ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 6, 2020

WIZARA YA ARDHI KUANZISHA MFUKO WA KUBORESHA MAKAZI

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Bilinith Mahenge akifafanua jambo wakati akizindua Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani jijini Dodoma leo tarehe 5 Oktoba 2020.
Baadhi ya Maafisa kutoka Idara na Taasisi mbalimbali wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Bilinith Mahenge wakati wa uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma leo tarehe 5 Oktoba 2020.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Kalimenze akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyia jijini Dodoma leo tarehe 5 Oktoba 2020.
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Usanifu Miji na Mipango Kabambe Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Immaculate Senje akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma leo tarehe 5 Oktoba 2020.
Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt Bilinith Mahenge (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa kutoka Idara na Taasisi mbalimbali wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani yaliyofanyika jijini Dodoma leo tarehe 5 Oktoba 2020. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kukabiliana na changamoto za kifedha na kutekeleza matakwa ya kisera inarajia kuanzisha Mfuko wa Kuboresha Makazi na Ujenzi wa Nyumba za Gharama Nafuu.

Hayo yalibainishwa leo tarehe 5 Oktoba 2020 jijini Dodoma kupitia hotuba ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi iliyosomwa kwa niaba na Mkuu wa mkoa huo Dkt Bilinith Mahenge.

Kupitia hotuba yake Waziri Lukuvi alisema, Mfuko huo una lengo la kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kupata nyumba bora za gharama nafuu au kupanga.

Alisema, Mfuko wa kuboresha Makazi utaanzishwa kwa kutumia tengeo la bajeti ya Serikali na unatarajiwa kujiendesha kwa kutumia vyanzo vingine vya mapato vikiwemo riba kutokana na mikopo itakayotolewa kwa wananchi na taasisi zinazojishughulisha na maendeleo ya nyumba.

Aidha, kupitia Maadhimisho hayo ya Siku ya Makazi Duniani aliziagiza ofisi za ardhi za mikoa na mamlaka ya upangaji kusimamia kikamilifu zoezi la utambuzi, upangaji, upimaji na umilikishaji wa makazi kwa kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyotolewa ili kila mwananchi mwenye kiwanja na nyumba sehemu zinzzokjubalika kisheria aweze kumilikishwa.

Sambamba na hilo alizitaka Halmashauri zote nchini kuwapatia waendelezaji miliki huduma watakazohitaji kama vile kuanisha maenepo yaliyoiva kimipango miji, kuandaa mipango ya uendelezaji miji, kupima viwanja na kuweka miundo mbinu.

‘’Halmashauri zinapaswa kutoa hati miliki za ardhi na vibali vya ujenzi kwa wakati bila kusahau jukumu la msingi la kusimamia na kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi’’ alisema Lukuvi kupitia hotuba yake.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Kalimenze alisema wakati Tanzania ikiadhimisha siku ya makazi duniani inaonesha kuna uhitaji mkubwa wa makazi bora katika maeneo ya mijini na vijini kutokana na ongezeko la watu na kubainisha kuwa kati ya asilimia 70 hadi 80 ya makazi nchini yapo katika maeneo yasiyo rasmi.

Alifafanua kuwa Tanzania bado ina uhaba mkubwa wa nyumba hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini na kubainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nyumba zilizojengwa zimegharimiwa na wananchi wenyewe.



Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa kila jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba ya kila mwaka na siku hiyo huadhimishwa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutafakari hali ya makazi katika nchi na ujumbe wa mwaka huu ni Nyumba kwa wote Miji bora ya Baadaye.

No comments: