Advertisements

Sunday, December 9, 2018

WAKALA WA CHAKULA NA DAWA ZANZIBAR KUYAFUNGIA MACHINJIO YASIYO NA VIWANGO

 Kaimu Mkurugenzi Wakala wa Chakula na Dawa Dkt Khamis Ali na Mkaguzi wa Chakula Dkt. Faki Mohd Haji wakikagua Chinjio la Kinyasini linalomilikwa na Abdalla Mohd walipofanya ziara ya kuangalia mazingira ya machinjio ya mkoa Kusini Unguja.
 Mmiliki wa Chinjio la Kinyasini Abdalla Mohd akiwaeleza wakaguzi juhudi anazochukua katika kuhakikisha mazingira ya sehemu yake ya kazi yanakuwa salama na wananchi wanapata kitoweo kilicho bora kwa afya zao.
 Wakaguzi wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Khamis Ali wakiangalio chinjiola kisasa la Donge Muwanda  walipofanya ziara ya kuangalia hali ya mazingira ya machinjio ya Mkoa Kaskazini Unguja.
 Wakaguzi wa Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar wakitembelea Chinjio la Mahonda ambalo halijaruhusiwa kutumika kwa kukosa baadhi ya mahitaji ya lazima ya kufanyakazi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Chakula na Dawa Dkt. Khamis Ali akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara ya kukagua machinjio matatu ya Mkoa Kaskazini Unguja.

PICHA NA RAMADHANI ALI - MAELEZO ZANZIBAR

Na Khadija Khamis –Maelezo
Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imeahidi  kusimamia na kudhibiti ubora wa machinjio ya ng’ombe na yatakayobainika hayana kiwango cha kufanya kazi hiyo yatafungiwa ili kuhakikisha wananchi wanapata chakula kilicho salama kwa afya zao.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Dkt. Khamis Ali Omar ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea machinjio ya Kinyasini,Donge  Muwanda na Mahonda  katika Mkoa wa Kaskazini Unguja kuangali mazingira na ubora wa machinjio hayo.

Amesema juhudi za Serikali kupitia Wakala wa Chakula na Dawa ni kuhakikisha wananchi wanapata chakula kilichoandaliwa katika ubora unaostahiki ambao utamlinda mtumiaji asipatwe na madhara.  

Alisema Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar walianzisha kanuni ya kuwataka wananchi wanaosafirisha nyama ya ngombe kwa ajili ya biashara kutumia gari maalum za kusafirisha kutoka machinjioni kwa lengo la kulinda usalama wa chakula hicho

Dkt. Khamis amezitaka taasisi zinazosimamia suala la uingizaji wa ngombe ikiwemo Idara ya Mifugo, na Kilimo Wakaguzi pamoja na vyombo vya ulinzi kuwa na mashirikiano ya pamoja ili kuhakikisha ngombe hawachinjwi katika mazingira hatarishi.

Diwani wa Wadi ya Mahonda Haji Fadhil Mkadam amewaomba Wakala wa Chakula na Dawa kuwasaidia kumaliza ujenzi wa chinjio lao liweze kuanza kazi  ili kuepuka usumbufu na kuvunja sheria ya kuchinja ngombe katika sehemu zisizorasmi.

Wakala wa Chakula na dawa wanaendelea kulizuwiya Chinjio la Mahonda lisifanye kazi kutokana na kukosa mahitaji maalum yanayotakiwa kuwepo kabla ya kuanza kazi za kuchinja ng’ombe.

Akizungumza na wakaguzi wa wakala wa chakula na dawa  Mmiliki wa Chinjio la Kinyasini Abdalla Mohamed amesema wamekuwa wakifanya juhudi kubwa kuhakikisha sehemu yake ya kazi iko katika mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli hizo.

 Aliwashukuru wakaguzi wa chakula kufanya ziara za mara kwa mara kwa lengo la kuwapa maelekezo ya kuweka mazingira safi katika sehemu za machinjio.


 Awali Mkaguzi  wa Chakula Maulid Khamis Shaabani  wa chinjio la Kinyasini alisema wamekuwa wakifanyakazi usiku na mchana kufuatilia usalama wa ng'ombe wanaofikishwa katika sehemu hiyo kwa ajili ya kuchinjwa na wakigundua kasoro wanazuia kazi isiendelee.

No comments: