ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 5, 2020

SERA YA NYUMBA KUANDALIWA KUWEZESHA UPATIKANAJI NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU


Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA

Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani leo tarehe 5 Oktoba 2020, Serikali iko katika hatua mbalimbali za kuandaa Sera ya nyumba ili kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo sambamba na kuwezesha mazingira ya upatikanaji nyumba za gharama nafuu.

Akitoa salamu za Siku ya Makazi Duniani mwishoni mwa wiki mkoani Iringa, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema sera hiyo itatoa dira ya uendelezaji wa sekta ya nyumba nchini.

Aliongeza kuwa, kupitia sera hiyo juhudi zitaelekezwa katika kubuni mbinu mbalimbali za kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata nyumba zilizo bora.

Aidha, Waziri Lukuvi alisema serikali imeanzisha miradi na mifuko mbalimbali ya kusaidia kuwezesha maendeleo ya sekta ya nyumba nchini na kubainisha kuwa, kupitia mradi wa mikopo ya nyumba mabenki na taasisi za fedha zimekuwa zikipatiwa mitaji kwa ajili ya kutoa mikopo ya nyumba. Kwa mujibu wa Lukuvi hadi sasa Serikali ya awamu ya tano imetoa mikopo isiyopungua bilioni 438.58 na wananchi wapatao 5,460 wamenufaika na mikopo kwa utaratibu huo.

Sambamba na hilo, Lukuvi alisema serikali inafanya kazi kwa karibu na taasisi mbalimbali za kifedha kwa kuimarisha vyama vya ushirika ili kuhakikisha fedha zinapatikana kwa makazi ya watu wa kipato cha chini na kubainisha kuwa mikopo midogomidogo imekuwa ikisaidia ujenzi wa wamu kwa watu wa kipato cha chini.

‘’Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa Taasisi zisizo za kiserikali (NGOs) katika kuboresha makazi na baadhi ya taasisi hizo zimekuwa zikishiriki katika uboreshaji wa nyumba za makazi yasiyokuwa rasmi’’ alisema Lukuvi

Aidha, Lukuvi alisema Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI itaendelea kutekeleza miradi ya urasimishaji nchini kwa kutambua miliki hatua kwa hatua ili kuyaweka maeneo yenye makazi holela huduma za kiuchumi na kijamii kupitia mpango shirikishi.

‘’Miradi hii itaendelea katika miji mbalimbali nchini kwa lengo la kuboresha hali ya maisha ya makazi husika na kupunguza umasikini, faida nyingine ni pamoja na kuongeza usalama wa miliki kwa kutoa hati miliki za ardhi’’ alisema Waziri wa Ardhi William Lukuvi.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema, Wizara yake iko katika maandalizi ya kufanya sensa ya nyumba ili kutambua idadi kamili ya nyumba na kusaidia kubaini uhaba na hali ya nyumba na kusisitiza kuwa matokeo ya sensa hiyo yatasaidia kuandaa mipango mikakati ya maendeleo ya nyumba.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa kila jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba ya kila mwaka ambapo Mataifa yote Duniani hujumuika kuadhimisha siku hiyo ikiwa ni azimio namba 40/202 la Umoja wa Mataifa la mwezi Disemba mwaka 1985. Siku hiyo hujulikana kote duniani kama siku ya makazi Duniani. Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa chini ya utaratibu wa Shirika la Makazi Duniani (UN-HABITAT) huadhimisha siku hii kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafakatri hali ya makazi katika nchi na changamoto zake husika na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo. Ujumbe wa mwaka huu ni Nyumba kwa wote Miji bora ya Baadaye.

No comments: