Advertisements

Wednesday, May 31, 2023

WAANDISHI WA HABARI WATAKIWA KUENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU CHANJO


Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuwapeleka watoto kupata chanjo mbalimbali zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya afya.

Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume wakati wa semina kwa waandishi wa habari wa Mikoa ya Mtwara, Lindi Pwani na Morogoro iliyofanyika kwenye ukumbi wa Anatoglo jijini Dar es Salaama.

Dkt. Mfaume amesema waandishi wa habari ni muhimu katika kuhamasisha masuala yote ya afya hususani chanjo ili kuweza kuwakinga watoto magonjwa yanayozuilika kwa chanjo.

Ameongeza kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha huduma za chanjo zinapatikana kila mahali ikiwemo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

"Tunamshukuru Rais wetu kwa uwekezaji mkubwa kwa sekta hii kwa upande wa chanjo tumepata majokofu yanayotumia nishati ya jua hakuna sababu tena ya kituo kukosa chanjo kwa sababu hii".

Aidha, amesema Mkoa wa Dar es Salaam wamepatiwa magari ya chanjo na hivyo kurahisisha utoaji wa chanjo na kuwafikia watoto wote wanaolengwa kupata chanjo hizo.

Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo umetoa mafunzo kwa waandishi wa habari lengo ni kuwafikia waandishi wa mikoa yote Tanzania.

No comments: