Advertisements

Thursday, March 21, 2019

WAZIRI WA JPM ANG’AKA RAIA KUNYWESHWA SUMU INATISHA

HALI inatisha! Waziri wa Madini, Dotto Mashaka Biteko ameng’aka kwa hasira baada ya kujionea maji yenye sumu yanayotiririka na kunywewa na wananchi, Uwazi lilikuwepo eneo la tukio.

Waziri Biteko alikutana na kisanga hicho kwa wananchi wa Tarime mkoani Mara licha ya Serikali kuagiza Mgodi wa North Mara kupitia Kampuni ya Acacia kuhakikisha maji hayo hayatiririki.

Waziri Biteko alifanya ziara hiyo katika vijiji vinavyozunguka mgodi huo, Machi 5, mwaka huu na kushuhudia maji hayo yakiendelea kutiririkia katika makazi ya watu na kuingia kwenye vyanzo vya maji wanayotuma wakazi wa vijiji hivyo na mifugo yao na kusababisha hali kuwa inatisha.

“Ninaipatia Kampuni ya Acacia ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, mwisho wa Mwezi Machi 30, mwaka huu iwe imezuia maji yanayokwenda kwenye makazi ya watu katika vijiji vinavyozunguka mgodi huu.

“Baada ya muda huo kuisha, nikirudi nikute mgodi haujafanya hivyo, nitaufunga na ndiyo itakuwa mara ya kwanza mimi Waziri wa Madini, Dotto Mashaka Biteko wa Serikali ya Dk John Joseph Pombe Magufuli kuufunga mgodi huu,” alisema waziri huyo akionesha kukasirika katika mkutano wa hadhara uliokusanya wananchi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Nyamongo.

Maji hayo yalibainika kuwa yana sumu Januari 10, mwaka huu baada ya wataalam kutoka ofisi kuu ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wataalam wa Wizara za Maji na Umwagiliaji, Madini na Muungano na Mazingira walipoyapima.

Majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali yalitolewa na ujio wa makatibu wakuu wa Wizara za Maji na Umwagiliaji, Muungano na Mazingira na Madini siku ya Januari 10, mwaka huu katika eneo la Nyamongo yalionesha yana sumu.

Makatibu wakuu hao siku hiyo walitoa adhabu ya kulipa mamilioni ya shilingi kwa mgodi huo kutokana na makosa mbalimbali likiwemo la kuvujisha maji yanayodaiwa kuwa na sumu kutoka bwawa lao la Nyabirama maarufu TSF na kushindwa kuchimba bwawa lingine.

Pia kuanzisha kimakosa bila kuzingatia taratibu na sheria za uhifadhi wa sumu, bwawa la maji machafu la mashimo ya Gokona na Nyabigena. Aidha, Waziri Biteko alicharuka na kuuonya mgodi huo kuacha mara moja kutanguliza maafisa wadogo tena, Waafrika katika mikutano yake na anataka meneja mkuu wa mgodi awe anahudhuria ili ajibu changamoto zinazoulizwa na wananchi.

Mkutano huo ulifanyika baada ya waziri huyo wa madini kuzungukia vijiji vya Matongo, Nyabichune, Nyangoto, Mjini Kati na aliongozana Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na viongozi wengine wa Serikali na Meneja Uhusiano wa Mgodi, Richard Ojendo.

Katika mkutano huo, Neema Daniel Mohere wa Kijiji cha Matongo ambaye mwanaye Ayubu Daniel Mohere alifariki dunia kutokana na kumuogesha maji ya sumu ya kutoka mgodini hapo mwaka 2016, alilalamika kwa waziri jinsi alivyotelekezwa na mgodi hadi mwanaye kufariki dunia katika Hospitali ya KCMC.

Mama huyo alimkabidhi Biteko nakala ya barua ya ikulu aliyoandikiwa Mkuu wa Mkoa, Malima ya Septemba 11, mwaka jana yenye kumbukumbu namba PP;B1/205/V/01 ilimuagiza mkuu wa mkoa huyo ashughulikie malalamiko yake dhidi ya mgodi huo aliyodai yalimsababishia kifo mwanaye.

Biteko aliuagiza mgodi huo kushughulikia kero ya maji ya sumu na matatizo mengine na amewapa hadi mwisho wa mwezi huu wawe wametekeleza. Kwa upande wa mgodi kupitia msemaji wake, Richard Ojendo alikubali kutekeleza marekebisho yote yanasababisha kuvujisha maji ya sumu na kupenya katika makazi ya watu.

Gazeti la Uwazi limekuwa likiripoti juu ya madhara ya maji hayo ya sumu tangu mwaka 2009 ambapo kwa takriban miaka kumi sasa, watu kadhaa wamepoteza maisha ukiachilia mbali mifugo yao kama ng’ombe na mbuzi. 

GPL

No comments: