Advertisements

Thursday, June 20, 2019

WATANZANIA TUWE MACHO NA WAMAREKANI NA WASHIRIKA WAO


Juni 19, 2019.
Kwa uzoefu wangu wa ufuatiliaji wa masuala ya kidiplomasia na siasa za kimataifa, kilichofanywa na Ubalozi wa Marekani katika Tahadhari yao iliyotolewa saa 1:19 Jioni tarehe 19 Juni, 2019 kuwa kuna minong’ono ya kutokea mashambulizi katika maeneo ya Masaki hususani katika hoteli na migahawa inayotumiwa mara nyingi na watalii na pia maeneo ya Slipway Msasani ni Mikakati ya makusudi isiyoitakia heri Tanzania.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa kupitia akaunti rasmi ya Twitter ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Marekani imekiri kuwa haina ushahidi wa kuwepo kwa tishio hilo na muda ambao mashambulizi yatafanyika na inawataka wananchi kuchukua tahadhari.

Kwa tabia za Marekani hasa pale wanapokuwa hawakubaliana na baadhi ya mambo kwa Taifa fulani hii ni mbinu ambayo huitumia ili kudhohofisha Serikali kwa kuwatisha Watalii, wawekezaji, Wafanyabiashara na hata wananchi wenyewe. Yapo maeneo ambayo hufikia hata hatua ya kutekeleza mashambulizi yenyewe ili mradi ionekane nchi hiyo sio salama na Serikali inashindwa kusimamia usalama wa nchi yake.

Huu ni ukoloni wa kupigiwa mfano na haukubaliki hata kidogo.

Zipo hoja kadhaa za kujiuliza kwenye tahadhari hii ya Marekani

1. Mkataba wa Vienna unaosimamia masuala ya Ubalozi na mashirika ya kimataifa katika nchi nyingine unaelekeza pamoja na mambo mengine, ni makosa kuingilia mambo ya ndani ya nchi ambayo Ubalozi upo. Mkataba huu unaelekeza kuwa kama kuna jambo lolote basi Ubalozi ama Shirika husika liwasiliane na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje. Kwenye jambo hili Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania umekiuka kwa makusudi kwa sababu ni mpango mahususi wa kuichafua nchi.

2. Ubalozi wa Marekani unatoa taarifa nyeti kama hiyo kwenye jamii bila kuwa na uhakika na jambo lenyewe. Tena unakiri kuwa hauna ushahidi. Hili ni jambo la ajabu na hatari sana hasa linapotolewa na Ubalozi wa nchi yenye hadhi kama Marekani. Maana ya hili ni moja tu kufanikisha mpango wake wa kuichafua nchi baada ya kuona njia zote zingine haziwezekani. Kulikuwa kuna ulazima gani kwa Ubalozi wa Marekai kutangaza kupitia Twitter kwa jambo ambalo hawana uhakika nalo tena bila hata kuvijulisha vyombo vya ulinzi na usalama na Wizara ya Mambo ya nje ya nchi?

3. Kilichofanywa na Ubalozi wa Marekani ni kama kujivika usemaji wa masuala ya usalama kwa Tanzania, nchi ambayo ni Huru na ina uhuru wa kufanya mambo yake yenyewe. Ni vizuri Watanzania wakajiuliza hivi leo Balozi wa Tanzania nchi Marekani Mhe. Wilson Masilingi atoe taarifa kwa vyombo vya habari kuwa kuna minong’ono imeenea kuwa maeneo fulani ya Jiji la New York ama Washington DC yatashambuliwa na anatoa tahadhari kwa wananchi huku akikiri kuwa hana uhakika na minong’ono hiyo, PATAKALIKA?

4. Kama kweli kuna hiyo hatari isingekuwa busara kwa Marekani kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kupanga namna ya kukabiliana na mashambulizi hayo badala ya kukimbili kutangaza kwenye mitandao ya kijamii. Ama kuvijulisha vyombo vya ulinzi na usalama ili vyenyewe ndivyo vichukue hatua ya kutangaza na kuweka tahadhari?

Lakini pia ni vizuri Watanzania tujiulize kwa nini mambo yafanyike leo siku ambayo Jarida la Forbes limeitangaza Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa Amani katika Afrika Mashariki?

Kwa nini yatangazwe leo wakati ambapo Tanzania inaendelea kung’ara kila mahali kwa msimamo wa Rais wake Dk. John Magufuli ambaye ameamua kupigania maslahi ya Watanzania dhidi ya unyonyaji uliofanywa na watu na makampuni mbalimbali yakiwemo ya Kimarekani kama vile Symbion, kampuni iliyoleta vichwa vya Treni bila kuzingatia utaratibu na mengine mengi yaliyojiandaa kutupiga katika gesi, madini na mikataba ya kinyonyaji?

Mchezo kama huu umeshafanywa na Marekani katika maeneo mengi baadhi yake ni Korea Kaskazini ambako sote tunajua mzozo uliopo kati ya nchi hiyo na Marekani, Canada na Uganda kwa kutaja machache.

Najua wapo wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania ambao kwa umbumbu na ubinafsi wao watashangilia na kuunga mkono kinachofanywa na Marekani lakini Watanzania ni lazima tuwe macho na jambo hili.

Wamarekani ni wazuri sana kwenye kuharibu amani na uchumi wa nchi ambazo wanalazimisha maslahi yao. Na hutumia mbinu hii hii ya kuwatumia watu wa ndani na hapa kwetu wanatumiwa wanasiasa wa vyama vya upinzani. Walifanya hivyo Libya yanayowakuta Libya leo kila mtu anayaona, wamefanya Tunisia na kwingineko.

Watanzania tuvisikilize vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, na bahati nzuri tayari vimeshazungumza kuhusu jambo hili. Tuwaambie wawekezaji, wafanyabiashara na watalii ambao wanakuja kwetu Tanzania kuwa nchi yetu ipo salama na vyombo vya ulinzi na usalama vipo na vinaendelea na majukumu yake ya kila siku ya kulinda usalama wa nchi na watu wake. Hata siku moja jukumu la ulinzi wa nchi yetu halijawahi kuwa mikononi mwa Wamarekani na nchi yetu ina historia ya kuwa kisiwa cha amani na utulivu.

Kwao Marekani kila uchao watu wanauawa kwa kupigwa risasi, tena ni nchi ambayo silaha za moto zinauzwa kama saa ya mkononi. Silaha zimezagaa kila mahali na mauaji ya kutumia silaha yametamalaki lakini hata siku moja Balozi wa Tanzania hajawahi kutangaza hali ya hatari katika Marekani.

Huu ni uhuni.

Wasituvuruge

Ni Mimi Balozi Mstaafu

No comments: