Advertisements

Friday, July 1, 2022

NAIBU WAZIRI ASUSIA TAASISI YA CHAKULA NA LISHE, AWAONYA KUTOTUMIA FEDHA ZA WADAU VIBAYA

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ameitaka Taasisi ya chakula na lishe Tanzania (TFNC) kuacha kufanya shughuli zake mjini na badala yake wawafikie wananchi wa vijijini na kutumia vizuri fedha za wadau.

Dkt. Mollel amesema hayo leo leo tarehe 30/6 /2022 wakati akimuwakilisha Waziri wa afya Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa Makala ya siku ya afya na lishe Kijijini uliotarajiwa kufanyika jijini Dodoma.

Katika uzinduzi huo ambao Naibu Waziri hakuuzindua kutokana na kuwepo na dosari badala yake alichukua nafasi hiyo kuelimisha taasisi hiyo pamoja na wadau waliohudhuria waweze kufanya miradi ya lishe ikiwemo uzinduzi wa shughuli ambazo zinalenga jamii moja kwa moja zifanyike huko huko na sio mijini.

“Suala la lishe ni nyeti sana kwani linabeba afya za wananchi, nimekataa kuzindua leo kwa sababu Makala hii ilitakiwa izunduliwe kijijini kwa walengwa na sio Dodoma. Tulitegemea hawa wenzetu wangepeleka hili suala katika Kijiji ambacho kimeathirika zaidi kwa lishe duni”. Amesema Dkt. Mollel.

Aidha, Dkt. Mollel ameongeza kuwa lishe ni suala la kitaifa ambalo linatakiwa liwashirikishe viongozi wa eneo husika, madiwani, wabunge pamoja na viongozi wa Serikali ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi za lishe bora na elimu ya vyakula vya lishe ambavyo vinapatikana katika maeneo yao.

Dkt. Mollel amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele katika uboreshaji wa huduma za afya ikiwemo masuala ya lishe hivyo amewataka kila mmoja kuchukua hatua katika upande wake ili kumuunga mkono Rais.

Kufuatia hatua hiyo, taasisi ya TFNC pamoja na wadau wamekubali kurekebisha makosa yaliyofanyika pia wameahidi kuweka mikakati ya kutoa huduma zitakazowagusa wananchi moja kwa moja mahali walipo.

No comments: