Advertisements

Friday, September 17, 2021

WAGANGA WAKUU WATAKIWA KUONDOA MALALAMIKO YA WANANCHI KATIKA MAENEO YAO

Na Asila Twaha – DODOMA.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Festo Dugange amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha wanajitahidi kuondoa malalamiko ya wananchi katika kutoa huduma bora za Afya kwenye maeneo yao.

Dkt. Dugange amebainisha hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri Jijini Dodoma.
Akitoa Salamu za Wizara kabla ya kumkaribisha Waziri wa Afya kufungua Mkutano huo, Dkt. Dugange alisema, Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya Afya kwa kupeleka fedha kwa bajeti ya mwaka 2020/21.

Amesema, hadi kufikia Septemba, 2021 shilingi bilioni 37.5 zimepelekwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya 150 kwenye Tarafa.

Naibu Waziri amefafanua kuwa, kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha inaendelea kutatua changamoto katika sekta ya Afya ili wananchi wanufaike na huduma bora zinazotolewa ikiwemo upatikanaji wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma, na kuwataka viongozi hao kusimamia na kuhakikisha kero zinapungua.

“Niwaombe Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri pamoja na wataalamu wengine mfahamu ni niwajibu wetu kusimamia, kudhibiti rasilimali fedha kwa matumizi yasiyofaa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vitendanishi na vifaa tiba na dawa zinatumika ipasavyo kama inavyotarajiwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu’’ amesema Dkt. Dugange.

Aidha, amewapongeza wataalamu wote wa Sekta ya Afya nchini kwa kuendelea kutoa huduma na kupambana dhidi ya ugonjwa wa UVIKO – 19 na kutoa wito kuendelea kutoa elimu kwa jamii ya namna ya kujilinda na kupokea chanjo.

Mkutano huo umebebwa na kauli mbiu Ustahamilivu wa Mifumo ya Afya katika Mapambano dhidi ua UVIKO-19 ‘CHANGAMOTO NA FURSA’

No comments: