Advertisements

Monday, March 8, 2021

PROF. KABUDI ATEMBELEA MIRADI YA KIMKAKATI INAYOTEKELEZWA NA SERIKALI MKOANI KIGOMA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi,Mhe. Balozi Albert Shingiro wakimsikilizaMkurugenzi wa Eneo Maalum la Uwekezaji la Kigoma (KiSEZ), Bw. Omar walipotembelea eneo hilo ili kujionea miradi ya uwekezaji iliyopo. Ziara hiyoilifanyika tarehe 6 Machi 2021 ikiwa ni sehemu ya kuhitimisha mkuatano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu uliofanyika kati ya Tanzania Burundi Mkoani Kigoma tarehe 3 hadi 5 Machi 2021.
Mmoja wa Wataalam katika kampuni ya kufua umeme wa jua ya ...akitoa maelezo kuhusu mitambo mbalimbali inayotumika kufua umeme huo.
Mtaalam wa umeme wa jua akitoa maelezo kwa Mhe. Prof. Kabudi walipotembelea eneo maalum la uwekezaji ili kujionea mradi huo ambao ukikamilika utazalisha megawati 5 zitakazosambazwa kwa wakazi wa mkoa wa Kigoma

Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza ujenzi na ukamilishaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ile iliyopo katika mikoa inayopakana na nchi jirani ili kuharakisha maendeleo ya maeneo hayo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi, alipowaongoza Wajumbe wa mkutano wa sita wa tume ya pamoja ya kudumu kati ya Tanzania na Burundi kutembelea miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali katika mkoa wa Kigoma.

Miradi iliyotembelewa ni pamoja na Eneo Maalum la Uwekezaji wa Kigoma (Kigoma Special Economic Zone-KiSEZ); Uwanja wa Ndege wa Kigoma, Bandari Kavu ya Katosho na Bandari ya Kigoma pamoja na Kituo cha Pamoja cha Kutoa huduma Mpakani (OSBP) kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Manyovu mkoani Kigoma.

Akiwa kwenye eneo Maalum la Uwekezaji, Prof. Kabudi na Wajumbe wengine walijionea uwekezaji mkubwa uliofanywa kwenye eneo hilo na Kampuni ijulikanayo kama Next Gen Solar wa kuzalisha umeme wa jua wa megawati tano ambao utaanza kusambazwa rasmi kwa wakazi wa Kigoma mwezi Aprili 2021. Upatikanaji wa nishati hiyo ya umeme unatarajiwa kuwanufaisha wakazi wa mkoa huo kiuchumi.

Kadhalika Mhe. Prof. Kabudi na Wajumbe wengine walipata fursa ya kutembelea kampuni ya Third Man Limited inayozalisha Asali ijulikanayo kama Upendo (Upendo Honey) ambayo nayo imewekeza kwenye eneo hilo maalum la KiSEZ. Katika maelezo yake kwa Mawaziri, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw. Alex Scovic alisema kuwa Kampuni yake ambayo inachakata asali inayozalishwa bila kutumia kemikali (organic) inanunua asali hiyo kutoka kwa wafugaji wa nyuki zaidi ya 3,000 waliopo Kigoma na mikoa jirani kama Tabora, Katavi, na Rukwa na baadaye kuiuza asali hiyo nje nchi hususan nchini Marekani.

“Kampuni yetu ni ya kwanza kuwekeza kwenye eneo hili. Tunazalisha Asali safi isiyo na kemikali ambayo ina soko kubwa nje ya nchi hususan nchini Marekani. Biadhaa zetu tunazitangaza kuwa zimetoka Tanzania” alisema.

Pia alijulisha kuwa, Kampuni yake imeajiri zaidi ya vijana 60 wa kitanzania na kwamba mbali na kuchakata asali, kampuni hiyo inazalisha nta ambayo huuzwa nchini Ujerumani ambao huitumia kwa ajili ya kutengeneza vipodozi. Kampuni ya upendo huzalisha zaidi ya tani 4,000 za asali kwa mwaka.

Katika ziara yao kwenye eneo la Bandari Kavu la Kitosho, Mawaziri na Viongozi wengine walijulishwa kuwa eneo hilo limeanzishwa maalum kwa ajili ya kurahisisha usafirishaji na uhifadhi wa mizigo na bidhaa mbalimbali zinazokwenda Burundi kutokea Bandari za Tanzania. Tayari eneo hilo limepata mzabuni atakayeanza ujenzi mwaka huu. Pia Mawaziri hao walitembelea Bandari ya Kigoma na kupata fursa ya kujionea meli kongwe na ya kihistoria ya MV Liemba ambayo ina miaka 108 tangu itengenezwe, MV Mwongozo na MV Sangara ambazo zote zitaanza kufanyiwa ukarabati ili kuziwezesha kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Kigoma na kutoka nchi jirani.

Wakiendelea na ziara ujumbe huo ulitembelea Uwanja wa Ndege wa Kigoma ambapo ulipata maelezo kutoka kwa Meneja wa TANROAD wa Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma kuwa, mradi huo unalenga kupanua na kukarabati maeneo mbalimbali ya Uwanja huo ikiwa ni pamoja na kuongeza urefu wa barabara ya kuruka na kutua ndege ambayo awali ilikuwa na urefu wa mita 1800 na sasa mita 1,300 zitaongezwa ili kuwezesha ndege kubwa kutua. Pia mradi unalenga kujenga jengo la abiria, maegesho ya ndege, usimikaji wa taa na mitambo ya kuongozea ndege, ujenzi wa jengo la kuongozea ndege, maegesho ya magari pamoja na uzio wa usalama.

Mhe. Prof. Kabudi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Mhe. Balozi Albert Shingiro walihitimisha ziara yao kwa kutembelea eneo kitakapojengwa Kituo cha Kutoa Huduma kwa Pamoja Mpakani (OSBP) cha Manyovu na Mugina kwa upande wa Burundi. Wakiwa Manyovu waliweza kutembelea maeneo ambayo vituo hivyo vitajengwa kwa upande wa Tanzania na upande wa Burundi pamoja na kupokea taarifa ya mradi huo ambapo walijulishwa kwamba tayari usanifu wa ujenzi wa kituo hicho cha Manyovu ambacho kitakuwa cha aina yake umeanza na utakamilishwa mwishoni mwa mwezi Machi 2021.

Akitoa hotuba kuhitimisha ziara kwenye miradi hiyo, Prof. Kabudi alisema Tanzania inawekeza kwenye miradi hiyo ili kurahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi mbalimbalii inazopakana nazo ikiwemo Burundi. Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shingiro alipongeza jitihada hizo za Tanzania na kuahidi kutumia fursa za miradi hiyo ambayo mingi inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brig. Generali Wibert Ibuge akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye wakati waliposhiriki ziara ya Mawaziri wa Mambo ya Nje kwenye maeneo mbalimbali.
Mhe. Prof. Kabudi akiwa na Mhe. Balozi Shingiro pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho wakimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Asali ya Third Man Limited inayozalisha ijulikanayo kama Upendo, Bw. Alex Scovic akifafanua kuhusu Kampuni yake ambayo imewekeza kwenye Eneo Maalum la Uwekezaji la Kigoma,
Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakiangalia Asali inayozalishwa na Kampuni ya Upendo
Mhe. Pfof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakiangalia mapipa ambayo hutumika kusafirisha Asali nje
Mhe. Prof. Kabudi akiangalia nta iliyokuwepo kwenye Kampuni ya Asali ya Upendo
Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakimsikiliza Mkurugenzi wa TANROAD-Kigoma, Mhandisi Narcis Choma alipokuwa akitoa taarifa fupi kuhus ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma
Mhe. Prof. Kabudi akionesha eneo ambalo mita 1300 za barabara ya kurushia na kutua ndege zitaongezwa
Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe Balozi Shingiro wakiwasili kwenye eneo la Kitosho mjini Kigoma itakapojengwa Bandari Kavu kwa ajili ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha shehena mbalimbali zinazokwenda nchini Burundi kutokea Tanzania
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Mhandisi Deusdedit Kakoko akitoa maelezo kuhusu Bandari Kavu hiyo
Mawaziri wakimsikiliza Mhandisi Kakoko walipowasili kwenye Bandari ya Kigoma
Mhe. Dkt. Chamuriho naye akizungumza kuhusu masuala ya uchukuzi bandarini hapo
Mhe. Prof. Kabudi akisaini kitabu ca wageni mara baada ya kutembelea Meli Kongwe ya Mv Liemba. Meli hiyo ambayo ina historia ya muda mrefu ilitengenezwa mwaka 1913. Serikali inao mpango wa kuikarabati meli hiyo ili iendelee kutoa huduma kwenye Ziwa Taznganyika. Kulia ni Mhe. Dkt. Chamuriho na kushoto ni Nahodha wa Meli hiyo , Bw. Titus Mnyanyi
Nahodha Mnyanyi akitoa maelezo kuhus meli ya MV Liemba
Balozi Ibuge nae akisaini kitabi cha wageni kwenye Meli ya MV Liemba
Mhe. Prof.Kabudi akiwa kwenye chumba cha nahodha huku akionesha namna meli hiyo inavyoendeshwa
Mhe. Balozi Shingiro nae akijaribu usukani wa meli hiyo kongwe nchini
Waheshimiwa viongozi wakifurahia kuwa ndani ya meli hiyo yenye historia kubwa
Mhe. Prof. Kabudi akiwa ameongozana na Mhe. Balozi Shingiro wakiteremka kutoka kwenye Meli ya MV Liemba baada ya kutembelea meli hiyo
Mhe. Prof. Kabudi kwa pamoja na Mhe. Balozi Shingiro wakisaini kitabu cha wageni walipowasili kwenye Ofisi za Forodha za Tanzaniazilizopo katika eneo la Mpaka wa Manyovu. Mhe. Prof. Kabudi alifika eneo hilo kwa ajili ya kukagua mahali kitakapojengwa Kituo cha Pamoja cha Kutoa Huduma Mpakani /(OSBP)
Makatibu Wakuu wakiwa kwenye Ofisi za Forodha za Tanzania mpakani Manyovu
Mhe. Prof. Kabudi akionesha eneo ambalo Kituo cha OSBP kitajengwa
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Jilly Maleko akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Bw. Frank Mwega wakati wa ziara huko Manyovu
Mhe. Prof. Kabudi akiwa na Mhe. Balozi Shingiro wakivuka mpaka kuelekea Burundi kwa ajili ya kujionea eneo ambalo limetengwa na Serikali ya Burundi kwa ajili ya ujenzi wa OSBP
Mhe. Prof. Kabudi akiwa na Mhe. Balozi Shingiro wakiangalia jiwe ambalo ni mpaka kati ya Tanzania na Burundi
Hotuba
Picha ya pamoja ya viongozi wakionesha upande wa Tanzania

Picha ya viongozi wakiwa mpakani

Picha ya pamoja

No comments: