Advertisements

Sunday, May 22, 2022

WAZIRI MULAMULA AFANYA ZIARA KATIKA MAHAKAMA YA KIMATAIFA YA KESI MASALIA ZA MAUAJI YA KIMBARI (IRMCT)


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (kulia) akifafanua jambo wakati wa kikao na Uongozi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari kilichofanyika tarehe 21 Mei 2022 katika eneo la Lakilaki, jijini Arusha. Pembeni ya Mhe. Waziri ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Caroline Chipeta.
Kutoka kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (IRMCT) Bw. Abubaccar Tambadou na Jaji wa Mahakama hiyo Mheshimiwa William Sekule akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mahakama kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula.
Ujumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulioambatana na Mhe. Waziri katika ziara hiyo ukifatilia majadiliano katika kikao hicho. Kushoto ni Msaidizi wa Mhe. Waziri, Bw. Seif Kamtunda na Kulia ni Afisa Mambo ya Nje, Bi. Laila Kagombora.
Uongozi wa Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (IRMCT) ukifatilia majadiliano ya kikao.
Kikao kikiendelea
Picha ya Pamoja Waziri Mulamula na Msajili wa Mahakama Bw. Tambadou na Mhe. Jaji Sekule.
Picha ya pamoja ujumbe wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Mhe. Waziri Mulamula na Uongozi wa IRMCT.
Waziri Mulamula akipata maelezo katika chumba cha Mahakama na taratibu nyingine za uendeshaji wa kesi katika mahakama hiyo.
Muonekano wa chumba cha Mahakama.
Waziri Mulamula akipata maelezo kutoka kwa afisa anayesimamia Makavazi (Archieve) ya mahakama hiyo.
Waziri Mulamula akipata ufafanuzi juu ya uendeshaji na usimamizi wa Makataba inayosimamiwa IRMCT ambapo alielezwa kuwa hadi sasa Makataba hiyo inashirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Makumila kutoka Tanzania na Chuo Kikuu cha Makelele kutoka Uganda.
Picha ya pamoja Mheshimiwa Waziri na Watanzania wanaofanya kazi IRMCT

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya ziara ya kikazi katika Mahakama ya Kimataifa ya Kesi Masalia za Mauaji ya Kimbari (IRMCT) tarehe 21 Mei 2022 katika eneo la Lakilaki, jijini Arusha.

Pamoja na mambo mengine dhumuni la ziara hiyo lilikuwa kukutana na Uongozi wa IRMCT na kujadili utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kimsingi unaofanywa na taasisi hiyo sambamba na yale ya kimahakama.

Waziri Mulamula alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa Tanzania inathamini imani inayotolewa na mashirika ya kimataifa pamoja na kikanda ya kuifanya kuwa mwenyeji wa mashirika hayo na kutoa nafasi za ajira kwa Watanzania.

‘’ Serikali inafuatilia kwa karibu utendaji kazi wa Mahakama hii, hivyo ni vema mkatekeleza kwa tija malengo mahsusi ya kuanzishwa kwake,” alisema Balozi Mulamula.

Pia akasisitiza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano wa kiutendaji wakati wowote itakapohitajika ili kuiwezesha Mahakama kutekeleza majukumu yake ya msingi ikiwemo kukamilisha taratibu za kesi zilizosalia na lile la kuwa kituo cha kumbukumbu kwa kesi hizo linatekelezwa kwa ufanisi.

Naye Msajili wa Mahakama hiyo Bw. Abubaccar Tambadou amemshukuru Mheshimiwa Waziri Mulamula kwa kuthamini Mahakama hiyo na kutenga muda wake kujadili masuala mbalimbali ya kiutendaji.

Pia akaeleza kuwa kikao hicho kimewezesha kupatikana kwa ufumbuzi wa papo kwa papo katika baadhi ya mambo na kuleta uelewa wa pamoja kati ya uongozi wa Mahakama na Serikali mwenyeji juu ya masuala ya kiutendaji wa taasisi hiyo.

Naye Jaji wa Mahakama hiyo Mheshimiwa William Sekule alifafanua kwa kina juu ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kimahakama na pia akaeleza kuwa kufanikiwa kwa Mahakama hiyo kunahitaji msaada kutoka kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na nchi mwenyeji katika kutetea maslahi mbalimbali kwa ajili ya kuwezesha uendeshaji wa shughuli za taasisi.

‘’Naipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kupigania upatikanaji wa bajeti ya uendeshaji wa Mahakama, hivyo ni vema tukatambua thamani ya mahakama hii kuendelea kuwepo nchini na kukamilisha majukumu yake,” alisema Jaji Sekule.

Tangu Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe Azimio Nambari 1966 mwaka 2010 la kuanzisha Mahakama hiyo nchini, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilisimamia hatua mbalimbali za awali ili kuhakikisha ujenzi wa Mahakama hii unakamilika hususan upatikanaji wa eneo la ujenzi, uwepo wa huduma ya umeme, barabara na maji katika eneo la Lakilaki Jijini Arusha.



No comments: