Saturday, February 25, 2012

Mjibu mpenzi wako maswali haya kwa vitendo - 3

NAAM! Tumekutana tena kwenye kona yetu, nina imani kwa uwezo wa Mungu wote mu wazima wa afya.  Leo tunamalizia mada yetu inayochukua wiki tatu sasa. Maswali gani ambayo unatakiwa kumjibu mwenzako ambayo huwa vigumu kuyasema kwa mdomo. 


Baada ya kutambua maswali, nini cha kufanya?
Unapoanzisha uhusiano unatakiwa kumsoma mwenzako anapenda nini na kipi ambacho hakipendi. Vichukue vyote kisha kaeni chini na kuchambua kimoja baada ya kingine. Angalia mifano ifuatayo:
Mosi
Mpenzi wako anapenda baada ya kazi muwe pamoja, je, kwa upande wako nini kinakufanya usiwe pamoja na mwenzako? Kama kina sababu ya msingi basi kaeni chini na kujadiliana bila kutumia mabavu.

Pili
Mpenzi wako huenda anapenda muoge na kula chakula cha usiku pamoja, kuna sababu ya kukuchelewesha? Kama hakuna ni nafasi nyingine ya kuongeza upendo ndani ya nyumba.
Mara nyingi wafanyakazi huwa mbali na wapenzi wao kwa muda mwingi, lakini inapotokea unaoga na kula pamoja na wenzako, hali hiyo usababisha kuondoa upweke na kumfanya mwenzio ajione upendo wako kwake bado upo juu.
Kumekuwa na matatizo mengi katika uhusiano kwa wanaume wengi kuamini fedha ni kila kitu. Unaweza kumpa kila kitu mkeo kwa kumnunulia nguo, vyakula na kuhakikisha hana shida, lakini huna muda wa kukaa naye badala yake mawazo na akili vyote vipo kwenye kutafuta fedha na kusahau mwenzako naye anakuhitaji.
Hivyo basi pamoja na ugumu wa kazi unatakiwa kutenga muda angalau saa mbili ili kuzungumza na kubadilishana mawazo ikiwemo kula na kuoga pamoja. Siyo kumkuta kitandani na kumuacha kitandani.

Tatu
Mpenzi wako anahitaji umuonyeshe unakijali chochote anachokupatia, kumekuwa na tabia za baadhi ya wanawake kutoshukuru zawadi zisizowafurahisha. Hii inapunguza upendo na kumfanya mwenza wako asiwe na hamu ya kukuletea kitu kwa kuhofia hutakipenda.
Siku zote onyesha kujali kile unachopewa hata kikiwa kidogo, kufanya hivyo ni kuonyesha unajali na kumfanya mwenzako akuletee kikubwa zaidi.

Mwisho
Jiepushe kuwa chanzo cha maumivu ya wenzetu, jaribu kuyafanya yote ambayo hayahitaji nguvu wala fedha kumfurahisha wenzako. Mpende mwenzako kwa vitendo kwa kuyafanya zaidi anayoyapenda na kuyaacha asiyoyapenda.
Muonyeshe unamjali kwa kuwa naye karibu hata kumshirikisha katika mambo yanayowahusu, kwani mwenzako ni sehemu yako, hivyo, ushauri wake ni muhimu. Kama utakuwa umefuatilia tangu mwanzo wa mada hii, nina imani nimeeleweka, kilichobakia ni utekelezaji.

Leo inatosha tukutane wiki ijayo.

www.globalpulishers.info

1 comment:

  1. Tunapendana sana na mpenzi wangu ila tatizo ni kuoga pamoja, hapo imenigusa mimi, napenda nimuogesha mpenzi wangu kama mtoto mdogo, nimuondoe stress za siku nzima. Mkishakuwa wapenzi haikuna aibu. Na pia inadumisha mapenzi na upendo.

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake