Wednesday, February 22, 2012

Mtendaji Kata amtunishia msuli DC

Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa. 


KATIKA hali isiyo ya kawaida Mtendaji wa Kata ya Nondwa katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma,amemtunishia msuli Mkuu wa Wilaya hiyo, Betty Mkwasa. 

Hali ilitokea baada ya Mkwasa kuhoji ni kwa nini kata hiyo ya Nondwa haijachangia ujenzi wa shule ya sekondari na kusababisha watoto waliofaulu katika kata hiyo kupelekwa kusoma kata nyingine. 

Mtendaji huyo, Yoram Ndahani baada ya kuhojiwa aliinuka na kujibu kwamba yuko tayari kuchukuliwa hatua yoyote kwani hakuwa na maelekezo ya michango ya namna hiyo.
 

Hali hiyo ilifanya Mkuu wa Wilaya kuinuka na kumhoji kiongozi kwa nini anajibu jeuri kwani alikuwa na haki ya kuulizwa juu ya utendaji wake. 

"Usipende kudharau wanawake, sizungumzi kama mwanamke nazumgumza kama kiongozi tena ni Mkuu wa Wilaya, lakini najua angekuja Mkurugenzi hapa usingemjibu hivi kwa vile anakulipa mshahara,” alisema Mkwasa na kuongeza: “Utambue kuwa hata huyo Mkurugenzi 
anaripoti kwangu na angekuwa kiongozi mwingine hapa wewe usingebaki hapa angeenda kukutupa mahabusu ujifunze namna ya kuzungumza na kumjibu kiongozi wako" . 

Kutokana na hali hiyo, Ofisa Tarafa wa Kata ya Mpalanga Michael Mkunya aliomba radhi kutokana na kauli hiyo huku viongozi wa kata waliokuwepo hapo wakiomba radhi kutokana na kitendo hicho ambacho walikiita kisichopendeza. 

"Kazi ya kiongozi ni kuelekeza, suala la msimamo linatupa shida kidogo kama ni suala la msimamo wa kisiasa ijulikane wakati mwingine anapofika kiongozi mkuu kubali kuelekezwa na 
si kubishana," alisema Katibu Tarafa. 

Mkuu wa Wilaya huyo alikuwa katika ziara ya kutembelea shule tano za sekondari za Tarafa ya Chipanga ili kuonana na walimu waliopangiwa kufundisha katika shule hizo na idadi ya wanafunzi walioripoti kuingia kidato cha kwanza. 

Mtendaji alidai kuwa hakuna kiasi kilichochangishwa kwani hakukuwa na maelekezo yoyote ya uchangishaji. 

"Mna matatizo gani mpaka msome katika kata nyingine? Najiuliza kwa nini watoto wenu wakasome kata nyingine? 

Kwa nini Nondwa hamjachangia ujenzi wa sekondari wakati mnajua azma yetu ni kila kata isimamie uchangishaji, sasa kuna faida gani kuwa na viongozi ambao hawataki maendeleo?” alihoji. 

Alisema kuwa, kila mmoja ni lazima atambue kuwa kipaumbele cha kwanza ni elimu lakini katika kata hiyo kila siku imekuwa na tatizo la uwajibikaji kwa viongozi wake . 

"Hivi Diwani wa hapa anatekeleza Ilani ya chama gani, nina wasiwasi hatekelezi ilani ya CCM, kwani CCM inaimba wimbo mmoja tu wa maendeleo, siwalaumu wananchi nawalaumu sana viongozi hasa Diwani kwani ni Mwenyekiti wa Maendeleo ya Kata alipaswa kusimamia," alisema. 

Aidha, alivitaka vijiji viwili vya Kata ya Chifutuka, ambavyo ni Chifutuka na Magaga kujenga darasa moja na vijiji viwili vya Kata ya Nondwa ambavyo ni Nondwa na Zejele kujenga darasa 
moja ili watoto wasome karibu na si kutembea umbali mrefu kufuata shule. 

Awali Ofisa Mtendaji wa Kata ya Chifutuka, Gasper Ernest alisema kuwa, walijipanga kila kata kuchangia ujenzi wa shule lakini Kata ya Nondwa ilikataa kuchangia hali iliyofanya kasi ya utekelezaji kuwa ndogo.



Habari Leo

2 comments:

  1. Hapa hata Mkuu wa Wilaya alikosa busara. Iwapo anahisi kudharauliwa asingekimbia kujikinga kwa kudai amedharauliwa kwa kuwa yeye mwanamke! Alipaswa kumdharau huyo Bwana kwa kuhimiza agenda yake na baadae kumrudi kwa kupitia viongozi wake. Kujigamba kwamba hata huyo Mkurugenzi yeye in Boss wake in kuonyesha kukosa kujiamini kwa kiongozi!

    ReplyDelete
  2. Betty Mkwasa ameonyesha udhaifu... kiongozi haishi kwa assumptions bali evidence. Amejuaje amemdharau kwavile ni mwanamke?

    ReplyDelete

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake