Monday, March 14, 2011

Mwalimu awachapa wanafunzi kwa waya

SHULE ya Msingi Bunge ya jijini Dar es Salaam imeingia katika kashfa baada ya mmoja wa walimu wake, kudaiwa kuwachapa wanafunzi kwa waya wa transfoma huku uongozi wa shule hiyo ukielezwa kuwanyima wachelewaji haki ya kuhudhuria masomo, kama njia ya kuwaadhibu. 

Kwa mujibu wa habari kutoka vyanzo mbalimbali shuleni hapo, wakiwemo baadhi ya wanafunzi waliowahi kuadhibiwa kwa staili hiyo inayopingana na maelekezo ya Serikali juu ya adhabu sahihi kwa wanafunzi wakosaji shuleni, idadi ya viboko wanavyochapwa huongezeka kulingana na siku waliyotenda makosa. 


Vyanzo hiyo vilimtaja Mwalimu Preygod Issaya (23) anayefundisha Hisabati katika mkondo A na B katika darasa la sita, kuwa ndiye mwenye tabia ya kuwachapa wanafunzi wanaotenda makosa mbalimbali kwa kutumia waya huo wa transfoma. 

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hadija Telela ndiye anayetajwa kuanzisha, kubariki na kusimamia zoezi la kurejeshwa nyumbani kwa watoto wanaofika shuleni hapo wakiwa wamechelewa nyakati za asubuhi. 

Inadaiwa Mwalimu Issaya, bila kujali umri au darasa la mwanafunzi anayemwadhibu, humchapa viboko kuanzia vitatu iwapo ametenda kosa Jumatatu na idadi ya viboko hivyo huongezeka hadi kufikia saba kwa Ijumaa. 

“Ukitenda kosa siku ya Jumanne, unachapwa viboko vya waya vinne, vivyo hivyo hadi Ijumaa. Jumamosi tunakuja shule, lakini huwa hatuchapwi,” alieleza mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo na kufafanua kuwa hurudishwa nyumbani wanapochelewa bila kuzingatia ulitumia usafiri wa daladala au wa mabasi ya wanafunzi kufika katika shule hiyo iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam. 

Gazeti hili lilifika shuleni hapo mwishoni mwa wiki na kukutana na walimu waliohusishwa na kashfa hiyo mbele ya Mwalimu Mkuu Msaidizi, Christina Wambura na Katibu wa Taaluma wa shule hiyo, Saumu Athumani, walioshirikishwa kwenye mahojiano hayo na mwalimu mkuu mwenyewe aliyekiri kuwepo kwa utaratibu wa kuwarudisha nyumbani wanafunzi wanaochelewa na kuutolea ufafanuzi. 

Katika kikao hicho kilichofanyika ofisini kwa Mwalimu Telela, Mwalimu Mkuu huyo alimtaka Issaya kueleza jambo juu ya tuhuma zinazomkabili mbele yake na walimu wenzake wawili ili asikie kutoka kwenye mdomo wake mwenyewe kwa maelezo kuwa zilikuwa hazijaifikia ofisi yake. 

“Nimewaita hapa ghafla kwa sababu kuna tuhuma zimenifikia kutuhusu sasa, sikutaka kufanya mambo haya kiholela kwa kuyatolea majibu tu wakati wahusika wote tupo,” alieleza Telela na kuongeza: 

“Sasa nafikiri itakuwa vizuri tukamsikia mwalimu Issaya mwenyewe akieleza kama kweli anachapa wanafunzi kwa waya wa transfoma au anasingiziwa ili tumtendee haki ili na mimi nifafanue, pia kuhusu kuwarudisha wanafunzi nyumbani wanapochelewa,” alisema Telela. 

Alipotakiwa kujieleza, Mwalimu Issaya alisema, “Taarifa kuwa ninawachapa wanafunzi kwa kutumia waya wa transfoma sio za kweli kwa sababu waya ninaoutumia mimi kuwachapa wanapokosea ni wa antenna ya TV, unaotumika kusaidia kunasa chaneli mbalimbali kwa kuwekwa huko juu (alikuwa akitoa maelezo hayo huku akionesha kwa mikono mahali zinapotundikwa waya za aina hiyo). 

“Nimefanya hivyo mara mbili tu nakumbuka kwa watoto saba wa darasa la tano waliokuwa wakipiga kelele kule darasani kwao, na wanafunzi wa darasa la sita waliokuwa wameshindwa kukamilisha kazi niliyowapa Jumatatu moja hivi,” alieleza mwalimu huyo mbele ya wenzake. 

Mwalimu Issaya aliyeajiriwa kufanya kazi hiyo mwaka 2008 ikiwa ni ajira yake ya kwanza akitokea Chuo cha Ualimu Bustani wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, alisema uamuzi wa kutumia waya kama fimbo, aliupata baada ya kuona wanafunzi wanaendelea kukosa wanapochapwa kwa fimbo za miti. 

“Nilichukua uamuzi huo kwa nia njema nikidhani ninawasaidie ili wajirekebishe kwa sababu wanaendelea kutomaliza kazi zangu na kupiga makelele hata nikiwachapa kwa fimbo za miti…nia yangu ilikuwa kuwarekebisha na si kuwaumiza,” alijitetea mwalimu huyo. 

Naye Mwalimu Mkuu Telela alisema adhabu ya kuwarudisha wanafunzi nyumbani huitekeleza siku za mwanzo wa kufungua shule, baada ya likizo ndefu kwa nia ya kuwakumbusha madereva wajibu wa kuwawahisha wanafunzi shuleni. 

“Sio utaratibu rasmi kwa kweli na zaidi tunaufanya kwa wanafunzi wanaoletwa na mabasi yanayobeba wanafunzi yanayomilikiwa na watu binafsi…siku zote tunapofungua shule wanakuwa wakilegalega na kuwaleta watoto baada ya saa mbili sasa mimi huwa ninawarudisha na wanafunzi waliomo ndani na kuwaamuru wawafikishe kwenye vituo walipowatoa ili iwe fundisho,” alisema Telela. 

Alisema anapofanya hivyo hawi na makusudi ya kuwanyima haki ya kusoma wanafunzi wanaorejeshwa nyumbani, bali lengo lake ni kuwaadhibu madereva wazembe. 

“Masomo yanayopotea huwa tunayafidia kwenye muda wa vipindi vya ziada ambayo huanza baada ya saa nane kila siku na Jumamosi…ni utaratibu wetu sisi hapa na wala haujaelekezwa kutoka mahali kwingine kokote”. 

Gazeti hili lilielezwa kuwa huduma hiyo ya usafiri inalipiwa Sh 30,000 kwa mwezi na kila mwanafunzi anayeitumia na wanafunzi wanaochelewa huachwa vituo vya basi bila barua kutoka kwa uongozi wa shule zinazowaarifu wazazi juu ya uamuzi huo na hivyo kuwaacha bila taarifa za watoto wao kukosa masomo. 

Mwaka 2006, wakati wa Bunge la Bajeti mjini Dodoma, aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza alikataza adhabu ya viboko kwa wanafunzi isiyozingatia utu na kutoa mwongozo wa Serikali kwamba inapolazimika, wachapwe viboko viwili kwenye makalio.


CHANZO:HABARI LEO

2 comments:

  1. Hii yote ni upuuzi mtupu, huyu mwalimu mkuu ni mpumbavu kwisha kazi, utawaadhibu vipi madereva kwa kuwarudisha wanafunzi nyumbani na kuwakosesha masomo, mimi nadhani anawaadhibu wanafunzi na siyo madereva, eti ni nia ya kuwakumbusha madereva wajibu wa kuwawaisha wototo shule!!!!
    Na huyu mwalimu anayetumia waya, mimi kama ingekuwa uwezo wangu, angekuwa wa mfano kwa walimu wote wengine wapumbavu kama yeye, hapa naomba nisieleweke vibaya, najua kuna walimu wengi wazuri na wenye nia njema kabisa ambao wanafanya kazi yao katika mazingira magumu bila vitendea kazi muafaka, lakini juu ya yote haya bado haiwapi haki ya kuchapa wanafunzi wanavyojisikia tu. Mimi nakumbuka mwalimu mmoja alikuwa anamfinya mwanafunzi huku akimwambia "MUONE SURA KAMA MAMA YAKO" sasa unajiuliza mama wa huyu mwanafunzi amekosa nini, hata kama huyu mwanafunzi alifanya kosa, basi huna haja ya kumuingiza mama yake, na swali jingine ni je hiyo sura ni mbaya kama mama yake au ni nzuri kama mama yake!!!! sote tunajua alikuwa akimaanisha ni mbaya!!!

    ReplyDelete
  2. Safi sana!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake