampeleka Naibu Mtendaji Mkuu mpya anayeshughulikia uendeshaji kufuatia aliyekuwepo, Kaimu Naibu Mkurugenzi Mkuu (Operesheni), Lazaro Twange, kushindwa kusimamia majukumu yake.

Aliitaka Bodi na Menejimenti ya TPA kumpa ushirikiano ili atoe matokeo chanya kwenye bandari hiyo. “Tunaleta Naibu Mtendaji Mkuu mpya ambaye atasimamia operesheni. Naomba apewe ushirikiano ili kusaidia Serikali. Huyu ambaye anakaimu tunamuondoa, ameshindwa kwenda na kasi yetu,” alieleza waziri huyo.

Hata hivyo, hakumtaja ofisa mpya aliyeletwa na juhudi za kufahamu ni nani hazikufanikiwa. Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ilisema jana ziara ya Profesa Mbarawa ni mwendelezo wa ziara bandarini kukagua utendaji wa shughuli.

“Nimelazimika kuwaita watendaji na Bodi ya TPA ili kuwaeleza kasoro zenu ambapo inaonesha wazi kuwa asilimia kubwa ya mambo yanayotokea mnakuwa wazito katika kutoa maamuzi,” alieleza Waziri.

Alisema katika bandari hiyo, ipo mizigo ya kahawa ambayo imefika bandarini tangu mwaka 2014 huku kukiwa hakuna sababu za kueleweka za wenye mali kutochukua mizigo yao. Alisema hahitaji wasaidizi wanaokaa vikao na kulipana posho bali wanapaswa kufanya kazi ya kuangalia shughuli zote za bandari.

“Kama hamtabadilika nitaendelea kuja katika bandari hii ili kuchukua hatua pale ambapo inaonekana inabidi kufanya hivyo kwani haipendezi kila kukicha malalamiko kutokea,” alieleza Profesa Mbarawa.

Ameitaka bodi na menejimenti kuhakikisha inatatua changamoto ya kushusha na kupakia mizigo kutoka Zanzibar na kuingia Bara ambayo wafanyabiashara wanalalamikia utaratibu unaotumika kuwahudumia.

Alisema haingii akilini kuona mizigo inayotoka au kwenda Zanzibar kutozwa kodi baada ya saa huku inayotoka nje ya Tanzania ikitozwa baada ya siku saba. Mwenyekiti wa Bodi ya TPA, Ignas Rugaratuka alisema wamejipanga kutendea haki nafasi waliyopewa kwa kusimamia mabadiliko ndani ya bandari.

Alisema tangu waingie wamekuwa wakipambana kuhakikisha upungufu TPA unaisha na wamefanikiwa kurekebisha utawala kwa kutoa mafunzo kwa watumishi na kuzuia wizi ambao ulikuwa umekithiri.

Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema tangu aingie TPA wamejitahidi kurekebisha upungufu na kumuahidi waziri ataongeza jitihada, “Kama ni mabadiliko tumefanya makubwa hasa katika utawala na uongozi ila kila anayehusika katika sekta hiyo anapaswa kutoa msaada,” alisema Kakoko.

Katika ziara zao kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa waliibua madudu bandarini ya kukuta magari 53 ya Polisi na mengine 50 ya kubebea wagonjwa yakiwa hapo tangu mwaka 2015 huku yakidaiwa yameagizwa na Ofisi ya Rais wakati ofisi hiyo ikiwa haijui kuingiza magari hayo.

Rais Magufuli alitoa siku saba kwa taasisi za uchunguzi na TPA, Mamlaka ya Mapato (TRA) na wizara kueleza magari hayo ni mali ya nani na kwa nini yapo hapo kwa miaka miwili na hayana mwenyewe.

Waziri Mkuu alipofanya ziara hapo alibaini pia kuwa kuna matrela 44 ya Kampuni ya NAS ambayo viongozi wake wanadaiwa walitaka kuyatoa kinyemela bandarini kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.

HABARI LEO

No comments: