ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 5, 2020

SERIKALI YAFUTA MTAALA WA UALIMU NGAZI YA CHETI KUBORESHA ELIMU

Na. Emmanuel Mbatilo, Dar es salaam

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imefuta mtaala wa ualimu wa ngazi ya cheti kwa elimu ya awali na msingi kwa lengo la kuboresha elimu nchini.

Kauili hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu leo wakati akizungumza na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Semakafu amesema kuwa hatua hii inakwenda sambamba na kufanyia kazi maoni ya wadau ambao wamekuwa wakiyatoa likiwemo la kufuta mtaala huo.

“Mtaala ulioboreshwa unatoa nafasi kwa mwalimu katika mwaka wa pili wa masomo kuchagua eneo la umahiri atakalobobea tofauti na mfumo wa zamani ambao haukuwa katika muktadha huo”, ameeleza Dkt. Semakafu.

Aidha Dkt. Semakafu ameeleza kuwa Mtaala huu mpya utaanza kutumika katika mwaka wa masomo 2020/21 na kwamba mwalimu yeyote mwenye cheti cha ualimu atakuwa na sifa ya kusomea Diploma ya ualimu wa elimu ya awali au msingi na vilevile atakapohitimu na kufaulu atakuwa na sifa ya kujiunga na Chuo Kikuu kupata Shahada ya kwanza ya ualimu wa elimu ya awali au msingi.

Programu itakayofundishwa itakuwa ya miaka mitatu na kwamba masomo yatafundishwa kwa lugha mbili ambazo ni Kiingereza na Kiswahili kutokana na kuwepo kwa shule za English medium nchini.

“Walimu waliosoma Astashada (CHETI) bado Serikali inatambua Uhitimu wa cheti katika kada ya ualimu na ipo kwenye mfumo wa utumishi na itaendelea kuwepo na hakuna mwalimu atakayefukuzwa kazi kwa kuwa yeye ni mwalimu wa ngazi ya cheti”, amesisitiza Dkt. Semakafu.

Vile vile Dkt. Semakafu ameongeza kuwa walimu walioko kazini watakaopenda kujiendeleza wanaweza kusoma kwa masafa kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE) kwa njia ya masafa, njia ambayo haita athiri utendaji na mwisho kufanya mitihani ili kupata Diploma.

Pia Dkt. Semakafu ameeleza kuwa walimu ambao wana vyeti na hawajaweza kupata fursa ya ajira, watatakiwa kurudi vyuoni na kuweza kupata Diploma ya ualimu.

No comments: