Advertisements

Monday, October 25, 2021

TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE YAIBUKA KINARA MATUMIZI YA TEHAMA SEKTA YA AFYA

Na: Mwandishi wetu – Arusha

23/10/2021 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imepewa tuzo ya Taasisi ya mabadiliko Tehama bora katika utoaji wa huduma za afya nchini.

Tuzo hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Zainab Chaula wakati wa kongamano la tano la siku tatu kwa maafisa TEHAMA Tanzania lililomalizika Jana Jijini Arusha.

Akizungumza wakati wa kufunga kongamano hilo Bi. Chaula alisema kuwa JKCI ni miongoni mwa Taasisi za serikali ambayo inatoa huduma nzuri ya matibabu ya moyo kwa wagonjwa kupitia mifumo ya Tehama.

“Lengo la serikali ni pamoja na kuiwezesha nchi ya Tanzania kuendana na kasi ya mabadiliko ya Tehama duniani jambo ambalo JKCI inalifanya kuendana na matumizi ya Tehama”, alisema Bi. Chaula.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo Mkuu wa Kitengo cha Tehama wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Raymond Machary aliishukuru serikali kwa kutambua na kuthamini huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo kupitia mfumo wa Tehama.

Machary ambaye pia ni mbobezi kwenye tasnia ya Tehama alisema hivi sasa taasisi hiyo imekua ikitoa huduma zake nyingi ikiwemo huduma za wagonjwa kupitia mfumo wa Tehama na kupunguza matumizi ya karatasi.

“Kwa takwimu za wagonjwa wanaofika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa mwezi ni takribani 9000 na zaidi ambapo kwa siku ni wastani wa wagonjwa 300 hadi 500. Kutokana na idadi hii ya wataka huduma kuwa kubwa suala la matumizi ya Tehama halikuweza kuepukika”,

“JKCI pamoja na mambo mengine, ilifanya maamuzi ya kusudi kuwa Tehama itumike katika uendeshaji wa Taasisi hivyo kuifanya kuwa chachu ya kuboresha huduma zinazotolewa, haikuwa kazi kubwa kwa Idara ya Tehama kuhakikisha Tehama inatumika kwenye maeneo yote ya ofisi hivyo kurahisisha huduma na kupunguza gharama za karatasi na muda”, alisema Machary.

Aidha Machary alisema kuwa kutokana na mwamko mkubwa wa matumizi ya Tehama, Idara ya Tehama iliweza kuandaa mifumo mingi ambayo inatumika hadi sasa na Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na mfumo wa utoaji wa huduma za kitabibu (eHealth), usimamizi wa vifaa na madawa, mfumo wa kukusanya changamoto za mifumo, mifumo kwa ajili ya tafiti ndogo ndogo, pamoja na mfumo wa kukusanya changamoto za wagonjwa.

“Mifumo iliyopo mingi iliandaliwa na wataalamu wa ndani kulingana na mahitaji yetu, mifumo yote iliyoandaliwa imeleta mafanikio na tija kubwa kwa Taasisi yetu”,

“Mafanikio haya yote ni kutokana na dhamira ya serikali kuona umuhimu wa Tehama, tunaishukuru sana Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, tume ya Tehama, Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto na Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kushirikiana na Taasisi yetu kuongeza ubunifu katika kutoa huduma bora kwa watanzania”, alisema Machary.


MWISHO –

No comments: