Advertisements

Saturday, March 6, 2021

KAMATI NA MUONGOZO WA KUSIMAMIA USAFISHAJI MCHANGA, TOPE NA TAKA NGUMU KWENYE MITO NA MABONDE MKOA WA DAR ES SALAAM VYAZINDULIWA RASMI

Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu azindua rasmi mwongozo wa usafishaji mchanga, tope na taka Ngumu Kwenye Mito na Mabonde Mkoa wa Dar es Salaam. Uzinduzi huo umefanyika wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa jijini Ilala Dar es Salaam
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dar es Salaam wakisikiliza kwa makini Hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu (Hayupo Pichani)

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu, amezindua rasmi Kamati na Muongozo wa Usimamizi wa Uchimbaji Mchanga katika mito katika Mkoa wa Dar es Salaam. Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Anatoglo Mnazi Mmoja Jijini Ilala Mkoa wa Dar es Salaam katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa.

Aidha Mhe. Ummy amesema kuwa lengo kubwa la kuanzisha Muongozo na Kamati hiyo ni kuweza kupunguza changamoto zinazojitokeza za Kimazingira katika Mito na Mabonde. Mhe. Ummy amesema kuwa Kamati hii itasaidia katika kutoa ushauri wa kimazingira kabla ya kutolewa kwa kibali cha uchimbaji kutoka Mamlaka ya Bonde

“Kamati Maalum ya kusimamia usafishaji Mito na Mabonde katika Mkoa wa Dar es Salaam naipitisha rasmi leo. Kikosi kazi hiki kitakuwa na wataalamu kutoka Taasisi zote zinazohusika na uratibu na usimamizi wa usafishaji mito kwa kuondoa mchanga, tope na taka ngumu na kitakuwa chini ya uratibu wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam kama mwenyekiti, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC atakuwa katibu na wajumbe ni Mamlaka ya Bonde la wami Ruvu, Madini, vyombo vya usalama, Dawasco ,Tanroad, Tarula, Maafisa Mazingira wa Mkoa wa Dar es Salaam na NEMC” Mhe. Ummy

Ameendelea kusema kuwa kuna haja ya kusafisha Mito ili kupatikana mtiririko mzuri wa maji kuelekea baharini, ila changamoto iliyopo kwa sasa wachimba mchanga wanatoa mchanga lakini tope na taka zilizopo kwenye mito hawazitoi, hivyo kusababisha madhara makubwa kwa Wananchi na kusababisha uharibifu wa miundombinu iliyopo. Kutokana na kuanzishwa kwa kamati hii Mhe. Ummy amesema kuwa anaamini usafishaji wa Mito na Mabonde utasimamiwa ipasavyo.

“Suala la kusafisha mito ni jukumu letu kwani kuacha mchanga katika mito inasababisha athari kubwa za kimazingira, lakini uchimbaji mchanga katika mito uwe na utaratibu wake kwani zoezi hilo lisiposimamiwa kitaalamu hupelekea athari kubwa Zaidi kimazingira” Mhe. Ummy

Vile vile Mhe. Ummy amesema kuwa kila anayehitaji kuchimba mchanga ni lazima awe na kibali kutoka Mamlaka ya Bonde, ambacho kibali hicho kitatolewa kupitia kamati ya ushauri ambayo ameizindua. Amesema pia Halmashauri na Manispaa hazitakuwa na mamlaka ya kutoa kibali bali watakuwa washauri katika kamati hiyo.

“Uchimbaji wa kusafisha mito bila kibali hautaruhusiwa. Kibali ambacho kitaruhusiwa ni kile kilichotolewa na Mamlaka ya Bonde, lakini bonde hatatoa kibali bila kupata maoni ya kikosi kazi. Kuanzia sasa Halmashauri haitaruhusiwa kutoa kibali hicho japo nafahamu kwamba usafishaji mchanga katika bonde ni sehemu ya mapato ya Halmashauri lakini tunawajibu wa kulinda Mazingira yetu. Manispaa na Halmashauri zitakuwa watekelezaji wakuu wa Muongozo huu.”

Alimalizia kwa kusema “najua kunauhitaji mkubwa wa mchanga kwa matumizi mbalimbali ya ujenzi ya Miundombinu ya barabara na madaraja lakini ni dhahiri kuwa uko uchimbaji holela wa mchanga ambao unasababisha uharibifu mkubwa wa Mazingira na kusababisha mafuriko.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Aboubakari Kunenge, amempongeza Mhheshimiwa Waziri kufikia hatua hiyo kwani suala la kuchimba mchanga kwenye mito kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni changamoto kubwa.

“Nikuahidi Mhe. Waziri kuwa tutakayo kubaliana hapa kutokana na uchunguzi wa kitaalamu kwamba huu ndio utaratibu wa kufata nitausimamia kama Mku wa Mkoa wa Dar es Salaam na kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Mkoa kwa sababu masuala haya yanagusa maisha ya wananchi wetu lakini vile vile yana athari za kiusalama katika Maisha ya watu” Mhe. Kunenge

No comments: