Advertisements

Saturday, October 23, 2021

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA


KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA WA KUTUPA MTOTO.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kumkamata mwanamke JANETH PETER [32] Mkazi wa Kiwira Wilayani Rungwe kwa tuhuma za kutupa mtoto mchanga jinsi ya kike anayekadiriwa kuwa na umri wa siku tatu ambaye alikutwa tayari amefariki dunia baada ya kutupwa ndani ya shimo la choo.

Mtuhumiwa amekamatwa Oktoba 20, 2021 majira ya saa 19:00 jioni baada ya Jeshi la Polisi mkoani hapa kufanya msako mkali huko Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa ambaye amehojiwa na kukiri kutenda kosa hilo.

Awali mnamo Oktoba 20, 2021 majira ya saa 09:00 asubuhi huko Mtaa wa Makaburini uliopo Kata ya Kiwira, Tarafa ya Ukukwe katika Halmashauri ya Rungwe, Mwili wa kachanga ulikutwa ndani ya shimo la choo kilichopo nyumbani kwa SALOME LUTENGANO [36] Mkazi wa Mtaa wa Makaburini na ndipo jitihada za kuutoa zilianza lakini tayari alikuwa amefariki dunia. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

No comments: