Advertisements

Thursday, January 27, 2022

WACHIMBAJI WADOGO HUTUMIA TANI 18.5 ZA ZEBAKI KWA MWAKA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Bw. Edward Nyamanga akifungua warsha ya mafunzo kwa wakaguzi wa mazingira jijini Dodoma yenye lengo la kutoa mbinu za kuboresha utendaji wa kazi katika kusimamia matumizi ya Zebaki kwenye maeneo ya wachimbaji.
Mkurugenzi wa Tafiti na Usimamizi wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Medard Jangu akitoa mada wakati wa warsha ya mafunzo kwa wakaguzi wa mazingira jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Bw. Edward Nyamanga (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya mafunzo kwa wakaguzi wa mazingira jijini Dodoma. Wengine kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Danstun Shimbo na Mkurugenzi wa Tafiti na Usimamizi wa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Medard Jangu.

(PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais-Mazingira, Bw. Edward Nyamanga amesema sekta ya wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini hutumia zaidi ya tani 18.5 za Zebaki kwa mwaka.

Nyamanga amebainisha hayo wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa wakaguzi wa mazingira jijini Dodoma yenye lengo la kutoa mbinu za kuboresha utendaji wa kazi katika kusimamia matumizi ya Zebaki kwenye maeneo ya wachimbaji.

Alisema kuwa kiwango hicho cha Zebaki ambacho hutumika bila kuzingatia tahadhari kinaweza kusababisha athari kwa afya ya binadamu na mazingira na hivyo kuathiri ustawi wa maendeleo endelevu ya nchi.

Alitaja madhara makubwa ya kiafya yanayosababishwa na kemikali hiyo ni ni pamoja na magonjwa ya Minamata ambayo yanajumuisha kuathirika kwa mfumo wa neva za fahamu, kukosa nguvu, misuli kulegea, figo kuathirika na uono hafifu.

Mengine ni kupoteza uwezo wa kusikia na kuongea, mimba kuharibika, kupoteza kumbukumbu, kukosa usingizi kwa muda mrefu, kiharusi na hatimaye vifo.

Naibu Katibu Mkuu huyo alifafanua kuwa Zebaki ni moja ya kemikali hatarishi inayosababisha athari kwa afya ya binadamu na mazingira Duniani.

“Kutokana na athari hizo pamoja na utafiti wa zaidi ya miaka 50 katika maeneo mbalimbali duniani, ilibainika kuwa athari za uchafuzi unaotokana na Zebaki kwa afya ya binadamu na mazingira ni moja ya changamoto za uchafuzi wa mazingira duniani, hivyo, Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki ulianzishwa na kupitishwa mwaka 2013 na Tanzania iliuridhia,” alisema.

Alisema katika kutekeleza mpango-kazi wa Mkataba wa Minamata, Serikali iliandaa Mradi wa miaka mitano wa kupunguza au kuondosha kabisa matumizi ya Zebaki kwenye uchimbaji mdogo wa dhahabu hapa nchini (EHPMP) ambao utatekelezwa katika mikoa saba ya kimadini yenye wachimbaji wadogo wengi wa madini ya dhahabu.

Mikoa hiyo ni Geita, Mwanza, Mara, Shinyanga, Singida, Mbeya na Songwe ambapo ulisainiwa Oktoba 19, 2020 kati ya Benki ya Dunia na Serikali ya Tanzania na kuanza rasmi utekelezaji wake tarehe Oktoba 26, 2020 ukishirikisha Taasisi na Wizara za Kisekta zinazohusika na usimamizi na udhibiti wa Zebaki nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira, Dkt. Andrew Komba alisema lengo la warsha hiyo ni kuwajenga uwezo wakaguzi wa mazingira na migodi katika kusimamia masuala mbalimbali ya hifadhi na usimamizi wa mazingira ikiwemo utekelezaji wa Mikataba ya Minamata na Basel; pamoja na utekelezaji wa Mpango-Kazi wa Taifa wa Kupunguza Matumizi ya Zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu.

Akizungumza kwa niaba ya Dkt. Komba, Afisa Mazingira, Mhandisi Onesphory Kamukuru alisema warsha hiyo ina jumla ya washiriki 60 kutoka Wizara na Taasisi za Kisekta zinazohusika na usimamizi wa Zebaki nchini.

Pia inajumuisha watalamu na wakaguzi wa Mazingira na migodi kutoka Mikoa mikoa saba ya kimadini, maafisa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, wakaguzi wa mazingira na migodi kutoka Tume ya Madini, Maafisa mazingira kutoka NEMC na waandishi wa habari.

No comments: