Advertisements

Saturday, January 12, 2019

TANZANIA YATAFUTA SOKO LA UTALII UHOLANZI

Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju (mwenye miwani) akiwa na washiriki wengine katika Maonesho ya Utalii ya Kimataifa yanayofanyika nchini Uholanzi kuanzia tarehe 9 hadi 13 Januari 2019. 
Wageni mbalimbali wanatembelea banda la Tanzania ili kupata maelezo kuhusu vivutio vya uwekezaji nchini.
Banda la Tanzania linatia fora kwa kutembelewa na idadi kubwa ya watu wanaotaka kupata maelezo kuhusu fursa na vivutio vya utalii nchini. 
Wageni katika banda la Tanzania. 
Balozi Kasyanju na washiriki wenzake wakiwa katika badna la Tanzania tayari kuanza kazi ya kuuza vivutio vya utalii nchini Uholanzi. 



Tanzania yatafuta Soko la Utalii Uholanzi

Taasisi za Serikali na kampuni binafsi mbalimbali za utalii zipo nchini Uholanzi kushiriki maonesho ya utalii ya kimataifa kwa lengo la kutafuta fursa mpya za soko la utalii nchini humo.
Maonesho hayo maarufu kama Holday Fair 2019 (Vakantiebeurs2019) yalianza tarehe 9 Januari na yatakamilika tarehe 13 Januari 2019, hufanyika kila mwaka katika mji wa Utrecht na kushirikisha taasisi mbalimbali kutoka duniani kote.
Taasisi za Serikali zinazoshiriki ni Bodi ya Utalii Tanznaia (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). Kwa upande wa kampuni binafsi ni into Africa Eco Travel Ltd, Migada Adventures, Mbalaget Tented Camp Ltd, Kili Fair Promotions Ltd, East Africa Camps na Makasa Tanzania Safaris.
Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Irene Kasyanju amesema kuwa maonesho hayo ni fursa adhimu kwa nchi kutangaza vivutio vya utalii ambapo kwa mwaka 2019, waandaji kwa mara ya kwanza wametoa nafasi kwa Balozi za nje zilizopo nchini humo kutangaza pia fursa za biashara na uwekezaji.
Balozi Kasyanju ambao Ubalozi wake unashiriki katika maonesho hayo alieleza kuwa maonesho hayo yataenda sanjari na Vakantiebeurs Travel Congress, Vakantiebeurs Consumer Day na Vakantiebeurs Trade Day ambapo washiriki watapata fursa ya kupeana taarifa muhimu kuhusu mwelekeo na maendeleo ya biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali duniani, vivutio vipya pamoja na kufanya biashara.
Ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo utasaidia washiriki kukutana na wadau na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua soko la utalii nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu vivutio vilivyopo nchini na faida zake. 

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma, Tanzania
11 Januari 2019

No comments: